Euro 2024 ni darasa kwa AFCON

ULAYA na dunia kwa sasa inashuhudia fainali za Kombe la Mataifa ya Ulaya ‘Uefa Euro 2024’ zinazoendelea Ujerumani zikishirikisha nchi 24 na sasa zimeingia raundi ya p[ili hatua ya makundi.

Fainali hizi au European Championship Cup ni moja ya fainali kubwa duniani baada ya zile za Kombe la Dunia na zilianzishwa mwaka 1958, zikishirikisha mataifa mengi ya Ulaya Magharibi.

Fainali hizi zimekuwa na mafanikio makubwa kibiashara na katika kufuatiliwa na inadaiwa zinatazamwa na takriban watu milioni 500.

Fainali hizi ambazo hufanyika kila baada ya miaka minne bila  kuingiliana na zile za Kombe la Dunia la Fifa, ni mara chache sana hazikufanyika kwa sababu kubwa kama janga la ugonjwa wa Corona (Uviko19).

Kutokana na fainali hizi, mabara mengine kama Afrika, Amerika Kusini na Kaskazini, Asia na Oceania yalianzisha za kwao.

Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), zilianzisha miaka ya 1950 zikishirikisha mataifa huru ya Afrika na hivyo kuitwa kombe la mataifa huru ya Afrika na yaliyokuwa hayajapata uhuru kutoka ukoloni hayakushiriki fainali hizo.

Afcon zinaendesha na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), hufanyika kila baada ya miaka miwili na kalenda yake imekuwa ikigongana na ile ya Fifa na vyama vingine, hivyo wakati mwingine kuleta mgongano na klabu hasa za nje ya Afrika, kwani huwa zinasita kuwaachia wachezaji katikati ya msimu wa ligi zao.

Pia mara kadhaa Afcon zimeahirisha kutokana na wenyeji kutokuwa na miundombinu sahihi au matatizo ya kiusalama na kisiasa.

Nadhani ni wakati wa Caf kuangalia kalenda yake ili fainali hizi ziwe na maana na ikiwezekana zifanyike kila baada ya miaka

minne au hata mitatu katika kalenda ambayo haigongani na fainali za Kombe la Dunia.

Kwa idadi ya timu 24 zinazoshiriki Afcon, miaka miwili ni michache tofauti na zilipokuwa timu nane tu.

Fainali zinafanyika wakati ligi imesimama na wachezaji wako huru kuonyesha uwezo wao.

Kumekuwa na tuhuma mbalimbali kuhusu wachezaji wa Kiafrika kutoonyesha uwezo wao kwenye Afcon.

Si nia yangu kusema fainali za Afcon siyo nzuri, hapana, lakini ukweli Afrika bado ina safari ndefu ya mafanikio wakijifunza kutoka kwa wazoefu na waliofanikiwa.

Mwandishi wa makala haya ni Katibu Mkuu mstaafu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Related Posts