Mbeya. Wakulima katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wameiomba Serikali na wadau wa kilimo kutoa elimu ya matumizi bora ya teknolojia za kisasa kwenye uzalishaji wa mazao ya kimkakati ili kukwepa athari za mabadiliko ya tabianchi.
Wakiwa katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo Uyole, wakulima hawa wamezungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa, Juni 21, 2024, wakati wa hitimisho la siku ya maonyesho ya kilimo biashara.
Maonyesho hayo yamehusisha pia elimu ya matumizi ya teknolojia za kisasa kama vile uandaaji wa mashamba, matumizi ya mbolea, na upandaji wa mbegu zinazoendana na mabadiliko ya tabianchi.
Wakulima wamesema ukosefu wa elimu na taarifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi umekuwa ukichangia uzalishaji wa mazao yasiyo na tija, hali inayowafanya kushindwa kunufaika wanapoingiza mazao sokoni.
Safia Madenge, mkulima wa zao la ufuta kutoka Mkoa wa Iringa, amesema fursa za kilimo ni nyingi lakini uzalishaji unakosa tija kutokana na ukosefu wa elimu bora ya kilimo kinachoendana na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na uhakika wa masoko na tafiti za kina.
“Serikali inapohamasisha kilimo ni vyema kumtazama mkulima wa chini kwa kumpatia elimu kuanzia ngazi za awali za uzalishaji kutokana na dunia kukumbwa na mabadiliko ya tabianchi ambayo yameleta athari kubwa katika uzalishaji,” amesema Madenge.
Ameongeza kuwa kupitia maonyesho hayo, wamesikia mikakati iliyowekwa na Shirika la Care Tanzania kusaidia wakulima kwa kuwekeza katika mfumo wa ugani wa shamba darasa, ambao utakuwa mkombozi mkubwa kwao na kuomba serikali kuunga mkono.
Samson Mushi, mkulima mwingine, amesema maonyesho ya shamba darasa yamewajengea uwezo wa kuandaa mashamba na matumizi ya teknolojia za kisasa katika uzalishaji.
“Asilimia kubwa Serikali inategemea nguvukazi ya kilimo kutoka kwa wakulima wadogo, hivyo ni vyema sasa ikawekeza nguvu katika elimu ya mara kwa mara kwani dunia inabadilika kutokana na kukua kwa teknolojia za kisasa katika uzalishaji,” amesema Mushi.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Care Tanzania, Prudence Masoko, alizungumza katika maonyesho ya kilimo biashara yaliyohusisha wakulima zaidi ya 500.
Amesema wameweka mikakati ya kuangalia usawa wa kijinsia, usalama wa chakula, afya ya lishe na majanga.
“Tuko kwenye minyororo mbalimbali katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na Tanga kwenye mazao ya kimkakati kwa kuboresha mbinu za tafiti na majaribio kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo,” amesema Masoko.
Masoko alisema mifumo ya shamba darasa na biashara itawajengea uwezo wa kulima kwa kuongeza thamani na lishe ili kupata masoko makubwa ya kimkakati ndani na nje ya nchi.
“Care imekuja na mbinu ya ugani wa shamba darasa kupitia mikoa na halmashauri ambako imepeleka miradi, hususan mikoa ya Lindi na Mtwara, na imeleta matokeo mazuri. Tanzania ni miongoni mwa nchi 100 zinazonufaika kupitia shirika hilo,” ameongeza.
Christina John, meneja mwandamizi wa rasilimali na uhusiano katika Shirika la Care Tanzania, amesema wanafanya kazi katika nchi 100 duniani kwa kufanya tafiti za ugani kwenye kilimo zitakazoleta matokeo chanya.
Amesema kuwa kwa Tanzania walikuwa wakitumia sana wakulima kujifunza uzalishaji, ndio maana wamekuja na mpango wa kilimo biashara kwa kuwajengea uwezo wakulima kufanya tathmini ya uzalishaji na masoko kabla ya kuzalisha.
“Mbinu ya kilimo biashara itakuwa mwarobaini wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi sambamba na masuala ya tafiti za masoko, lishe na jinsia kwani asilimia kubwa ya wazalishaji ni wanawake ambao hawanufaiki,” amesema.