Sababu Polisi kumkomalia Dk Nawanda

Dar/Mwanza. Wakati waandishi watatu waliokuwa wakishikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza wakiachiwa kwa dhamana, usiri umeendelea kutanda dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahaya Nawanda kama ameachiwa au anaendelea kushikiliwa.

Waandishi hao, Dinna Maningo, Mwanga Wachu na Costantine Mathias wameachiwa leo Alhamisi, Juni 20, 2024 baada ya kushikiliwa kwa siku kadhaa na jeshi hilo wakidaiwa kusambaza taarifa za siri za jeshi hilo.

Dinna amesema alikamatwa na maofisa wa jeshi hilo, Juni 14, 2024, wilayani Tarime Mkoa wa Mara kisha kusafirishwa hadi Mwanza kuhojiwa kwa kosa la kuchapisha taarifa kwa kutumia nyaraka ya siri ya Jeshi la Polisi.

“Nimefurahi sana kupatiwa dhamana, japo wametuambia tunatakiwa kurudi kesho kituoni, wamebaki na vifaa vyangu ikiwamo simu zangu mbili, Laptop na kamera,” amesema Dinna.

Naye Wachu, alikamatiwa mkoani Dar es Salaam na kusafirishwa hadi Mwanza amesema baada ya kukamatwa na maofisa hao, alifikishwa kituoni hapo na kufanyiwa mahojiano kwa kosa la kuwa na nyaraka za Jeshi la Polisi.

Mathias ambaye amesota rumande kwa siku tano baada ya kukamatwa mkoani Simiyu,  amedai amehojiwa kwa kosa la kusambaza nyaraka hiyo kupitia ‘WhatsApp’ kwenda kwa Mwanga Wachu.

“Wamebaki na simu zangu mbili, laptop na kamera yangu aina ya Nickon D3100 kwa madai kwamba wanaendelea na uchunguzi wao,” amesema Wachu.

Wakati waandishi hao wakiachiwa kwa dhamana, wakili wao Amri Linus amesema tayari mteja wake, Dinna Maningo alikuwa ameshafungua Shauri la Jinai namba 16527/2024 katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza.

Wakili Linus amesema mteja wake alifikia uamuzi huo baada ya kuona danadana za kumpatia dhamana zinakuwa nyingi, hata hivyo ameahidi kuliondoa mahakamani shauri hilo.

“Tulikuwa tumeshafungua shauri mbele ya Jaji A. Matuma kuiomba Mahakama itoe amri kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RC), Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC), RCO, OC-CID, IGP na Attorney General (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) ila tutaliondoa kesho kwa sababu tayari wameachiwa kwa dhamana,” amesema Linus.

Wakati waandishi hao wakiachiwa, ukimya umeendelea kutanda dhidi ya Dk Nawanda, ambaye Juni 11, 2024, Rais Samia Suluhu Hassan, alitengua uteuzi wake wa mkuu wa mkoa.

Ameachiwa au anaendelea kushikiliwa ni moja ya swali lililopo.

Mwananchi Digital limedokezwa na vyanzo vyake kuwa, Dk Nawanda aliyekamatwa na Polisi Juni 13, mwaka huu, kwa tuhuma za kumwingilia kinyume na maumbile mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha St Augustine Mwanza, ndani ya gari lake, ameachiwa kwa dhamana.

Tangu alipokamatwa mchana wa Juni 13, Jeshi la Polisi limekuwa kimya na hata Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa alipotafutwa simu yake iliita bila kupokewa.

Wakati vyanzo hivyo vikieleza hayo, Mwananchi Digital leo Alhamisi Juni 20 2024 imezungumza na msemaji wa jeshi hilo, David Misime juu ya kinachoendelea kuhusu Dk Nawanda, amesema: “subirini.”

Alipoulizwa hadi lini, Misime amesema katika taarifa iliyotolewa awali na jeshi hilo ilielezwa uchunguzi ukiwa tayari taarifa zaidi zitatolewa.

Mwananchi ilipotaka kujua  kwa nini wanaendelea kumshikilia zaidi ya saa 24, Misime amesema kuna mazingira yanaweza kuwafanya kuendelea kumshikilia kwa mujibu wa sheria.

