Moshi. Wakati Mahakama ikilitupa ombi la mfanyabiashara, Rowland Sawaya la kuongezewe muda wa kukata rufaa, mdai katika shauri hilo amewasilisha ombi la kukazia hukumu, akitaka mdaiwa huyo afungwe gerezani kama mfungwa raia.
Lengo ni kumweka gerezani hadi alipe Sh584.3 milioni zinazotokana na hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Moshi ya mwaka 2004, iliyomuamuru kulipa Sh50.2 milioni, lakini zimeendelea kuongezeka kutokana na riba.
Mgogoro ulianzia katika kesi ya madai namba 12 ya mwaka 1998 ambayo mdai, Cornell Tarimo (sasa marehemu), alishinda shauri lililotokana na ajali iliyosababishwa na basi la Sawaya, mali ya mfanyabiashara huyo.
Katika hukumu aliyoitoa Oktoba 15, 2004, Jaji Lawrence Mchome (sasa mstaafu), alimuamuru Sawaya kumlipa Tarimo Sh50.2 milioni kama fidia kutokana na ajali iliyosababishwa na dereva wa basi hilo.
Hukumu ya Mahakama ya miaka 20 iliyopita iliona Sawaya kama mmiliki wa basi lililosababisha ajali, anawajibika na uzembe wa dereva wake, Raziel Ngowi aliyesababisha ajali ambayo ni kiini cha mgogoro huo.
Tangu hukumu kutolewa, Sawaya amekuwa akipambana kortini kujinasua, lakini ama rufaa anayokata au maombi yake ya kuomba kuongezewa muda ili akate rufaa, yamekuwa yakitupwa kutokana na dosari za kisheria.
Ni baada ya kuona hukumu ya mwaka 2004 haijabatilishwa na chombo chochote, Charles Tarimo, msimamizi wa mirathi ya Cornell Tarimo, amefungua maombi Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, akiomba kukazia hukumu ya mwaka 2004.
Katika maombi hayo yaliyopangwa kusikilizwa Julai 22, 2024 mbele ya Jaji Adrian Kilimi, Charles anaiomba mahakama itoe amri ya kumkamata Sawaya na kumweka kizuizini ili aweze kulipa fedha hizo na riba.
“Mshindi wa tuzo (decree holder) anaomba kukamatwa na kuwekwa kizuizini Sawaya ili kumlazimisha kulipa Sh584.3 ambazo ni pamoja na deni kuu, riba (ya miaka 20) na gharama za kukaza hukumu,” anaeleza Charles katika maombi yake.
Kutokana na mdai kuwasilisha ombi la kukazia hukumu, Sawaya alifungua maombi namba 37 ya 2023 katika Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, kuomba kuongezewa muda kukata rufaa dhidi ya hukumu ya mwaka 2004.
Maombi hayo ameyafungua dhidi ya Charles, kama mjibu maombi wa kwanza, Raziel Ngowi (dereva wa basi) kama mjibu maombi wa pili na kampuni ya bima ya National Insurance Corporation of Tanzania Ltd kama mjibu maombi wa tatu.
Ombi hilo aliliwasilisha chini ya hati ya kusikilizwa kwa haraka akiambatanisha kiapo cha wakili wake, Dickson Ngowi akisema sababu ya uharaka ni kuwa mshindi wa tuzo anataka kukazia hukumu.
“Sababu ni kuwa mjibu maombi wa kwanza anatafuta kutekeleza amri iliyochafuliwa na ubatili mkubwa wa kisheria kwa vile (Charles) pia anataka kumtia mbaroni mwombaji (Sawaya) kama mfungwa wa kiraia,” ameeleza wakili wake.
Katika uamuzi alioutoa Juni 19, 2024, Jaji Kilimi amerejea mtiririko wa shauri hilo namna mfanyabiashara huyo alivyoshindwa kesi mwaka 2004 na akakata rufaa Mahakama ya Rufani ndani ya muda kupitia rufaa namba 53 ya 2007.
Rufaa hiyo ilitupwa na Mahakama ya Rufani Agosti 21, 2012 kutokana na dosari za kisheria kwa kuwa kumbukumbu za rufaa alizowasilisha kortini, zilikosa uthibitisho kuwa alimpatia nakala ya notisi mjibu maombi wa tatu.
Baada ya uamuzi huo, mfanyabiashara huyo aliwasilisha ombi Mahakama Kuu kupitia maombi namba 30 ya 2012 akiomba kibali cha mahakama cha kuongezewa muda wa kukata rufaa, maombi yaliyoruhusiwa na mahakama Novemba 7, 2014.
Kulingana na maelezo ya Jaji, baada ya kupata kibali aliwasilisha rufaa kwa mara ya pili kupitia rufaa namba 1 ya 2015 ambayo Septemba 28, 2017, mahakama ilibaini nyaraka zilikosa nakala ya kibali kilichomwongezea muda.
