Unguja. Hoja ya ulinzi, usalama na amani inatarajiwa kuchukua nafasi kubwa wakati wa mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani unaotarajiwa kufanyika Oktoba nchini Uswis.
Mbali na hoja hiyo, mengine yanayotarajiwa kujadiliwa ni masuala ya akili bandia na mabadiliko ya tabaianchi.
Akizungumza leo Juni 20, 2024 baada ya kukamilisha kikao cha Kamati Tendaji ya IPU, Rais wa IPU Dk Tulia Ackson amesema kamati hiyo imeamua ajenda hizo ziwe kubwa katika mkutano huo na ule utakaofanyika mwakani.
“Tukianza kujadili vita, watu huwa tunakimbilia mashariki ya kati, upande wa Ukraine na Russia lakini zipo nchi zingine za Afrika ambazo zina changamoto kubwa ya vita, kwa hiyo tumependekeza tutajadili hatua zinazochukuliwa na kuzishauri nchi zetu kuwekeza katika masuala ya ulinzi, usalama na amani,” amesema Dk Tulia ambaye pia ni Spika wa Tanzania.
Kwa hiyo tunatamani tutakapokuwa tunajadili suala hili la amani na usalama, tutaangazia maeneo yote yenye changamoto na changamoto hizo, zitatazamwa kwa mapana yake ili vita vipya vinapoibuka watu wote tunaelekeza nguvu kwenye huko na kusahau vingine vyote kwamba vinaleta athari kwa binadamu.
Amesema jambo mojawapo kubwa, ni hoja ya akili mnemba (bandia) kwa kuendelea kufanya utafiti kwenye eneo hili kwa sababu linaleta maendeleo upande mmoja, upande mwingine linaleta changamoto kwa sababu mtu anaweza kuelewa ni kitu halisi.
“Mtu anaweza kujibadilisha akasema mie ndio spika au ndio Tulia, mtu akakukubali kumbe sio, mambo ya utawala bora na demokrasia ikitumika akili mnemba kwenye uchaguzi inaweza kutengeneza namba, kwa hiyo mazingira kama hayo tumejadili na kuamua kufanyike utafiti zaidi ili maspika watakapokutana mwakani waangalie namna ambavyo kila nchi inachukua jukumu la kufanya utafiti katika eneo hili,” amesema.
Amesema wamejadili namna ambavyo mabunge hayo yanaweza kuzishauri Serikali zao kuwekeza katika eneo hilo ili madhara yasipatikane katika demokrasia, utawala bora na haki za binadamu.
Amesema maamuzi ambayo wamefanya yatasaidia umoja huo kuendelea kupiga hatua mbele na wameangazia sera mbalimbali zinazohusu unyanyasaji wa kijinsia na wanapokutana wanapenda kila mmoja awe na amani.
“Tumepitisha sera mojawapo inayohusu unyanyasaji wa kijisnia kila mtu ajione yupo salama,” amesema.
Kataika hatua nyingine kamati hiyo imetembelea maeneo ya kihistoria kisiwani humo, hatua itakayowanya wawe mabalozi wazuri watakaporejea kwenye mataifa yao na kuwashawishi kuja kutembelea Zanzibar.
Spika Tulia amewataka Watanzania waendelee kuvitunza vivutio vya utalii ili kuweka historia kwa ajili ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
Kuhusu suala la mabadiliko ya tabianchi, amesema litajadiliwa na kuangazia miakati inayotakiwa kutumika kwenye mataifa hayo kupunguza athari.
Ofisa Masoko wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Juma Rajabu Ussi amesema Serikali imetumia fursa hiyo kuwatembeza wgeni hao ili wawe sehemu ya kuhamsiaha utalii nje ya nchi.
“Wameona watu wa kawaida wanaishi na kusifu amani iliyopo Zanzibar kwa sababu bila amani hata maendeleo hatuwezi kuyapata,” amesema.