Arusha. Kijana Willium Mollel (45) Mkazi wa Kata ya Kiranyi, wilayani Arumeru ameuawa na wananchi wenye hasira kali kwa tuhuma za kuiba mkungu wa ndizi mbichi shambani.
Willium aliuawa kwa kupigwa na wananchi, baada ya kukiri kuitambua kofia yake iliyookotwa shambani eneo la tukio kulikokatwa ndizi usiku wa kuamkia jana.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Juni 20, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema mtu huyo ameuawa jana Juni 19, 2024 asubuhi baada ya kupokea kipigo kutoka kwa watu waliomtuhumu kwa wizi.
“Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru kusubiri taratibu za maziko, huku Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi kuwapata wahusika wa mauaji hayo,” alisema Masejo.
Akizungumzia tukio hilo, mke wa marehemu, Mariam Willium amesema jana Juni 19, 2024 majira ya saa 3 asubuhi walikuja watu watatu nyumbani kwao na kugonga mlango kabla marehemu hajatoka na kuanza kumhoji kabla ya kuondoka naye.
“Tukiwa nyumbani walikuja watu watatu wakagonga mlango na akawafungulia, kisha nilisikia wakimuita pembeni wakaanza kumhoji alikuwa wapi jana usiku, akasema alikuwa nyumbani, wakamuuliza kofia yako iko wapi, akashindwa kujibu,” amesema Mariam na kuendelea;
“Aliponyamaza kidogo, mmoja wa watu waliokuja akiwa ameweka mikono nyuma, kumbe alishika hiyo kofia, ndio akaitoa na kumuuliza hii kofia ya nani? Mume wangu akajibu ni yake, ndipo wakamwambia basi tufuate, wakaondoka naye,” amesema mke wa marehemu.
Amesema baada ya dakika 30 hivi, alisikia kelele barabarani na alipotoka alikutana na watu wanamwambia juu ya mume wake kupigwa.
“Nilipopewa habari hizo, nilikimbilia eneo na tukio lakini nilipofika watu walisema amechukuliwa nikionyeshwa njia walipopita. Hadi nafika nyumbani, nikakuta ameletwa na toroli na kuachwa jikoni akiwa anavuja damu nyingi na anatapatapa,” amesema Mariam.
Amesema alitoka kwenda kuomba msaada wa kumpeleka hospitali lakini aliporudi alikuta mumewe alishafariki, kabla ya polisi kumchukua.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Loserian Kambey amesema kijana huyo maarufu kama “Babu” amekuwa na tuhuma nyingi za tabia ya wizi na ulevi, ndio chanzo cha mauaji hayo.
“Mimi niliona watu wamemshika wanaondoka naye, lakini kwa sababu ya tabia yake ya kulewa mara zote na tuhuma za wizi, sikutaka hata kuingilia ugomvi huo nikijua ni wa kawaida tu, siyo wa kusababisha umauti, maana nilimuonya mara nyingi juu ya tabia zake lakini imekuwa ngumu kubadilika,” amesema jirani huyo.
Hata hivyo, amesema kitendo cha wananchi kuchukua sheria mkononi za kumpiga mtu huyo sio cha kiungwana na kuwataka wananchi kuacha mara moja kujichumia laana za kumwaga damu za watu.