Vicky aipania Zambia baada ya kung’ara Moro

BAADA ya ushindi mnono  katika mashindano ya gofu ya Alliance One, nyota wa timu ya taifa ya gofu ya wanawake,  Vicky Elias ameanza mchakato wa kushinda mashindano ya wazi ya wanawake ya Zambia yanayoyatarajiwa kufanyika mjini Lusaka mwishoni mwa mwezi huu.

Vicky, ambaye alishinda kitengo cha wanawake wa daraja la juu kwa kupiga mikwaju 161 na kupata alama bora kabisa kwa wanawake, amedai jijini jana kuwa kung’ara katika mashindano ya wazi ya wanawake nchini Zambia ndiyo azma yake kuu na atatumia mchezo wa ubingwa wa mwezi utakaofanyika katika viwanja vya Dar es Salaam Gymkhana kesho kutwa kama sehemu ya mazoezi ya kujifua kwa ajili ya mashindano ya Zambia .

“Nilifanya mazoezi ya kutosha ili kuhakikisha nashinda mashindano ya gofu ya Alliance One na baada haya kutimia sasa najiandaa kwa mashindano ya Jumamosi katika viwanja vya Dar es Salaam Gymkhana kabla ya kuanza harakati za maandalizi kwa ajili ya mashindano ya  wazi ya Zambia,” alisema Vicky mara tu baada ya kurejea kutoka Morogoro.

Akielezea zaidi, Vicky alisema safari hii alivimudu vyema viwanja vya Morogoro ambavyo ni pekee kuwa na mashimo ya mchanga (brown) kuliko ilivyokuwa wakati wa mashindano yaliyopita ya Lina Nkya.

“Lilikuwa ni juma zuri kwangu baada ya kushinda mjini Morogoro na nategemea kufanya vizuri zaidi wakati wa michuano ya ubingwa wa mwezi katika viwanja vya Dar es Salaam Gymkhana Jumamosi hii,” alifafanua.

Kuhusu matarajio yake ya safari ya Zambia, Vicky anasema mambo yanaenda vizuri  kwani anachosubiri ni tiketi ya ndege kwenda na kurudi Lusaka.

“Hata hivyo bado nahitaji msaada wa ufadhiri ili safari yangu iwe na uhakika. Nitashukuru endapo nitapata msaada kutoka kwa wahisani na wadau wa gofu nchi nzima,”  alisema  Vicky ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya wanawake.

Related Posts