Samatta afunguka kinachomstaafisha Stars | Mwanaspoti

SIKU chache baada ya Mwanaspoti kuripoti nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kuomba kustaafu mwenyewe ameibuka na kutaja sababu zilizomfanya afanye hivyo kuwa ni umri.

Akizungumza na Mwanaspoti, Samatta amesema ni kweli ameliandikia barua Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) kuomba kupumzika kuitumikia timu hiyo kutokana na kuona umri wake umeenda.

“Ni kweli nimefanya hivyo umri unaenda na natumika sana naitumikia timu, nawapenda mashabiki zangu naomba waendelee kunisapoti hadi nilipofikia sasa bila wao nisingeweza naomba pia wawape sapoti vijana ambao wameibuka na wamekuwa wakilipambania taifa,” alisema na kuongeza;

“Kuna kuchoka na umri pia unaenda ni lazima nipate wakati wa kupumzika, mashabiki wamenilea wengi wao wameniona tangu nikiwa kijana mdogo kwakiasi kikubwa mafanikio niliyoyapata wao wamechangia.” Alisema.

Samatta alisema walichokifanya upande wake tangu anaanza kuitumikia Taifa Stars wanatakiwa kukiendeleza kwa wachezaji waliopo sasa huku akiwaomba wachezaji hao kufanya kazi kubwa kwa lwengo la kuendeleza ubora na historia nzuri kwenye kikosi cha timu hiyo.

“Tuwape ushirikiano tusiwakatishe tamaa ni wapambanaji nina imani kubwa na wachezaji waliopo naamini wataendelea kulisongesha gurudumu na hatimaye kufikia malengo.” Alisema Samatta.

Wakati Samatta akikiri hilo, TFF wamegoma kupokea uamuzi wa mshambuliaji huyo wakiweka wazi kuwa watatoa kauli yao mara baada ya kukaa kikao na staa huyo kwaajili ya kujadili suala hilo. Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, alifafanua juu ya jambo hilo hivi karibuni akisema;  “Hatuwezi kumuacha mchezaji mwenye CV kubwa kama yake, anajiuzulu kirahisi, sisi kama viongozi wa TFF, hatupo tayari kwa hilo tutakaa chini kuzungumza naye.”

Related Posts