Dar es Salaam. Wajasiriamali 30 wa mazao ya uvuvi wakiwemo wachakataji na wauzaji wanapewa mbinu za kuboresha mazao ya uvuvi ili kupata masoko ya uhakika, ikiwa pamoja na udhibiti wa hatari za biashara, usafi na usalama wa chakula.
Mbinu nyingine ni pamoja na haki miliki na usajili wa jina la biashara, uundaji na usimamizi wa ushirikiano, kutumia majukwaa ya kidigitali, ufungaji na namna ya kuweka nembo, taratibu za mauzo ya nje na fursa za biashara chini ya jumuiya nyingine.
Akifungua mafunzo hayo leo Ijumaa Juni 21, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Uvuvi Tanzania (Tafiri), Dk Ismael Kimirei amesema mafunzo hayo pia yanalenga kuwajengea uwezo wajasiriamali hao kuzipata fursa za masoko ya kimataifa.
“Mtajifunza viwango vya bidhaa na uthibitisho kwa masoko ya ndani na ya kimataifa ya bidhaa za chakula zitokanazo na viumbe wa kwenye maji, udhibiti wa hatari katika uzalishaji wa bidhaa hizo, chakula kitokanacho na viumbe hai wa kwenye maji kinavyokaushwa, kufungashwa na zana za ukuzaji wa biashara,” amesema.
Dk Kimirei amesema mafunzo hayo yamekuja wakati ambao wajasiriamali hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto zinazosababisha washindwe kupata bidhaa bora.
“Ukweli ni kwamba mmekuwa mkikabiliwa na changamoto zinazowakwamisha kupata tija ya kazi zenu kutokana na kuzalisha bidhaa zisizo na ubora, hali inawakwamisha kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi,” amesema Dk Kimerei.
Pia, wadau hao wa mazao ya bidhaa za vyakula vitokanavyo na viumbe vya kwenye maji kutoka mikoa mbalimbali nchini ukiwamo Mara wamejengewa uwezo kuhusu stadi za ujasiriamali.
Mafunzo hayo ya siku nne yanafanyika katika ofisi za Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), yakiratibiwa na taasisi za Aquatic Bio Solution Tanzania (ABiST) na WorldFish.
Naye, Mwenyekiti wa ABiST inayojihusisha na utafiti na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza sekta ya uvuvi, ufugaji wa viumbe maji, Profesa Yunus Mgaya amesema mafunzo hayo yanalenga zaidi kuboresha ubora kwa kila wanachokizalisha.
Pia, Profesa Mgaya amesema mafunzo hayo yamelenga kuhakikisha kunakuwa na usalama wa chakula ili watumiaji wasipate madhara, akisema wadau hao watapewa stadi za ujasiriamali sambamba na kuwaunganishwa na masoko na sekta za fedha.
Mmoja wa wajasiriamali kutoka mkoani Mwanza, Fatma Katula amesema mafunzo hayo yatawawezesha kupata ujuzi watakaousambaza kwa wenzao ili kuongeza thamani na tija katika uzalishaji mazao ya uvuvi.