Dar es Salaam. Hatima ya mabadiliko katika sekta ya habari, itaamuliwa na mageuzi kwenye maeneo sita, yaliyoazimiwa na wadau wa taaluma hiyo, baada ya kongamano la siku mbili.
Wadau wa habari walikutana kuanzia Juni 18 hadi 19, 2024, kujadili mustakabali wa sekta ya habari na hivyo kuazimia mambo sita yanayotajwa kama msingi wa mabadiliko katika sekta hiyo.
Mambo hayo ni kufanyika tathmini ya madeni ya vyombo vya habari kwa Serikali ili yalipwe, kuondolewa ukomo wa umiliki wa asilimia 49 ya hisa kwa wawekezaji wa kigeni katika vyombo vya habari, badala yake wamiliki kwa asilimia 75.
Mengine ni marekebisho katika vifungu 12 vya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, vyombo vya habari vya umma na binafsi vitoe fursa sawa kwa wagombea wote kuelekea uchaguzi.
Jambo lingine ni vyombo vya mtandaoni kuongeza ubunifu wa maudhui yenye tija.
Maadhimio hayo yameelezwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Thobias Makoba jana Juni 19, 2024 wakati wa kufunga kongamano la pili la Maendeleo ya sekta ya habari.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ametoa ufafanuzi kuhusu vifungu 12 vya sheria vilivyobaki ambapo zilipelekwa hoja zaidi ya 20.
“Tuliweka hoja za wadau na Serikali tukazizungumza na kukubaliana tukasema hoja hizi tisa tunakubaliana tukazibadilishe zilizobaki tukaelezana kwa sasa haziwezekani,” amesema.
Akitolea mfano wa umiliki wa pamoja wa vyombo vya habari amesema hoja hiyo ipo kwenye sera ya mwaka 2003 wakati huo akiwa anaanza kazi Chama cha Mapinduzi (CCM) hivyo inawezekana mazingira ya kipindi hicho walihitaji kuwasidia wazawa.
“Sera ni kubwa kuliko sheria na kanuni na kwenye mjadala wetu tukasema hili lisubiri marekebisho ya sera kwa sababu tupo kwenye mchakato huo,” amesema.
Hivyo amesema leo wakisema hilo kwa Serikali kulifanya hakuna atakayefanya kwa sababu ya kukubaliana na kwenye ripoti ya uchumi wa vyombo vya habari imewekwa hadi asilimia zinazotakiwa kuwa.
“Ni azimio sawa lakini lilishaisha kwa sababu lilikuwa kwenye mchakato wa sera sasa leo Waziri nafanyaje naandikaje sheria au kanuni kinyume na sera lilishaisha jamani nayapo mengine tumekubaliana kupeleka kwenye kanuni,” amesema.
Katika kuwahakikishia anachofanya ni kwa ajili ya wote amesema anayofanya si kwa ajili yake bali na kizazi kijacho endapo atatunga sheria mbovu zitawaumia hata kizazi chake na yeye mwenyewe.
“Mniamini tutaitengeneza sekta nzuri nafurahia kwenye hii sekta kwa sababu nimeisomea tuaminiane tutafika salama,” amesema Nnauye.
Amesema hata kuhusu leseni watalipeleka kwenye kanuni na walikubaliana kulipeleka huko kwa uwezekano wa mbele ya safari likaboreshwa zaidi badala ya kupeleka kwenye sheria.
Aidha, Nnauye amesema kuwepo kwa utamaduni wa kuita viongozi ili kujenga mijadala itakayojenga nchi.
“Kwa siku mbili tulizokuwa hapa tumejenga misingi bora zaidi katika seka yetu na hii niseme huu ni mwelekeo ambao Rais Samia anautamani na jana amesema mwenyewe na sisi wasaidizi wake tunapaswa kwenda katika muelekeo hu katika kuijenga sekta hii muhimu katika maenedelo ya nchi yetu,” amesema Nnauye.
Amesema katika kuleta mageuzi ya kweli sekta ya habari ni muhimuya kiuchumi, kijamii na hata kisiasa kwa kuelimisha vizuri wananchi ili watambue wajibu wao katika kuleta ustawi wa Taifa.
“Nina hakika wanahabari hali ya uchumi wa nchi yetu utabadilika kwa kuwawasukuma na asiyetaka atakwenda tu lakini wanahabari tuamue, tukiamua tutajenga Taifa letu linavyoendesha siasa zake tuna uwezo,” amesema.