Tanzania yatoa maagizo kukabili mauaji ya albino

Dodoma. Wakati matukio ya ukatili dhidi ya watu wenye ualibino yakianza kuibuka nchini, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametaja mikakati na maagizo kwa vyombo vya usalama, viongozi wa Serikali, dini, waganga wa kienyeji, wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla, ili kukomesha vitendo hivyo.

Hatua hiyo imekuja kutokana na mauaji ya mtoto, Asimwe Novath (2) mwenye ualbino, aliyeporwa mikononi mwa mama yake Mei 30, mwaka huu na watu wasiojulikana nyumbani kwao Kijiji cha Mulamula, Wilaya ya Muleba, mkoani Kagera na siku 19 baadaye ulipatikana mwili wake.

Mwili wa Asimwe ulipatikana Juni 17, mwaka huu kwenye kalavati katika barabara ya Luhanga wilayani Muleba, huku baadhi ya viungo vikiwa vimenyofolewa. Tayari mwili huo umeshazikwa.

Kutokana na tukio hilo, juzi, Jeshi la Polisi nchini limetangaza kuwashikilia watu tisa, akiwemo baba mzazi wa Asimwe.

Tukio jingine lilitokea Mei 4, 2024 ambapo mtoto Julius Kazungu (10) mwenye ualbino, mkazi wa Katoro, Mkoa wa Geita, alivamiwa saa 2.00 usiku na mtu asiyejulikana aliyekuwa ameficha sura yake na kuanza kumkata na panga kichwani na mikononi.

Mtoto huyo amelazwa hospitali na anaendelea vizuri. Serikali ya Mkoa inagharamia matibabu yake.

Matukio hayo yamelaaniwa na watu mbalimbali, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan aliyeonyesha kusikitishwa jinsi mtoto huyo alivyoporwa, kisha kubainika kuwa ameuawa na baadhi ya viungo vyake kunyofolewa.

Katikati ya mijadala hiyo, leo Alhamisi, Juni 20, 2024, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni jijini Dodoma, Kassim Majaliwa ametumia muda huo kutoa taarifa dhidi ya matukio hayo.

“Ninasimama mbele ya Bunge lako tukufu nikiwa na huzuni kubwa kutokana na matukio ya kikatili yaliyotokea hivi karibuni,” amesema Majaliwa.

Ameeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kuhakikisha ulinzi na usalama wa makundi mbalimbali, likiwemo kundi la watoto na jamii ya watu yenye ulemavu, wakiwemo wenye ualbino.

Jana Jumatano, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alitoa taarifa za kukamatwa watu tisa wakituhumiwa kwa mauaji ya Asimwe, akiwemo baba mzazi, Novart Venant, Desideli Evarist (mganga wa jadi), mkazi wa Nyakahama, Dastan Kaiza, mkazi wa Bushagara, Faswiru Athuman mkazi wa Nyakahama na Gozibert Alkadi, mkazi wa Nyakahama Kamachumu.

Pia wamo Rwenyagira Burkadi, mkazi wa Nyakahama Kamachumu, Ramadhani Selestine, mkazi wa Kamachumu na Nurduni Hamada, mkazi wa Kamachumu.

“Elipidius Rwegoshora, Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bugandika ndiye anayedaiwa kumfuata na kumshawishi baba mzazi wa mtoto huyo, ili wafanye biashara ya viungo vya binadamu,” alisema Misime.

Katika maagizo yake, Majaliwa ameelekeze Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, kwa tukio la Kagera, baada ya upelelezi, wale watakaobainika wafikishwe mahakamani, ili sheria ichukue mkondo wake.

“Hii itasaidia kutoa fundisho kwa wengine wanaofikiria kufanya hivyo, wakijua kuwa mkono wa sheria hautawaacha salama,” amesema.

Maagizo mengine kwa Jeshi la Polisi ni kuendelea kufanya operesheni ya kuwakamata wote waliotajwa na watakaotajwa kuhusika kwenye matukio ya aina hiyo kwa lengo la kuua mtandao mzima wa wahalifu hao na operesheni hizo ziwe endelevu.

Majaliwa ametaka Polisi Jamii ishirikishwe kikamilifu, ili kupata taarifa zote muhimu katika maeneo husika na watoa taarifa walindwe ipasavyo na kutumia taarifa za makazi na idadi ya watu wenye ualbino, ili kuelekeza nguvu zaidi za ulinzi kwenye maeneo hayo.

“Kuendelea kufuatilia kutumia taarifa fiche zinazopatikana kutoka vyanzo mbalimbali. Hii itasaidia kubaini mipango inayopangwa na wahalifu, ikiwemo wanaotafuta wateja wa biashara hizo na kuwabaini na kuwachukulia hatua kabla ya kutenda tukio,”amesema.

Pia ameagiza jeshi hilo pia kufanya upelelezi kwa weledi, ili kesi zinazopelekwa mahakamani ziwe na ushahidi wa kutosha.

Majaliwa ameagiza kutumia polisi kata kuhakikisha maeneo wanayoishi watu wenye ualbino yanatembelewa mara kwa mara, ili kupata taarifa zao na kutambua mapema viashiria vyovyote vya kihalifu, pia kuwapa elimu namna ya kutambua mtu mwenye nia ovu na yule mwema.

Majaliwa amesema wazazi nao wana wajibu kwa watoto wao kwa kuwapa malezi bora yatakayowawezesha kuwa watu wema katika jamii.

Amesema malezi hayo yanahusu yale yote anayofanyiwa mtoto tangu akiwa tumboni mwa mama hadi anapofikia umri wa kujitegemea na kuwataka wazazi wote wawili (baba na mama), wanahusika kikamilifu katika malezi.