Matarajio ya wengi ilikuwa ni kuona ama mtuhumiwa huyo anapelekwa mahakamani au anapewa dhamana baada ya saa 24 tangu alivyokamatwa na jeshi hilo kama inavyoelekezwa katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20.

Kifungu cha 32 cha sheria hiyo kinasema, “mtu yeyote akikamatwa na Jeshi la Polisi akiwa mikononi mwao isipokuwa kwa makosa ambayo adhabu yake ni kifo au makosa yaliyo na mazingira magumu, haraka iwezekanavyo anapaswa kufikishwa mahakamani kwa muda usiozidi saa 24, vinginevyo apewe dhamana kwa masharti yatakayokubaliwa.”

Akizungumzia hilo, Wakili Jebra Kambole amesema kisheria polisi wanapomtia nguvuni mtuhumiwa, wanapaswa kumpeleka mahakamani ndani ya muda usiozidi saa 24.

Hata hivyo, sharti la kumpeleka mtuhumiwa mahakamani ndani ya muda huo, alisema linatokana na aina na mazingira ya kesi husika.

Mathalan, kwa kesi zilizokuwa katika mazingira magumu zikiwamo zile ambazo adhabu zake ni kifungo cha maisha au kunyongwa, alieleza polisi wanaweza wasimpeleke mtuhumiwa mahakamani ndani ya muda huo.

Lakini, amesema hawapaswi kuendelea kubaki naye, badala yake anastahili kupewa dhamana huku mambo mengine kama kukamilisha ushahidi yakiendelea.

Msingi wa ufafanuzi wa wakili Kambole ni kifungu cha 32 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai sura ya 20.

Kifungu hicho kinaeleza: “Mtu yeyote akikamatwa na Jeshi la Polisi akiwa mikononi mwao isipokuwa kwa makosa yaliyo na mazingira magumu, haraka iwezekanavyo anapaswa kufikishwa mahakamani kwa muda usiozidi saa 24.”

Ameyafafanua makosa yaliyo katika mazingira magumu ni yale ambayo adhabu zake ni ama kifungu cha maisha jela au kunyongwa na aghalabu ni kosa linalohusisha mauaji ya zaidi ya mtu mmoja.

Hata hivyo, amesema katika mazingira ya makosa ya namna hiyo bado polisi hawapaswi kubaki na mtuhumiwa mahabusu, anastahili kupewa dhamana.

“Sio sawa kumshikilia kwa zaidi ya muda huo ni vizuri wakampa dhamana au wakampeleka mahakamani, hata kama upelelezi haujakamilika,” amesema wakili Kambole.

Amesema sababu za masharti hayo ni uhalisia wa mazingira ya vituo vya polisi kutokuwa na miundombinu wezeshi ya kumwezesha binadamu kukaa kwa zaidi ya saa 24.

Anawezaje kukosa dhamana?

Hata kama kosa linadhaminika kwa mujibu wa sheria, yapo mazingira yanayosababisha mtuhumiwa aendelee kushikiliwa na kunyimwa dhamana, kama inavyofafanuliwa na Dk Iddi Mandi mhadhiri wa masuala ya sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Dk Mand amesema polisi wanaruhusiwa kuendelea kumshikilia mtuhumiwa kwa zaidi ya saa 24 na bila kumpa dhamana iwapo itabainika kupewa kwake dhamana kunaweza kuathiri upelelezi.

“Ikibainika mtuhumiwa iwapo atapewa dhamana ana uwezo au nguvu ya kwenda kuharibu ushahidi, katika mazingira hayo huwa anaendelea kushikiliwa hata kama kosa lake linadhaminika,” amesema.

Mazingira mengine yanayosababisha mtuhumiwa kuendelea kushikiliwa, ameeleza ni iwapo itabainika kuachiwa kwake kunaweza kuathiri usalama wake.

“Hii ni katika mazingira ambayo, pengine mtuhumiwa akiachiwa anaweza kupigwa na wananchi wenye hasira kali au kudhuliwa kwa namna yoyote, katika kumlinda inabidi abaki ndani,” amefafanua.

Dk Mandi amesema mazingira mengine yanayoweza kumwacha mtuhumiwa ndani ni kama kosa lake halidhaminiki, ikiwamo mauaji ya kukusudia, uhaini na utakatishaji fedha.

Related Posts