KLABU ya Pamba imeanza mazungumzo ya kumpata Kocha wa Biashara United, Amani Josiah kwa ajili ya maboresho ya benchi la ufundi.
Hatua hiyo inajiri baada ya Klabu hiyo iliyopanda Ligi Kuu Bara msimu ujao kumtangaza aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba na Tabora United Mserbia, Goran Kopunovic aliyechukua nafasi ya Mbwana Makata ambaye muda wowote atatua Tanzania Prisons.
Taarifa kutoka ndani ya kikosi hicho zililiambia Mwanaspoti, viongozi wameanza mawasiliano na Josiah ili akawe msaidizi wa Goran kutokana na uwezo aliouonyesha akiwa na Biashara kwani hawana mpango wa kutafuta kocha mwingine nje ya nchi.
“Tuko kwenye mazungumzo na makocha kadhaa lakini Josiah ni miongoni mwao, siwezi kukuhakikishia moja kwa moja kwa sababu bado hatujafikia makubaliano rasmi, muda wowote tutaweka wazi ila kocha wetu msaidizi ni mzawa,” kilisema chanzo hicho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Pamba, Bhiku Kotecha alisema, kwa sasa kinachoendelea ni vikao vya ndani kwa ndani katika timu hiyo na kila kitu kitakapokamilika wataweka wazi ila mashabiki wa kikosi hicho watarajie mambo mazuri.
Kwa upande wa Josiah alipotafutwa na Mwanaspoti alisema, kinachoendelea kwa sasa ni tetesi ila kuna timu nyingi ambazo ameshafanya mawasiliano nazo kwa ajili ya kuzifundisha msimu ujao, japo hajafanya maamuzi ya moja kwa moja wapi anaenda.