Dodoma. Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby amesema wapo wapigaji wengi ambao wanasikika wakimsifia Rais Samia Suluhu Hassan anaupiga mwingi kumbe wanaiba fedha nyingi.
Shabiby ameyasema hayo leo Alhamisi Juni 20, 2024 wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Serikali ya mwaka 2024/25 ya Sh49 trilioni.
Amesema atanyoosha maelezo katika mchango wake kwa kuwa hatoki Singida (anakotoka Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba) na kwamba atazungumza ukweli utakaowasaidia mawaziri wawili ambao ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo na Dk Mwigulu.
“Siyo kama tupo CCM tu tunasifiana sifia humu tu hata kama vitu haviendi vizuri. Kama vitu vinaenda vizuri tusifiane ndio ubinadamu, kama vitu vinakwenda tunaambiana ukweli,” amesema.
Amemtaka Dk Mwigulu kupenda sana watu wanaomwambia ukweli kama yeye na kwamba yeye alitaka kujikita zaidi katika barabara.
Shabiby amesema yeye ni mjumbe wa Kamati ya Bunge Kudumu ya Miundombinu na kwamba barabara zilizochoka ziko 71 nchini ambazo muda wake umekwisha na ziko hoi.
“Ukichukua mfano wa Shinyanga, Mwanza, Lindi, Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma ziko nyingi tu ukiangalia barabara ambazo mmepangia Wizara ya Ujenzi ni Sh1.7 trilioni lakini madeni ni Sh1.2 trilioni kwa hiyo inamaana wao watabakia na Sh500 bilioni hiyo itafanya nini,” amehoji.
Shabiby amesema watawalaumu Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) bure wakati wanafanya kazi nzuri lakini yeye atakuwa mtu wa kwanza kupinga bajeti kama bajeti ya ujenzi wa barabara haitaongezwa.
Amemtaka Dk Mwigulu kuchukua maoni ya kamati yao ya kuongeza vyanzo vya uhakika vya mapato ya ujenzi wa barabara.
“Huo ndio ukweli, mimi sitaki kuzungumzia sukari kwa kuwa utazungumzia, utawazungumzia nani na nani kwa sababu ukiwachukulia nani nani hapa tukiongelea itakuwa balaa bora tunyamaze tu lakini kwenye hizi barabara zetu, tafuta vyanzo vya uhakika chukua ushauri wetu,” amesema.
Amemtaka kuchukua ushauri wao angalau kuongeza bajeti ya Sh2.2 trilioni kwenye Tanroads na Sh400 bilioni kwenye Tarura.
Amesema hata wabunge wakirejea majimboni kwao waonekane kuwa wamefanya kazi.
Aidha, amesema mwaka jana Serikali ilisema inatumia zaidi ya Sh500 bilioni kuagiza magari yake na bado anajiuliza maswali Serikali ni tajiri sana ama kuna shida gani.
“Umekuja na kuleta mpango kuwa kwa kuondoa gharama hizo kila mtumishi atanunua gari lake, uchungu atausikia lakini mwaka huu sijalisikia. Sijajua kama imekuja mpya ama lile limeshindikana,” amesema.
Shabiby amesema ukiangalia serikalini, halmashauri, manispaa na majiji magari mabovu hayauzwi na yakiuzwa hujiuzia watumishi wenyewe na kuhoji nchi inautajiri gani wa kutopiga mnada magari hayo.
“Nani alishawahi kusikia hapa kuna gari la Serikali linauzwa katika mnada? Haijawahi kutokea kwa hiyo magari yote mnajiuzia wenyewe. Utakuta gari ambalo lingepigwa mnada kwa Sh70 milioni linauzwa kwa Sh5 milioni. Halafu tunazungumzia kuwabinya watu wadogo wakati huku fedha zinapotea,” amesema.
Shabiby amesema ukienda katika Halmashauri ya Gairo mkoani Morogoro kuna magari saba na kwamba magari hayo yanatakiwa kuuzwa kwa mnada.
Pia, amesema kila taasisi ya Serikali imegeuka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuleta gawio pamoja na kuwa Serikali inategemea TRA.
“Nilikuwa nafikiri ule mpango wa Serikali ya awamu ya tano haukuwa mbovu, chukua pesa zote halafu wao waandike bajeti…Mnachotakiwa nyinyi BoT (Benki Kuu ya Tanzania) kuwafungulia akaunti (single treasury account) ili pesa zote ziingie kwenye akaunti moja ya Serikali,” amesema.
Shabiby amesema utaratibu umekuwa kinyume kwa Serikali kuwaachia, kutunga, kukusanya halafu wanazitandika lakini zifika kwao wanashangilia wakati ni fedha ndogo.
“Halafu tunakuja hapa tunashangilia. Mimi siwezi kuwa mshangiliaji ndio ukweli huo. Juzi hapa, nilikuwa nakuona unapata tabu sana kutafuta fedha. Baadhi ya taasisi zako zinakupinga lakini ukiwa Waziri wa Fedha unatakiwa uwe ngangari kama umeshindwa kuwa ngangari inabidi uachie hata mimi nije hapo,” amesema.
Amemwambia Dk Mwigulu hawezi kuwa mzuri kwa kila taasisi na kwamba nchi imefikia sasa hivi lazima waseme ukweli wapigaji wamekuwa ni wengi.
“Wapigaji wamekuwa ni wengi, wengine utasikia tu mama anaupiga mwingi siyo kwamba anaupiga mwingi anamsifia kwenye moyo aaha, anaupiga mwingi yeye anaiba fedha.
Anatandika fedha huku halafu anakuja huku anasifia na hata wewe na Mamlaka yako ya TRA nyie mnapata tabu. Waziri wa Fedha lazima nyinyi mkusanye kodi, lazima mzilete katika mishahara huku mzipeleke kwenye maendeleo wakati kuna taasisi mkizichanganya zinakusanya nusu ya TRA,” amesema.