Luis Miquissone atoa neno ‘Thank You’ ya Simba

Baada ya Simba SC kutangaza uamuzi wa kutoendelea na winga, Luis Miquissone, mchezaji huyo amevunja ukimya na kusema kitu juu ya uamuzi huo wa Msimbazi.

Akiwa mubashara kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Miquissone amekiri kufikia maamuzi hayo na Wekundu hao, huku akiwatuliza mashabiki wa Simba SCwaliokuwa wanahuzunishwa na hilo akisema ndio maisha ya soka.

Miquissone, amesema licha ya kuachwa na Simba SC, bado ataendelea kuwa shabiki wa timu hiyo, na kwamba mashabiki wa Simba SC watabaki kama kumbukumbu nzuri moyoni mwake.

“Nimeona nizungumze nanyi hapa kwa Sapraizi, sikuwa nimepanga kufanya hiki, lakini ni vizuri nikaongea nanyi. Kumekuwa na mambo yanayoongelewa ambayo baadhi hayakunifurahisha,” alisema Miquissone na kuongeza;

“Ni kweli sitakuwa Simba SC, kama ambavyo klabu imetangaza leo (jana), naomba msiumie. Ndio maisha ya soka yalivyo, mimi nitabaki kuwa shabiki wa Simba SC na mashabiki wa Simba SC nitawakumbuka wakibaki moyoni mwangu.”

Aidha Miquissone akijibu maswali ya mashabiki wakitaka aseme timu atakayokwenda, wengine wakimhoji kama ataibukia Yanga SC, lakini winga huyo amesema hataendelea kucheza soka Tanzania.

“Hapana sitacheza tena Tanzania, nimeshaondoka huko hivi sasa ninavyoongea nanyi, nipo kwangu Msumbiji hapa Tete. Sitacheza timu yoyote Tanzania, mtajua hivi karibuni wapi nitakwenda, nitawatangazia hapa.”

Miquissone anakuwa mchezaji wa nne wa kikosi cha Simba SC kupewa ‘Thank You’ baada ya nahodha John Bocco, Saido Ntibazonkiza na Shaaban Idd Chilunda aliyekuwa akicheza kwa mkopo KMC.

Related Posts