TIMU ya kikapu ya Mkoa wa Kigoma ilianza vyema mashindano ya Kombe la Taifa kwa kuifunga Mkoa wa Dodoma kwa pointi 49-42, katika pambano kali lililopigwa kwenye viwanja vya Chinangali, mjini Dodoma, huku nyota wa timu hiyo Amin Mkosa akitamba ubora na uzoefu vimewabeba.
Mashindano hayo ya Kombe la Taifa yanashirikisha timu 13 za wanaume kutoka mikoa ya Iringa, Mara, Kilimanjaro, Shinyanga, Unguja, Dodoma, Kigoma, Manyara, Morogoro, Arusha, Mtwara na Rukwa.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka Dodoma, Mkosa alisema ushindi wao huo ulitokana na uzoefu wa wachezaji walionao katika mashindano mbalimbali.
“Tumeamua kurudi nyumbani kupigania mkoa wetu katika mashindano haya, naamini kwa ubora tulionao tunaweza tukabeba kikombe,” alisema Mkosa.
Mkosa anayechezea timu ya Mchenga Stars katika Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), aliwataja baadhi ya wachezaji wao nyota ni Mwalimu Heri, Tyron Edward, Baraka Sadiki na Stanley Mtunguja.
Alisema wachezaji hao wote wanachezea timu ya taifa ya wakubwa isipokuwa Mtunguja anachezea timu ya taifa ya vijana ya umri wa miaka 18.
Katika Ligi ya BDL, alisema mchezaji huyo anachezea timu ya Ukonga Kings na katika Ligi hiyo anaongoza kwa kuasisti mara 89.