SIKU chache baada ya Simba kutangaza kumtema aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, John Bocco ambaye kwa sasa ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya vijana ya klabu hiyo U17, makocha kadhaa akiwamo Idd Pazi ‘Father’ amedai kushangazwa na nyota huyo kutupa taulo mapema.
Pazi, nyota wa kimataifa wa Tanzania aliyewahi kuwika na Majimaji, Simba na Taifa Stars na kucheza soka la kulipwa nje ya nchi amesema Bocco alikuwa na nafasi ya kuendelea kuicheza kama asingesikiliza kelele za mashabiki na kuwapa ushauri wachezaji wengine kukaza kama wanavyofanya kila Erasto Nyoni, Kelvgin Yondani, Shomary Kapombe na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Kipa huyo wa kwanza kufunga bao katika Dabi ya Kariakoo mwaka 1984 katika sare ya 1-1 dhidi ya Yanga, alisema wapo baadhi ya wachezaji wazawa wanaoonekana umri umewatupa mkono, ila anaamini wakienda nchi jirani watang’ara kama wageni wenye umri mkubwa wanvyong’ara nchini.
Pazi alisema taarifa za Bocco kustaafishwa zimemshtua kwani anaamini angeenda kucheza soka katyika nchini za Kusini mwa Afrika ikiwamo Afrika Kusini, anaamini angeng’ara na angeendelea kuitwa timu ya taifa, Taifa Stars.
“Ukiachana na Bocco, kuna Kelvin Yondani, Erasto Nyoni,Shomari Kapombe, Salum Abubakar ‘Sure Boy na wengine wengi ambao bado wana uwezo mkubwa uwanjani ni wakati wao wa kwenda kushang’ara nchi za watu kwa vipaji walivyonavyo,” alisema kipa huyo wa zamani wa El Merrikh ya Sudan na kuongeza;
“Nimewashuhudia wachezaji wengi wa kigeni katika ligi yetu, wenye umri mkubwa na wanafanya vizuri, mfano Fabrice Ngoma, Yanick Bangala, Khalid Aucho, Meddie Kagere, Ley Matampi, hao nchini kwao walionekana wamemaliza, sasa kwa nini sisi wa kwetu, wanashindwa kujaribu.”
Akimzungumza hatma ya Aishi Manula kuendelea kuitwa Tanzania One, kuona ipo mikono mwa Simba na Azam FC, vinginevyo afanye maamuzi magumu ya kwenda nje.
“Kama Simba ikimuacha Manula na Azam haitamchukua, akienda timu ambazo zinashika nafasi kuanzia ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu, kuna ubora kwake utapungua, hapo Aishi atapaswa afanye maamuzi magumu ya kwenda nje,” alisema Father huku, mdau mkubwa wa soka nchini, Heri Chibakasa ‘Heri Mzozo’ alisema “Wachezaji baadhi wa kigeni ni watu wazima kuliko Bocco, Yondani, Kapombe, Haruna Moshi ‘Boban’, lakini wanapewa heshima.
“Watanzania tuna tabia za kuwachoka wachezaji wetu, mfano Saido naona ni mzee kuliko Boban, Aucho namuona mkubwa kuliko Bocco, ila kwa sababu tunapenda wageni wetu tunawaona wamechoka, ila na wao wanapaswa kwenda kujaribu maisha mengine nje,” alisema Mzozo kocha wa zamani wa Friends Rangers.