LAKINI ukweli ni kwamba kijiji kilikuwa salama kwa sababu kila ambaye hakufika hapo alikuwa anaendelea na maisha yake. Lakini wapo watu wachache ambao kwa sababu zao walijaribu kuruka uzio kwa lengo la kulifikia jumba kwa malengo mbalimbali, waliishia kwenye kinywa cha joka hilo lililokuwa na kasi na nguvu za ajabu sana.
Zamani wakati tukio hili la kubariki dawa zake lilipokuwa likifanyika, baadhi ya wanakijiji walikuwa wanakwenda kushuhudia tukio hilo na kuliona joka likitoka kwenye mtungi na kumzunguka Mzee Zimataa. Yalikuwa ni makundi kwa makundi ya watu.
Lakini kuna kitu kilikuwa kinatokea, ambacho hakikuwa cha kawaida. Kwamba watu wote waliokuwa wakitoka kwenye tukio hilo na kuliona joka, walikuwa wanakumbwa na homa kali na wachache wao walikuwa wanafariki.
Baada ya watu kugundua kwamba homa kali zinazowapata watu na vifo vya ghafla, huwa vilikuwa vinaambatana na tukio hilo, wakapiga marufuku wanafamilia hao kwenda kushuhudia jambo hilo. Na ndiyo ikawa sasa Mzee ZImataa hufika kwenye jengo hilo na kufanya anachopaswa kufanya na kuondooka bila bughudha yoyote kutoka kwa wananchi.
Kwa hiyo familia zikawa makini kuhakikisha hakuna kijana wao ambaye anafika kwenye lile jengo. Ndio maana jengo hilo limejitenga mbali kidogo na watu.
“Kweli hii ni miujiza.” Mbunge alianza huku macho kayaelekeza kwenye tukio analoliona.
“Joka kubwa kiasi kile linaishi kwenye mtungi? Sijawahi kuwaza wala kufikiri kwamba duniani miujiza mizito kama hii bado ingalipo.”
Diwani akatanguliza kichwa kukukubali.
“Ndiyo Mheshimiwa Mbunge. Ni kama vile nilivyokueleza. Nimekuleta ili ushuhudie kwa macho yako
Akiwa hapo, Mbunge aliendelea kulitazama joka likimzunguka Mzee Zimataa.
“Kwa hiyo… Joka la Zindiko linalinda hili jengo kwa miaka yote 20 uliyonambia, si ndio?”
“Nilipochaguliwa kuongoza hapa miezi sita iliyopita, nimekuta orodha ya makumi kwa makumi ya watu waliomezwa kwa kusogea kwenye viunga vya jengo lile. Jitihada zote zilizofanywa kuliondoa zilishindikana.
“Na viongozi waliothubutu kula njama na kuleta waganga wa kuliondoa, walikufa wao na waganga wao waliposogea tu kwenye uzio tena hata bila kuingia ndani. Mazingira ya vifo vyao yanayohusishwa na nguvu za zindiko la joka lile.”
Diwani aliweka nukta kuhitimisha sentensi yake hiyo.
Joka likamaliza kazi ya kumzunguka Bw. Zimataa, kisha likarudi kinyumenyume kuingia mtungini hadi likamalizika.
Ni jambo lililoangaliwa kwa mshangao mkubwa na Mbunge ambaye licha ya kujua lile jambo, lakini alikuwa hajawahi kuona. Ile ilikuwa ni miujiza mikubwa.
Miujiza si kuona nyoka au joka. Hivyo ni viumbe ambavyo alipata kuviona kwa nyakati tofauti. Miujiza ilikuwa ni kuliona joka refu lisilo na mwisho tena likiishi mtungini. Kwamba umbali wowote litakalokuwa linatoka, bado sehemu inayobakia huwa inabakia kwenye mtungi. Ndio kusema kwamba mwili wake unavutika kwa urefu wowote ule.
Hizo ni taarifa ambazo zilikuwa zikisimuliwa, lakini mwenyewe alizithibitisha.
“Hili ni jambo ambalo lazima liwe la hatari. Hii ni miujiza. Hiki si kitu cha kawaida kabisa. Kulishinda joka la namna hii, kunataka nguvu maalum! Na mimi kuna mtu ambaye namtumia kwenye mambo yangu na shughuli zangu. Ana nguvu kubwa, amenivusha kwenye majanga mengi mazito na ya ajabu.
“Japo hili ni la ajabu, lakini ntamweleza. Na kwa pamoja tutashinda. Nia yako ni usalama wa wanakijiji wa hapa, na mimi nina lengo pia kuhusu jengo hili na ardhi iliyolizunguka.
