Baraza lapitisha sheria kuidhinisha makisio ya matumizi ya fedha 2024/25

Unguja. Baraza la Wawakilishi limepitisha sheria kuidhinisha makisio ya matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesema kupitishwa kwa muswada huo kutaiwezesha Serikali kukopa fedha ndani na nje ya nchi, kwa ajili ya matumizi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Muswada una vifungu vinane kikiwemo kinachozungumzia utoaji wa Sh5.182 trilioni kutoka mfuko mkuu wa Hazina ya Serikali.

Kifungu kingine kinazungumzia uwezo wa waziri kukopa, kifungu cha tano chenye vifungu vidogo vitatu kinazungumzia uwezo wa Waziri wa maombi ya ziada, kwa lengo la kukabili matumizi mengine ya dharura au pale haja itakapotokea.

Kifungu cha sita kinazungumzia marejesho ya mkopo na riba, huku kifungu cha saba kinazungumzia kukubaliwa kwa fedha zilizopitishwa kwa matumizi ya kazi za kawaida na miradi ya maendeleo, huku kifungu cha nane kinazungumzia, mfuko wa pamoja wa fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Katika hatua nyingine, Waziri Saada amewasilisha muswada wa sheria ya kutoza kodi na kufuta baadhi ya kodi na tozo na kurekebisha baadhi ya sheria za fedha na kodi zinazohusiana na ukusanyaji na udhibiti wa mapato ya Serikali na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Amesema barazani leo Juni 21, 2024 kuwa baadhi ya hatua za kuimarisha usimamizi na ukusanyaji wa mapato hazikuingizwa katika rasimu ya muswada wa sheria ya fedha ya mwaka 2024, kutokana na sheria husika kumpa mamlaka waziri husika kufanya marekebisho ya tozo kupitia hati za kisheria.

Hati hizo zitawasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar kwa ajili ya kutangazwa ili ziweze kuwa sheria.

Miongoni mwa hatua zilizotangazwa katika bajeti ya Serikali lakini zitatekelezwa kupitia hati za kisheria ni kutoa unafuu wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa vifaa vinavyotumiwa na watu wenye mahitaji maalumu.

Waziri Saada amesema kutoa unafuu wa kodi wa VAT kwa usambazaji wa boti zinazotengenezwa nchini, kutoa unafuu wa kodi ya VAT kwa uingizaji wa majokofu makubwa na gari zenye majokofu nchini.

Pia ni kutoa unafuu wa kodi ya VAT kwa uingizaji wa mitungi ya gesi ya kupikia, kutoa msamaha wa ushuru wa bidhaa kwa uingizaji wa gesi nchini (LPG).

Kutoza ushuru wa bidhaa kwa uingizaji wa kuku na samaki nchini, kuongeza kiwango cha kutoza ushuru wa bidhaa kwa uingizaji wa mvinyo na vinywaji vikali.

Kuongeza kiwango cha ushuru wa bidhaa kwa uingizaji wa shisha na sigara za kielektroniki, kutoza kiwango maalumu cha kodi ya miundombinu kwa wageni wanaolala katika ya visiwa au vyumba vya baharini.

Kutoza kodi ya miundombinu kwa kiwango cha Dola za Marekani, kutoza ada ya huduma za bandari kwa kiwango cha Dola, kuongeza kiwango cha ada ya huduma za bandari kwa abiria wanaosafiri nje ya Tanzania na kutoza ada ya udhibiti ya Sh50 kwa kilo kwa uingizaji wa gesi.

Wakichangia muswada huo, Mwakilishi wa Malindi, Mohamed Ahmada Salum alitaka kujua kilichosababisha fedha za wafadhili kupungua ikilinganishwa na kipindi kilichopita.

Waziri Saada amesema haijapungua ila washirika wa maendeleo wanapitia kufadhili miradi moja kwa moja tofauti na iliyokuwa awali.

“Hazijapungua ila kilichobadilika ni ‘modality’ kwa sasa wanakwenda kufadhili miradi moja kwa moja,” amesema.

Mwakilisi wa Ziwani, Suleiman Makame Ali amesema: “Tumeshaongea mengi tumeshachangia kwenye bajeti kwa hiyo kilichopo ni wewe nenda tu ukafanye kazi.”

Kuidhinishwa kwa bajeti za wizara na taasisi zote za Serikali kunasababisha muswada wa makisio na matumizi kutoa uwezo kwa Serikali kutumia kutoka mfuko mkuu wa Serikali Sh1.6 trilioni kwa ajili ya kazi za kawaida na Sh3.2 trilioni kwa miradi ya maendeleo.

Sh18.944 bilioni kwa ajili ya matumizi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sh202.607 bilioni kwa taasisi za Serikali zinazojitegemea kutoka mapato wanayokusanya na kutumia wenyewe.

Kifungu cha 41(4)(b) cha Sheria ya usimamizi wa fedha za umma namba 12 ya mwaka 2016 kimeelekeza bajeti ya Serikali kuwasilishwa na muswada wa sheria ya matumizi katika Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kuidhinishwa kabla ya kumalizika mwaka wa fedha unaoendelea Juni 30 ili kuruhusu kuanza kutumika mwanzo wa mwaka mpya unaofuata Julai Mosi.

Related Posts