Bajeti SMZ yapitishwa, Waziri akitaja sababu kutoongezeka vyanzo vya mapato

Unguja. Wakati Bajeti ya Serikali na mpango wa maendeleo Zanzibar kwa mwaka 2024/25 vikipitishwa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya ametaja sababu za kutoweka vyanzo vipya vya mapato, kuwa ni kutoa fursa kusimamia vyema vilivyopo.

Dk Saada amesema hayo akijibu hoja zilizochangiwa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika bajeti iliyowasilishwa barazani Juni 13, 2024. Baraza limeidhinisha bajeti ya Sh5.182 trilioni leo Juni 21, 2024.

Dk Saada amesema kutokuja na vyanzo vipya vya mapato haimaanishi wamefikia mwisho wa kufikiri bali ni kutaka kuimarisha vilivyopo.

“Hatukuja na kodi mpya kwa sababu tunataka kusimamia vyema kodi zilizopo na hili halimaanishi kwamba tumefikia mwisho wa kufikiri ila tunaangalia na mwenendo wa uchumi wetu,” amesema.

Waziri amesema wanataka kuimarisha na kuwekeza kwenye mifumo iliyopo, jambo litakaloongeza mapato na makusanyo ya Serikali kuliko kuja na kodi nyingi.

Amesema wapo katika hali nzuri ya kuweka mifumo inayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuwa wamejielekeza kwenye mkakati maalumu wa kuwekeza katika ujenzi wa viwanda.

Amesema kwa wawekezaji wanaowekeza katika viwanda watapewa unafuu, lengo likiwa ni kuhamasisha uwekezaji mkubwa katika eneo hilo, litakalosaidia kukuza uchumi na kutoa ajira nyingi kwa vijana.

Akizungumzia deni la Taifa, waziri amesema bado Serikali itaendelea kukopa kujenga miradi na miundombinu itakayosaidia kuimarisha uchumi wa kisiwa hicho.

Amesema wanakopa ili kuwekeza huku wakihakikisha ulinzi wa miundombinu.

“Tutaendelea kukopa kwa umakini kuwekeza katika miundombinu na miradi mbalimbali ili uzalishaji tunaoutaka uweze kupatikana,” amesema.

Dk Saada amesema kulingana na uchumi wa Zanzibar, hawawezi kuendelea kutegemea fedha zake za ndani, hivyo wanakopa kwa kuangalia masharti nafuu na ya muda mrefu.

Amesema bajeti hiyo imelenga kumkomboa mwananchi wa hali ya chini na ndio maana wameondoa na kuongeza tozo katika baadhi ya huduma.

Amesema iwapo wakitaka kumsaidia mwananchi lakini wakaendelea kuruhusu samaki na kuku wanaotoka nje ya nchi watakuwa hawajamsaidia mwananchi.

Akizungumzia kuhusu mfumuko wa bei Waziri huyo amesema Serikali imefanya jitihada mbalimbali kukabiliana na mfumuko wa bei, ikiwa ni pamoja na kuweka unafuu katika baadhi ya bidhaa.

Amesema ndiyo maana wanawekeza zaidi kulinda bidhaa za ndani ili kukabiliana na mfumuko huo, kwani endapo bidhaa nyingi hususani za vyakula zikiwa zinapatikana nchini, hata yanapotokea majanga nchi inakuwa salama kwa kuwa na akiba yake ya chakula.

“Hakuna nchi duniani ambayo imeendelea kama haijawekeza kwenye bidhaa za ndani,” amesema.

Amefafanua kuwa tozo ya Sh300 kwa kila kilo moja ya kuku na samaki inalenga kulinda bidhaa za ndani.

Kuhusu kilimo, Waziri Saada amesema bajeti hiyo inazingatia kuongeza kilimo na kwamba, kuna mpango maalumu wa mageuzi ya kilimo unaotarajiwa kuwasilishwa serikalini kuhusu namna bora ya kukuza kilimo kisiwani hapo.

Waziri Saada amesema kuna mpango maalumu wa makusanyo katika mapato ya serikali za mitaa na kwamba hawataruhusu biashara holela.

Badala yake amesema watahakikisha wafanyabiashara wote wanaendesha biashara katika masoko, ambayo Serikali imetumia gharama kubwa kuyajenga ili kuboresha mazingira ya biashara.

“Hatutaruhusu biashara holela barabarani ili tuhakikishe mapato yanakusanywa katika masoko hayo,” amesema.

Wakati huohuo, amesema kwa wawekezaji wanaopewa ardhi na kuzihodhi watanyang’anywa na kuwapa wengine wenye nia ya kufanya uwekezaji wenye tija.

Kuhusu misamaha ya kodi amesema ipo kwa mujibu wa sheria na kwamba imeongezeka kwa sababu ya miradi mingi ya uwekezaji.

Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi, Mwanaasha Khamis Juma ameitaka Serikali kuhakikisha inazingatia hoja zilizotolewa na wawakilishi na kuhakikisha bajeti hiyo inatekelezwa kama ilivyopangwa.

Related Posts