“Nia zangu na misimamo yangu ndiyo iliyowafanya wanakijiji wote hapa kunipa kura za vishindo. Hili ni jambo kubwa na la heshima sana ambalo wananchi wa hapa wamenipa. Kwa maana hiyo, siwezi kuwaangusha hata kidogo, lazima nisimamie kile ambacho nimekizungumza.”
Mzee Zimataa alikuwa tayari ameshamaliza kazi yake, akageuka na kuanza kuondoka.
Na ndio muda huohuo ambapo Diwani na Mbunge walitoka kichakani walipojificha na kusimama njiani kumsubiri.
Zimataa alipochomoka tu kutoka kwenye geti, njia ya kwanza aliyoichagua kupita, akakutana ana kwa ana watu wawili wakiwa wamesimama hatua chache kutoka hapo, wakimtazama yeye.
Hakushangaa kwa sababu wote anawajua. Na ile sio safari ya kwanza kwa Diwani pale. Zaidi ya mara tatu amekuwa akimfuata palepale na kushuhudia kile kitendo kisha kumwambia maneno ya kishujaa! Maneno ambayo alikuwa akiyazungumza sana wakati wa kampeni za uchaguzi zilizomuweka madarakani. Na mbili,
Nje kidogo ya geti, akawaona Diwani na Mbunge wakiwa wanafika kumkabili, wakasimama nje ya geti kumsubiri atoke.
Mzee Zimataa alifika na kusimama kwa ndani ya uzio. Akawatazama.
Alikuwa na uhakika kwamba akiwa ndani ya uzio, yupo sehemu salama kwa sababu hiyo ni ardhi isiyoweza kukanyagwa na mtu mwingine yeyote Zaidi yake. Diwani analijua hilo na Mbunge analijua pia.
Akawa wa kwanza kuwasemesha.
“Mheshimiwa Mbunge na Diwani, mbona mnanishtua. Mnakuja huku? Mmesahau kwamba hili ni eneo hatarishi kwenu?”
“Najua. Na Mheshimiwa anajua pia,” Diwani aliongea na kumtazama Diwani ambaye alimuunga mkono.
“Ni kweli. Hata mimi najua hilo. Huu ni ufalme wako Bwana Zimataa.”
Mzee Zimataa akakataa kwa kichwa.
“Huyu anajua, lakini siamini kama kweli unajua kila kitu – au hadi unafika hapa, amekwambia nusunusu. Ilivyo ni kwamba, ukisimama hapo kushuhudia hiki kinachofanyika hapa, na kuliona joka la zindiko kwa macho yako – unaweza kupata madhara ya kiafya. Amekwambia na hilo?”
Mbunge akatabasamu, “ najua pia, alinambia – lakini wewe ndiye mtu ambaye ukiamua hatutapata hayo madhara…”
Aliona kama vile Mbunge anaweka kejeli kidogo kwenye maneno yake.
Hiyo ni kawaida ya wanasiasa au wasomi – kudharau mambo yenye nguvu za asili na kukumbatia mambo ya kigeni.
Ni mambo yaliyoanza zamani. Kwamba licha ya Waafrika kuwa na nguvu na uwezo mkubwa wa kufanya karibu kila kitu katika ulimwengu huu, lakini wageni waliovamia nchi hizi kutoka Uarabuni na Ulaya, walidharau nguvu hizo. Na kubwa zaidi waliwalisha sumu baadhi ya watu ambao waliwaamini wao na kukataa nguvu hizo.
Katika mazingira hayo, wanapokuwa wamekwenda kusoma kwenye hivyo vyuo kwenye nchi zao, hutumia nafasi hiyohiyo kuwajaza sumu nyingine. Wanaporudi wanakuwa wameiva.
Na hata ukiangalia, ujio wa dini ulikuja kutokana na misafara ya wageni hao, Waarabu na wazungu ambao walikuwa na mkakati wa miaka mingi wa kutawala ulimwengu.
Wao kwa wao walipigana vita mara nyingi sana kutaka kuwa watawala wa dunia. Na ndiyo sababu kubwa ya kufika kwenye kila nchi na kusambaza dini kwa lengo la kuwashika watu kiroho na kimwili. Hilo liliwezekana na kuzika mila na Imani za wenyewe ambazo zilikuwepo tangu zama na zama na ziliwasaidia pia.
“Asante kwa kuja Mheshimiwa. Naona huwa unafika huku wakati wa kampeni zaidi kuliko hizi siku za kawaida, sijakuona muda mrefu.”
“Nafika mara kwa mara. Labda wewe hunioni tu.”
“Basi karibu sana. Mbona naona kama ujio wenu sio wa kawaida. Kunifuata hadi huku? Basi semeni kilichowaleta, kwa sababu ninaamini kilichowaleta ni kitu kinachohusiana na hapa nilipo. Si ndio bwana diwani.”