Kufikia mwishoni mwa mwaka 2023, kiasi cha watu milioni 117 duniani kote waliyakimbia makazi yao kutokana na mizozo, mateso au vitisho vingine dhidi ya maisha yao. Takwimu hizi ni kulingana na ripoti ya hivi karibuni kabisa iliyotolewa na Kamishna Mkuu wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR. Kwa mujibu wa ripoti hiyo kiwango cha watu wanaogeuka wakimbizi kinaongezeka duniani.
Kati ya wakimbizi milioni 117 duniani waliorodheshwa na UNHCR, milioni 68.3 walikuwa ni wakimbizi wa ndani, ikimaanisha kwamba walilazimika kuyakimbia makazi yao na jamii, lakini walisalia ndani ya mipaka ya nchi zao za asili. Takwimu hizo za UNHCR zinahusu tu watu waliokimbia makazi yao kutokana na ghasia na vita. Kituo kinachofuatilia wakimbizi wa ndani cha IDMC kinakadiria kuwa watu milioni 7.7 zaidi wamekuwa wakimbizi kutokana na majanga ya asili na mabadiliko ya tabia nchi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo asilimia 48 ya wakimbizi wa ndani ni kutoka nchi za Kiafrika na asilimia 21 wanatoka Mashariki ya Kati. Sudan ndio inaongoza kuwa na idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani. Maeneo mengine yenye kiwango kikubwa cha wakimbizi ni Syria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Yemen.
Ulimwenguni kote, wakimbizi tisa kati ya 10 wanatoka Afghanistan, Syria, Venezuela, Ukraine, maeneo ya Palestina, Sudan Kusini, Sudan, Myanmar, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Somalia. Baadhi ya nchi za Ulaya, pia zimeshuhudia idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani. Kulingana na UNHCR takribani asilimia 43.4 ya watu duniani kote wanaishi nje ya nchi zao za asili kama wakimbizi au chini ya programu nyingine za ulinzi wa kimataifa kama vile hifadhi za muda za kibinadamu.
Soma pia: Misri yawarejesha makwao maelfu ya wakimbizi wa Sudan
Nchi nyingi zinazowapokea wakimbizi mara nyingi zinapakana na nchi za mizozo. Iran, Uturuki, Colombia na Jordan ndio nchi zinazopokea kiwango kikubwa cha wakimbizi, wengi wakitokea Afghanistan, Syria, Venezuela na Palestina. Takwimu pia zinaonyesha kwamba nchi zinazoendelea huchukua idadi isiyo na uwiano ya wakimbizi.
Baadhi ya nchi maskini zaidi duniani pia zinakabiliwa na mzigo mkubwa wa wakimbizi. Mojawapo ya nchi hizo ni Chad ambayo imewapokea zaidi ya wakimbizi milioni moja, licha ya kuwa moja ya mataifa yenye maendeleo duni ulimwenguni.
Soma: Makambi ya wakimbizi Chad yakabiliwa na mzozo wa kiutu
Mbali na wakimbizi wa ndani na wale waliotambulika, lakini kuna watu wapatao milioni 7 ambao bado wanasubiri vibali vyao vya ukimbizi kutambuliwa au kukataliwa na nchi zinazowahifadhi ambako walituma maombi. Ripoti inaeleza kwamba maamuzi kuhusu hali ya hifadhi haiendani na maombi yanayotumwa.
Kufikia mwaka 2023 wakimbizi wapatao milioni 1.1 wa zamani walirejea katika nchi zao za asili, ingawa wakati mwingine inakuwa sio salama. Wengi wao walirudi katika mataifa ambayo yalikuwa bado na vita na mizozo kama vile Sudan Kusini na Ukraine.