Doyo, Itutu kuchuana kurithi mikoba ya Hamad ADC

Dar es Salaam. Doyo Hassan Doyo na Shabani Haji Itutu, ndio wagombea waliojitokeza kuwania uenyekiti wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) katika uchaguzi utakaofanyika Juni 29, 2024 kwenye Ukumbi wa Lamada, wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam.

Wagombea hao wa ADC, moja ya vyama vya upinzani nchini wanachuana kurithi mikoba ya Hamad Rashid anayemaliza muda wake kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

Katiba ya ADC inaelekeza nafasi ya kiongozi ni vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja, baada ya hapo hataruhusiwa kugombea tena.

Mmoja kati ya Itutu na Doyo ndiye atatawazwa kuwa mwenyekiti mpya wa ADC hadi mwaka 2029.

Doyo kwa sasa ni katibu wa ADC pia ni miongoni mwa waanzilishi wa chama hicho, wakati Itutu aliwahi kuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho.

Akizungumzia uchaguzi huo, katibu wa kamati ya uchaguzi, Innocent Siriwa ameiambia Mwananchi Digital kwamba, wagombea sita wamejitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi huo.

Wengine ni Scola Kahana na Hassan Mvungi wanaowania nafasi ya Makamu Mwenyekiti-Bara na Fatma Salehe na Shara Amrani wanaowania nafasi hiyo upande wa Zanzibar.

Amesema nafasi 19 za wajumbe wa Bodi ya Uongozi Taifa, wagombea watachukua na kurudisha fomu siku hiyohiyo ya uchaguzi Juni 29.

‘Watapigiwa kura siku hiyo ukumbini, kati ya wagombea wote wanaotakiwa kupigiwa kura robo au nusu ya idadi hiyo wanapaswa kuwa ni wagombea kutoka Zanzibar,” amesema.

Amesema kuanzia leo Juni 21, 2024 kampeni zimeanza ambazo zitafanyika kwa siku nane hadi Juni 28.

“Wagombea wote wafuate kanuni na taratibu kama ambavyo katiba ya chama chetu imeelekeza kwa kufanya kampeni za kukijenga chama,” amesema.

Siriwa amesema wametoa saa 24 kwa wagombea kuwekewa pingamizi kuanzia jana Juni 20 saa 2.05 usiku na itakapofika muda kama huo leo Juni 21, muda wa mapigamizi utafungwa.

“Mpaka muda huu (leo saa 5.00 asubuhi) hatujapokea pingamizi lolote kutoka kwa mwananchama au kwa mgombea kumwekea mgombea mwingine, saa 24 zikipita tunafunga zoezi hilo,” amesema.

Amesema, kamati imeelekeza kila mgombea kuandaa ilani yake ya uchaguzi ambayo itaeleza ni kitu gani anataka kukifanyia chama endapo atapata ridhaa ya kuwa mwenyekiti.

“Ilani hizi zinapaswa kuletwa kimaandishi kwenye kamati hadi kufikia Jumatatu (Juni 24, 2024)” amesema.

Siriwa amesisitiza wagombea kufanya kampeni za kistaarabu ambazo zitagusa maisha ya wananchi na kukisaidia chama.

Amesema kuna kanuni ambazo zina penati kwa mgombea atakayezikiuka, hivyo amesisitiza wote kusoma katiba na kujua kanuni hizo na yule ayakayekwenda kinyume chake atachukuliwa hatua.

Related Posts