Majaliwa aeleza alivyofanya kazi na Nzunda

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameongoza waombolezaji kuaga mwili wa aliyekuwa Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Tixon Nzunda aliyefariki dunia kwa ajali ya gari Juni 18, 2024.

Nzunda (56) na dereva wake, Alphonce Edson (54) walipata ajali ya gari iliyotokea saa 8.30 mchana eneo la Njiapanda ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) wakienda kumpokea Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliyekuwa akielekea mkoani Arusha kikazi.

Akizungumza leo Ijumaa Juni 21, 2024 wakati wa kuaga mwili wa Nzunda nyumbani kwake Goba jijini Dar es Salaam, Majaliwa amesema atakumbukwa kwa uchapakazi wake.

Amesema amefanya naye kazi katika Serikali ya awamu ya tano akiwa Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu, alijua namna ya kuratibu shughuli za Serikali.

“Hakuna aliyekuwa na shaka naye, ushirikiano aliokuwa anautoa hatuna budi kuendeleza na kuenzi yote aliyoyafanya,” amesema Majaliwa.

Amesema kifo cha Nzunda   kimeacha majonzi kwa kuwa hakuugua, alikuwa ni mtu anayetegemewa na kuaminiwa kutokana na uchapakazi wake.

Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema uwezo wa Nzunda ulikuwa wa aina yake kutokana na uchapakazi.

Amesema kifo chake ni pigo kwa Tawala za mikoa na kwa familia kutokana na uwezo wake wa kiuongozi.

“Kifo ni kidonda kisichopona hasa kwa familia, ni pigo kubwa kwetu vijana, wengi wamejifunza mengi hasa kwa waliobahatika kufanya naye kazi,” amesema Mchengerwa.

Awali, Naibu Katibu Mkuu Tamisemi, Sospeter Mtwale alisoma wasifu wa Nzunda akieleza alitumikia kwa uaminifu mkubwa katika halmashauri za Handeni, Mbarali na Kibondo, ambako aliacha alama.

Amesema nafasi nyingine aliyotumikia ni Naibu Katibu Mkuu Tamisemi aliyeshughulikia elimu, akieleza alisimamia ujenzi wa madarasa.

“Unapomzungumzia Nzunda ni takribani miaka 12 ya utumishi wake ndani ya Serikali na hasa Tamisemi, ameacha alama kubwa,” amesema Mtwale.

Kwa upande wa familia, mtoto wa marehemu, Victor Nzunda amesema baba yake alikuwa miongoni wa walimu, mpenda haki, mpenda maendeleo, muadilifu na aliyeilea familia kwa hekima na busara.

Amesema baba yao alikuwa akiwaunganisha watu wenye mahitaji, wakiwamo yatima na wazee, pia alikuwa akienda hospitali kuwafariji wagonjwa.

Nzunda ambaye mwili wake uliagwa jana Juni 20, 2024 mkoani Kilimanjaro na kusafirishwa hadi Dar es Salaam, utazikwa kesho Jumamosi Juni 22, 2024 mkoani Songwe.

Viongozi mbalimbali wa kisiasa na Serikali, wamehudhuria kuagwa mwili wa Nzunda, akiwemo Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,  Nurdin Babu.

Wengine ni mawaziri, makatibu wakuu, wabunge, viongozi wa dini, watumishi na wakuu wa taasisi mbalimbali za Serikali na zisizokuwa za Serikali.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, juzi Juni 19,  mwili wa Nzunda baada ya kuagwa nyumbani kwake Goba utapelekwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na  kusafirishwa kuelekea Songwe.

Related Posts