Dodoma. Mahakama Kuu, imewapa kibali, mahakimu watatu wa zamani wa mhimili huo, ili wafungue maombi ya kuomba kurejewa kwa uamuzi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wa kuwafuta kazi na hatimaye kubatilisha uamuzi huo.
Uamuzi wa kuwaruhusu mahakimu hao wa zamani kufungua maombi hayo, ulitolewa Juni 18, 2024 na Jaji Fredrick Manyanda wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma baada ya ‘mahakimu’ hao kuvuka kizingiti hicho cha kwanza.
Watumishi hao wa zamani wa mahakama, Bageni Elijah, Thomas Ochuodho na Nyasige Nyamwaga walifungua maombi namba 7529 ya 2024 dhidi ya Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mtendaji Mkuu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Pamoja na maombi mengine, waliiomba mahakama ikubali kuwapa kibali kufungua maombi hayo ya marejeo (judicial review) ili kupitia maombi hayo, waombe ubatilishwe kwa uamuzi wa kuwafuta kazi uliofikiwa Desemba 7, 2023.
Walidai kuwa uamuzi wa kuwafuta kazi uliotokana na kile kilichodaiwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama kuwa ni kwa masilahi ya umma, haukuwa na mantiki, ulikuwa kinyume cha sheria, uligubikwa na ukiukwaji wa kanuni na taratibu.
Kupitia maombi hayo, wataiomba mahakama kumlazimisha mjibu maombi wa kwanza ambaye ni Tume ya Utumishi wa Mahakama, kuwalipa mafao yao ikiwamo pia malimbikizo ya mishahara kuanzia Januari 18, 2018 hadi Desemba 7, 2023.
Pia kupitia maombi hayo, watafungua maombi kuiomba mahakama imwamuru mjibu maombi wa kwanza kuwarejesha katika nafasi walizokuwa nazo, kulipa gharama za kesi na kuwapa nafuu yoyote ambayo mahakama itakayoona inafaa.
Kulingana na viapo vyao vilivyoambana na maombi hayo ya kibali, waombaji hao watatu walikuwa waajiriwa wa mjibu maombi wa kwanza kama maofisa wa mahakama wakihudumu kwenye nafasi ya hakimu katika kuhudumu maeneo mbalimbali nchini.
Katika kutekeleza majukumu ya ajira zao, kulijitokeza tuhuma za jinai kuhusiana na vitendo vya rushwa dhidi yao ambazo ziliwafanya washitakiwe kortini na kipindi hicho cha kusubiri maamuzi ya kesi hiyo, waliondolewa kazini.
Kulingana na viapo vyao, katika tarehe za kati ya mwaka 2012 na 2016, kesi hizo zilimalizika na walishinda lakini hata hivyo, vizuizi vilibakia hadi Januari 19, 2018 wakati ajira zao za uhakimu zilipokatishwa kwa masilahi ya umma.
Ilitokea kati ya 2016 na 2023, wakati wakisubiri maamuzi ya mahakama katika kesi ya jinai, ulitolewa ushauri kwa mjibu maombi wa kwanza kuhusu uadilifu na kutovumilia ufisadi hivyo waondolewe kazini hata kama walishinda kesi dhidi yao.
Hivyo waliondolewa rasmi kwenye ajira Novemba 29,2023 na walishangazwa na uamuzi huo kwa kuwa waliona ulikiuka haki ya msingi ya kusikilizwa, upendeleo, ubaguzi na bila kuwalipa mafao yao. Ndipo wakaamua kuomba kibali kortini.
Waliiomba mahakama iwape kibali kufungua maombi ya marejeo kupinga kufutwa kwao kazi waliegemea sababu 11 kuishawishi mahakama iwape kibali ikiwamo kuwa kuondolewa kwao ni kinyume cha sheria.
Pia walisema kuondolewa kwao kunakiuka Katiba ya Tanzania inayotoa takwa la lazima la usikilizwaji wa haki, kwani mjibu maombi wa kwanza alianzisha upya tuhuma dhidi yao na kuzijadili licha ya kwamba mahakama iliwaachia huru.
Jambo lingine ni hawakubaliani na hoja kuwa kitendo cha kuwaondoa kazini kwa madai ya masilahi ya umma kwa maelezo kuwa kitendo cha kufikishwa kwao kortini na kufunguliwa shauri la jinai kinaikosesha jamii imani juu yao.