Aidha, Majaliwa amesisitiza majukumu ya viongozi wa dini kukemea maovu yanayotendeka kwenye jamii yetu, hususan vya kuuawa kwa watu wenye ualbino.

“Nitumie nafasi hii kuwaomba viongozi wetu wa dini tuungane pamoja kupambana na mauaji haya ya watu wasiokuwa na hatia hata kidogo,”amesema.

Amewataka watumie majukwaa yao ya ibada kuwahubiria waumini wao kuachana na vitendo hivyo vya ukatili ambavyo hata Mwenyezi Mungu anavikataza.

Kwa upande wa waganga wa jadi, amewataka washiriki kikamilifu katika kampeni za kupinga mauaji ya watu wenye ualbino.

“Wakati umefika kwenu nyote kushirikiana na Serikali katika kutokomeza imani potofu zinazochangia mauaji haya,” amesema.

Kiongozi huyo amewataka waganga hao kueleza wazi kwamba hakuna tiba wala mafanikio yanayopatikana kwa kutumia viungo vya watu wenye ualbino, badala yake, matendo haya yanavunja haki za binadamu na kumomonyoa utu wetu kama Taifa.

Ameliagiza pia Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala lifanye usajili wa waganga wa jadi na vituo vyao sambamba na aina ya huduma wanayoitoa kwa wateja wao, ili kudhibiti huduma holela isiyofuata misingi ya utu na haki za binadamu.

“Nitoe wito kwa Chama cha Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala Tanzania (CHAWATIATA) kiwakatae na kuwatenga waganga wanaotumia njia za imani potofu, ramli chonganishi, ikiwemo kutoa masharti ya kufanya mauaji ya watu wenye ualbino ili kufanikisha mahitaji ya wateja wao,” amesema.

Kuhusu viongozi wa kimila, amewataka viongozi hao kutoka kila kona ya Tanzania, washiriki kikamilifu kukemea na kupinga mauaji ya watu wenye ualbino.

“Ninawaomba viongozi wetu wa kimila wakiwemo Machifu washirikiane na Serikali kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama pindi wanapopata fununu za mipango au vitendo vya mauaji ya watu wenye ualbino katika maeneo wanayoishi,”amesema. 

Pia Majaliwa amewataka Watanzania waache tabia ya kufanya mizaha isiyo na staha, hususan kuhusisha matumizi ya viungo vya watu, ama kuelezea kuwa viungo vya watu wenye ualbino vinaweza kuwaletea utajiri.

“Mizaha kama hii si tu inaonyesha ukosefu wa heshima kwa watu wenye ualbino na familia zao, lakini pia inachochea ubaguzi na unyanyapaa,” amesema.

Mikakati minane ya kuwalinda

Majaliwa amesema Serikali inaandaa Mpango wa Kuzuia Ukatili dhidi ya Watu wenye Ualbino (NAP) kwa kushirikiana na Chama cha Watu Wenye Ualbino (TAS) na wadau.

Pia amesema Serikali inaandaa kikao cha wakuu wa mikoa wote Tanzania Bara kitakachofanyika Julai 3, 2024 kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya ulinzi wa watu wenye ualbino.

Mkakati mwingine ni kutoa elimu ya kupinga ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu kupitia maofisa ustawi wa jamii, maofisa maendeleo ya jamii na maofisa elimu maalumu wa mikoa yote nchini.

“Kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu wenye Ulemavu ya mwaka 2004 na kuandaliwa kwa mkakati wake wa utekelezaji wa miaka mmitano (2024/2025- 2029/2030) na mkakati wa ufuatiliaji na tathmini wa miaka mitano itakayozinduliwa mwaka ujao wa fedha 2024/2025,” amesema.

Ametaja mkakati mwingine ni kukamilisha na kuzindua mkakati wa miaka mitatu 2024-2027 wa upatikanaji wa teknolojia saidizi kwa watu wenye ulemavu, wakiwemo watu wenye ualbino ambao umepangwa kuzinduliwa Julai, 2024;

Pia kuandaa na kukamilisha Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Watu wenye Ulemavu 2024/2025 – 2026/2027. 

“Kuendelea na ubainishaji na usajili wa watu wenye ulemavu ngazi za kijiji na mtaa kwa kutumia Mfumo wa Kielektroniki na Kanzidata ya Watu wenye Ulemavu niliouzindua Siku ya Kilele cha Maadhimisho ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani, Desemba 2, 2023 jijini Dodoma,”amesema.

Majaliwa amesema mkakati mwingine ni kuendelea kusimamia utekelezaji wa mwongozo wa ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu.

Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kuhakikisha kila halmashauri inaanzisha operesheni maalumu ya ulinzi kwa watu wenye ualbino.

“Oparesheni hizi zihusishe vikosi vya usalama, ili kuhakikisha ulinzi wa watu wenye ulbino dhidi ya mashambulizi na vitisho. Mamlaka za mikoa na wilaya zihamasishe uhakiki wa jamii kuhakikisha ulinzi na haki za watu wenye ualbino zinazingatiwa,”amesema.

Shangazi: Kila mtu ana haki

Akiuliza swali, Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi amesema Ibara ya 15(1) ya Katiba inasema kila mtu ana haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru.

Amesema katika maelezo ya Majaliwa kuwa kutaandaliwa kambi maalumu za kuwaweka vijana wenye ualbino, alihoji kuwa haoni kuwa hatua hiyo ni kuwanyima haki yao ya kuwa huru?

Akijibu, Majaliwa amewataka wabunge waendelee kuwapa muda Serikali kufanya tathimini ni njia ipi kufanya jamii yenye ulemavu kushiriki pamoja kikamilifu katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Related Posts