Kutokana na hilo, rufaa ikatupwa pia, lakini Sawaya akafungua maombi mengine namba 518 ya 2020 akiomba kibali cha kuongezewa muda ili awasilishe maombi ya marejeo nje ya muda kuanzia hukumu na tuzo iliyotokana na kesi ya 1998.
Hata hivyo, wakili wake, Melkior Sanga aliomba kuondoa maombi hayo na Mahakama ya Rufani ikakubali, ikayaondoa Julai 6, 2023.
Desemba 2023, Sawaya aliwasilisha maombi ya kuomba kuongezewa muda wa kukata rufaa akieleza mjibu maombi wa kwanza amewasilisha ombi la kukazia hukumu na anataka mteja wake afungwe gerezani.
Akisikiliza ombi hilo na kutoa uamuzi Juni 19, 2024 Jaji Kilimi amesema wakati mjibu maombi wa kwanza (Charles), akisema Cornell Kisinane Tarimo alifariki Novemba 14, 2014, alisema yeye ndio aliteuliwa kama msimamizi wa mirathi Mei 26, 2023.
Akipinga ombi hilo, Charles amesema muombaji ameshindwa kutoa maelezo alikuwa wapi kwa miaka yote 19 na kwamba hoja ya kuwepo kwa dosari au ubatili wa kisheria hauwezi kuletwa leo kwa sura ya kumbukumbu za mahakama.
Wakili Ngowi aliyemwakilisha Sawaya alieleza hukumu ya Mahakama Kuu katika kesi namba 12 ya 1998 iligubikwa na dosari za kisheria na ilikiuka haki ya mteja wake kusikilizwa kwani hakupewa nafasi hiyo.
Pia alidai mahakama iliyosikiliza shauri hilo ilikosa mamlaka kisheria kwa kuwa shauri lilipaswa kusikilizwa na kuamuliwa Korogwe, hivyo kimamlaka, ilipaswa isikilizwe na Mahakama Kuu Tanga.
Wakili, Ceaser Shayo aliyemtetea Tarimo akisaidiana na mawakili Lilian Mushi na Beatrice Chami, alisema hakuna haki ya kusikilizwa aliyonyimwa Sawaya kwani katika shauri hilo alikuwa na wakili.
Wakili huyo alidai muombaji mwenyewe, ndiye aliyetoa taarifa mahakamani wakati wa mchakato wa shauri hilo la 1998 kuwa anaumwa na kesi iliahirishwa na siku ilipoitwa tena, wakili wake alisema mawasilisho ya mwisho yamekamilika.
Kuhusu hoja ya uwepo wa uharamu wa kisheria katika kesi ya madai namba 12 ya 1998, Wakili Ceaser alidai hoja hiyo ilitupwa wakati kesi ikisikilizwa na Jaji Mchome.
Wakili huyo alidai pingamizi la awali lilitolewa na mleta maombi (Sawaya) lakini katika ukurasa wa 15, 16 na 17 wa mwenendo wa kesi hiyo, iko wazi kuwa Jaji Mchome alilitupa pingamizi hilo na kuamuru kesi iendelee.
Kuhusu hoja kuwa mahakama ilikosa mamlaka ya kusikiliza shauri hilo la mwaka 1998, Wakili Ceaser alidai Sawaya anatoa huduma ya usafiri wa mabasi mikoa mbalimbali, ilikuwa sahihi kesi kufunguliwa Moshi.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji alisema mwombaji katika maombi hayo, ameeleza moja ya sababu za kuomba kibali cha kuongezewa muda wa kukata rufaa ni kwa kuwa mdaiwa wa kwanza anataka kumtupa gerezani kama mfungwa raia.
Kwamba hiyo ndiyo sababu ya kuomba maombi yasikilizwe chini ya hati ya dharura, Jaji alisema ingawa kutoa kibali ni utashi wa mahakama, lakini hiyo inapaswa kufanyika kuepuka kutokutenda haki.
Jaji amesema kuongezewa muda kusiwe ni kwa ajili ya kumsaidia mtu ambaye huenda kwa makusudi anaomba kibali kama ujanja wa kupoteza muda na haki ya upande wa pili, jambo ambalo mahakama haiwezi kulifanya.
Akinukuu misimamo ya kisheria ya kesi nyingine, Jaji Kilimi amesema Sawaya alikuwa na wajibu wa kueleza siku alizochelewa kuanzia siku kesi ilipoondolewa mahakamani na sio siku aliyogundua kuna ombi la kumpeleka gerezani kama mfungwa raia.
Jaji Kilimi amesema kutokana na hayo, mahakama inaona hakuna sababu za msingi zilizowasilishwa mahakamani kuishawishi mahakama kutumia mamlaka yake ya kisheria, kumwongezea muda wa kukata rufaa kupinga hukumu ya mwaka 2004.