Sakata la sukari lamuibua Kingu, ataka wananchi walindwe

Dodoma. Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Elibariki Kingu amewakemea vikali baadhi ya watu wenye maslahi yao binafsi kutaka kukwamisha mpango wa Serikali wa kutaka kuwalinda watumiaji wa mwisho wa bidhaa ya sukari.

Kingu ameyasema hayo bungeni leo Alhamisi Juni 20, 2024 alipokuwa akichangia mjadala wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/2025 ya Sh49 trilioni.

Amesema kwa viwango vya kulinda uchumi, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba na Rais Samia Suluhu Hassan wamefanya vizuri.

Amesema ukiangalia suala zima mfumuko wa bei tangu dunia imetoka katika misukosuko ya Uviko-19 kwa takwimu katika nchi za Rwanda, Kenya, Tanzania inafanya vizuri katika ukanda wa Afrika Mashariki na ukanda wa nchi za Kusini mwa Afrika.

“Viwango vya namna uchumi wa Tanzania unakwenda shikamoo mheshimiwa Waziri, unajitahidi kaka yangu kuliweka Taifa katika misingi ambayo imeipunguzia mshtuko wa uchumi Watanzania,” amesema.

Amesema kati ya wabunge watakauunga mkono Muswada ya Sheria ya Fedha kwa mwaka 2024 ni yeye kwa sababu inawapunguzia watu wachache kuhodhi suala la sukari nchini.

Amesema hana maana kwamba viwanda vya sukari vinafanya vibaya lakini wanafanya vitu ambavyo vinaleta shida katika soko na kwa mlaji wa mwisho ambaye ni mwananchi.

Kingu ametoa mfano wa mwaka jana ambapo Wizara ya Kilimo ilifanya tathimini ya sukari nchini na kupata upungufu wa sukari tani 60,000 na wakawaita wenye viwanda na kuwapa jukumu la kuagiza sukari hiyo.

“Na kwambia mheshimiwa mwenyekiti, Waziri kama siyo makusudi ‘maviwanda’ yote yaligoma kuleta sukari nchini. Hivi kweli tuingie gharama ya kuwapa mzigo mlaji wa mwisho.

Sukari ilifika hadi Sh7,000. Ingekuwa mnaweza kubadilisha kanuni Muswada wa Sheria Fedha, wabunge wote tutaipitisha kwa msimamo mmoja,” amesema.

Amesema hawawezi kuruhusu watu saba kuhodhi biashara ya sukari nchini kwa kupewa vibali vya kuagiza sukari lakini wanakwenda kuuza.

Amesema hiyo ni kuwapa mzigo Watanzania ambao ni walipa kodi wa Taifa na yeye kama mbunge anayetokana na CCM, amekwenda bungeni kwa kazi ya kuwapigania walipa kodi.

Kingu amesema Muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2024, ukipelekwa bungeni wataupigia debe kwa sababu suala la sukari linagusa maslahi makubwa ya walipa kodi wa Tanzania.

“Serikali yoyote duniani itakapokosa nguvu ya kuingia soko inapoona raia wake wanafanyiwa makusudi na kuadhibiwa, Serikali hiyo inakosa uhalali wa kuongoza nchi,” amesema.

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan hawezi kuona kuna wafanyabiashara wachache wanajipanga na yeye kukaa kimya kwa madai ya kuwalinda wenye viwanda ndani.

Amesema hata angekuwa yeye asingekubali, na kuwa Serikali iliyochaguliwa na wananchi na ikaaminiwa jambo la kwanza ni kulinda ustawi wa watu wake.

“Haya mambo kwa wabunge waliosoma kwa kodi za wananchi, tunaojua thamani ya Taifa letu, hatutaruhusu hili. Tunaweza kuchekea na kuoneana aibu kwenye mambo mengine lakini yanapokuja mambo yanayohusiana na Taifa letu tutailinda Serikali yetu kwa wivu na maslahi makubwa,” amesema.  

Aidha, Kingu amewataka Serikali kwenda kwenye uchumi wa kidijitali ambao utasaidia katika kuongeza walipa kodi nchini.

Related Posts