Waganga wa tiba asili walaani mauaji ya albino, washangaa kuhusishwa

Dodoma. Umoja wa Waganga na Wakunga wa Tiba Asili Tanzania (Uwawata) imesema hakuna tiba asili ambayo inahusisha viungo vya binadamu na kwamba wote wanaofanya vitendo hivyo ni matapeli wanatakiwa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi 20, 2024 na Katibu Mkuu wa Uwawata Taifa, Lucas Mlipu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu waganga wa kienyeji kuhusishwa na matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Mlipu amesema umoja huo umesikitishwa na matukio yaliyotokea hivi karibuni ya kujeruhiwa kwa mtoto mwenye ualbino Julius Kazungu (10) huko Geita na watu wasiojulikana na mauaji ya mtoto Asimwe Novath huko Kagera na kwamba waliofanya matukio hayo ni wahalifu na wala siyo waganga wa kienyeji.

“Baada ya taarifa kutoka kuwa mganga wa kienyeji anatuhumiwa kwa mauaji hayo, nilianza kupiga simu ili nijue ni nani kati ya wanachama wangu ambaye amefanya tukio hilo, lakini taarifa nilizopata ni kwamba mtu huyo siyo mganga wa tiba asili bali ni muuza dagaa ambaye siku za huko nyuma alikuwa ni msaidizi wa mganga wa tiba asili lakini naona alishindwa na kuamua kuuza dagaa, hivyo siyo mganga wa tiba asili,” amesema Mlipu.

Mlipu ambaye alikuwa ameongozana na viongozi wengine kutoka mikoa ya Tanga, Pwani, Arusha na Kagera lilipotokea tukio hilo, wamesema kuwa hakuna mganga wa kienyeji ambaye anatumia viungo vya binadamu kutibu watu kwani wao huwa wanatumia miti shamba na si vinginevyo.

Amesema umoja huo unawatambua watu wenye ulemavu wa ngozi kama binadamu wengine, hivyo wapo tayari kushirikiana na serikali kuwalinda kwa gharama yoyote kwani viungo vyao havihusiani na tiba asili.

“Na kama viungo hivyo vinahusiana na tiba, kungekuwa na matukio ya mauaji kwa kipindi cha mwaka mzima, lakini kwa nini matukio haya yajitokeze zaidi wakati wa uchaguzi wakati tunasikia viungo hivyo vinatumika kwenye uvuvi, madini na kwingineko ambako shughuli zake zinafanyika mwaka mzima?” amehoji Mlipu.

Katibu wa Uwawata Mkoa wa Kagera, Patian Kashubi amesema mkoa huo una matukio mengi ya mauaji kutokana na kupakana na nchi nyingi ambako huwa wanazuka waganga wa kienyeji ambao hawajulikani na kuwatapeli watu na kutoweka.

Amesema kwa sababu wao hawana mamlaka, wanashindwa kuwadhibiti kwani hata wakitaka kuwatambua huwa wanakabiliwa na vipingamizi na ndiyo hao baada ya kuwatapeli watu hutoweka na kuacha madhara kwa jamii.

“Kwanza kama kweli mtu anajiamini kuwa yeye ana sifa za kuwa kiongozi hawezi kwenda kwa mganga ili ashinde na ndiyo maana huwa hawaji kwa waganga waliosajiliwa kwa kuona aibu huenda kwa matapeli ambao huwapa masharti magumu ambayo kiuhalisia hayawasaidii kushinda uchaguzi,” amesema Kashubi.

Mwenyekiti wa Uwawata Mkoa wa Pwani,  Leonard Kalikera amesema waganga wote wa tiba asili nchini wamesajiliwa na wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi, hao ambao wanapiga ramli chonganishi ni matapeli ambao wanataka kuchafua sifa za waganga wa tiba asili kwa manufaa yao.

Amesema kwenye kila taaluma Kuna matapeli ambao huwa wanaichafua taaluma hiyo na ndiyo maana kuna madaktari feki, wanajeshi feki, makanjanja na vishoka hivyo hata kwenye kazi ya uganga kuna matapeli ambao wanajinufaisha kupitia taaluma hiyo.

“Sisi kazi yetu ni kutibu wagonjwa kama vile wanayofanya hospitalini, mgonjwa anakuja anaeleza anachoumwa nampatia dawa inayomtibu na hakuna tiba inayohusisha viungo vya binadamu,” amesema Kalikera.

Related Posts