WAZIRI WA AFYA AZINDUA MSD MEDIPHAM MANUFACTURING CO.LTD

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amezindua Kampuni Tanzu ya Bohari ya Dawa inayoitwa MSD MEDIPHAM MANUFACTURING CO. Ltd., itakayosimamia viwanda vya kuzalisha bidhaa za afya, pamoja na kuzindua Bodi ya Usimamizi wa kampuni Tanzu hiyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Waziri Ummy Mwalimu amesisitiza kampuni tanzu hiyo kushirikisha wabia watakaokuwa tayari kushirikiana na MEDIPHAM kuzalisha bidhaa za afya, na kuendelea kutoa kipaumbele wazalishaji wa ndani.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MSD Rosemary Silaa ameeleza kampuni tanzu hiyo ni matokeo ya sheria ya MSD kufanyiwa makekebisho mwaka 2021, na kuongezewa jukumu la kuzalisha bidhaa za afya.

Hivyo amewaelekeza wajumbe hao wa bodi kuandaa mpango mkakati wa kampuni tanzu hiyo, pamoja na mfumo wa kutathimini namna ya kufikia malengo watakayojiwekea.

Silaa ameeleza kuwa ana imani kuwa kampuni Tanzu hiyo itafanikiwa, ikiwa na mikakati mizuri,akitolea mfano kuwa kiwanda cha barakoa kilianza mwaka 2021 na mtaji wa shilingi Bilioni 1.6 na hadi sasa wameshapata faida ya shilingi Bilioni 4.8.

Awali wa Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai ameeleza kuwa tayari kuna viwanda vitatu vinavyozalisha,ambavyo ni pamoja na viwanda viwili vya barakoa (surgical& N95)vilivyopo Keko na kiwanda cha mipira ya mikono kilichopo Idofi, Makambako.

Ameongeza viwanda vingine vilovyopo mbioni kuanzishwa,ni pamoja na kiwanda cha dawa Zegereni Kibaha na kiwanda cha bidhaa za pamba mkoani Simiyu.

Tukai, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya usimamizi wa Kampuni Tanzu (MSD MEDIPHAM) ameeleza kuwa jukumu lao kubwa ni kuhakikisha miradi yote iliyoanzishwa inaendelezwa na uendeshaji wake kuwa wenye tija.


Related Posts