Walieleza kuwa wakati mjibu maombi akieleza hilo kama sababu za kuwafuta kazi, mahakimu hao katika maombi yao walihoji mbona Hakimu Andrew Siwale na wengine wengi ambao walikumbwa na tuhuma kama hizo walirudishwa kazini.
Katika majibu ya wajibu maombi wakili wa Serikali, Daniel Nyakiha alisema hoja ya kuamuliwa na mahakama ilikuwa ni kama ndio ama la, waombaji wameweza kujenga msingi katika viwango vinavyokubalika kuweza kupewa kibali hicho.
Alijenga hoja kuwa mahakama inaongozwa na sheria, kanuni na misingi ya kisheria na kueleza kuwa ni takwa la kisheria kwa anayeomba kibali ili afungue shauri la marejeo lazima awe na sababu zenye mashiko kuishawishi mahakama.
Wakili Nyakiha alisema ni msimamo wa kisheria kama hakuna sababu za msingi au hazina mashiko ombi hilo linapaswa kukataliwa katika hatua za awali ili kuepuka kuipotezea muda mahakama.
Alisema vipo vigezo vinne ili kuruhusiwa kupewa kibali navyo ni muombaji kuwa na masilahi ya kutosha, kuwe na kesi inayobishaniwa, uamuzi uliofika mwisho na awe amepitia vyombo vyote vya rufaa kazini.
Mathalan, alisema hoja ya waombaji kudai mishahara na haki nyingi ni tuhuma na madai hazikustahili kuwa hoja za kuomba kibali cha kufungua shauri la marejeo, bali ni hoja za madai au mashauri ya kikazi.
Wakili huyo alisema waombaji hao wameshindwa kabisa kujenga msingi wa vigezo ambavyo vingewafanya wastahili wapewe kibali wanachokiomba, hivyo ombi lao mbele ya mahakama hiyo litupwe kwa kuwa halina miguu ya kusimama kisheria.
Jaji Manyanda alisema katika maombi yaliyokuwa mbele yake, wadaawa hawapingani na masharti kuwa muda wa kikomo, kuwepo kwa masilahi, uwepo wa uamuzi wa chombo cha umma na hakuna chombo kingine cha juu cha rufaa.
Kwa mujibu wa Jaji Manyanda, ni hoja ambayo haikubishaniwa na wakili Nyakiha kuwa waleta maombi walifunguliwa mashitaka kortini katika mahakama tofautitofauti kwa makosa ya rushwa na kuachiwa huru kuwa hawana hatia.
Kwamba katika kipindi chote cha kusubiri usikilizwaji na maamuzi ya kesi hizo, walihukumiwa na walistahili kupata mishahara yao licha ya kuachiwa huru, mjibu maombi wa kwanza hakuwarudisha waombaji hao kazini.
Ndipo waombaji pamoja na Andrew Siwale ambaye sio sehemu ya maombi haya, walifungua kesi ya madai namba 15 ya 2018, wakiomba mahakama ibatilishe uamuzi wa kuwafuta kazi kwa kile walichodai ni kwa masilahi ya umma.
Kulingana na Jaji, maombi ya mahakimu hao yalikuwa katika makundi mawili, moja ni kutolipwa mishahara na stahiki nyingine, pili ilikuwa ni malalamiko kuwa uamuzi wa kuwafuta kazi ulikuwa batili na haukuzingatia haki ya asili.
Katika shauri lililokuwa mbele yake, Jaji alisema anakubaliana na wakili wa Serikali kwamba masuala ya kikazi yalipaswa kupelekwa jukwaa tofauti lakini kuna dai la msingi la kuwepo ubatili, kutozingatiwa misingi ya haki ya asili na kanuni.
Pia kulikuwepo na hoja ya ubaguzi, upendeleo na ukandamizaji hivyo kuziamua hoja hizo katika hatua hiyo si sawa kwa kuwa itakuwa ni kama kuamua hoja katika maombi ya msingi ya marejeo itakayofunguliwa na waombaji.
Kwa kuongozwa na mamlaka iliyonayo mahakama katika suala la marejeo ya kimahakama na kwa maoni yake waombaji wametimiza vigezo vya kupewa kibali cha kufungua maombi ya marejeo na mahakama inawapa siku 14 kufanya hivyo.