Nairobi. Mwanaume mmoja aliyetambulika kwa jina la Rex Kanyike amefariki dunia kwenye maandamano yanayofanywa na vijana wa Kenya kupinga mapendekezo ya nyongeza ya kodi, Jeshi la Polisi nchini humo limesema leo, huku waandamanaji wakiitisha maandamano ya kitaifa wiki ijayo.
Jeshi la polisi limesema linachunguza madai kwamba mwanaume huyo alipigwa risasi na polisi baada ya maandamano ya juzi Alhamisi katika mji mkuu Nairobi.
Maandamano hayo yalianzia jijini Nairobi Jumanne iliyopita kabla ya kuenea nchi nzima, huku jana waandamanaji wakisambaza mabango ya kutaka kuitishwe mgomo wa kitaifa Juni 25, 2024.
Maandamano hayo yamechochewa na hali ya watu wengi kutoridhishwa na sera za kiuchumi za Rais William Ruto huku Wakenya wengi wakihangaika kujikimu kimaisha.
Maandamano ya Alhamisi jijini Nairobi sehemu nyingi yalikuwa ya amani, lakini maofisa walifyatua mabomu ya machozi na maji ya kuwasha siku nzima katika jaribio la kuwatawanya waandamanaji karibu na majengo ya bunge.
Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) imesema leo kwamba “imerekodi kifo” cha mwanaume mwenye umri wa miaka 29, “kinachodaiwa kuwa ni matokeo ya kupigwa risasi na polisi”.
“Mamlaka leo asubuhi imeanzisha uchunguzi kuhusu mauaji hayo,” IPOA imesema katika taarifa yake na kuongeza kwamba uchunguzi wa maiti utafanywa.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi wa Nairobi ambayo imewafikia AFP, kijana mwenye umri wa miaka 29 alipelekwa hospitali jijini Nairobi, saa 7:00 mchana Alhamisi “amepoteza fahamu kutokana na jeraha la kwenye paja” kabla ya kufariki kutokana na majeraha hayo, hata hivyo ripoti hiyo haikutoa maelezo zaidi.
Mathias Kinyoda, msemaji wa Amnesty International Kenya, ameiambia AFP kwamba “mwandamanaji mmoja alipigwa risasi jana katikati ya jiji la Nairobi alipokuwa akijaribu kuwakimbia polisi”.
Amesema kuwa aliyempiga risasi “alikuwa amevaa nguo za kawaida lakini alikuwa ameandamana na polisi” na ametaka uchunguzi wa kifo hicho ufanyike haraka.
“Tuliona kilichotokea,” shahidi ameiambia AFP, akielezea jinsi alivyokuwa miongoni mwa watu waliokusanyika kwenye ghorofa ya pili ya jengo hilo.
“Tuliweza kuona polisi wakilifyatulia risasi kundi lililokusanyika hapo,” mtu huyo amesema.
“Alikuwa ofisa wa polisi aliyevalia kofia ya beziboli, kwa sababu alishuka kutoka kwenye gari la polisi na kukimbilia tena baada ya kufyatua risasi wakati umati ulipotawanyika.”
Alhamisi, mashirika kadhaa, ikiwa ni pamoja na Amnesty International Kenya, yalisema kuwa takriban watu 200 walijeruhiwa jijini Nairobi.
Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya kupitia ukurasa wake wa X lilieleza kuwa watu wanane wako katika hali mahututi.
Huku habari za kifo cha mwandamanaji zikienea mtandaoni, waandamanaji walisambaza mabango ya kutaka kuitishwe mgomo wa kitaifa Juni 25.
“Jumanne Juni 25: #DhibitiBunge na KuzimaKabisa Kenya. Maandamano ya kitaifa,” lilisomeka bango lililosambazwa sana mtandaoni na kuongeza kuwa: “Gen-Z inawapa Wakenya wote wanaofanya kazi kwa bidii siku ya mapumziko. Wazazi waacheni watoto wenu nyumbani kwa mshikamano.”
Wito huo wa mgomo ulifuatia maandamano ya Alhamisi wakati maelfu ya watu walikusanyika kutoka wa Mombasa hadi ngome ya Ruto ya Bonde la Ufa, Eldoret.
Kufuatia maandamano jijini Nairobi mwanzoni mwa wiki, serikali inayokabiliwa na uhaba wa fedha ilikubali kurudisha nyuma nyongeza kadhaa ya kodi zilizowekwa katika muswada mpya.
Lakini utawala wa Ruto bado unanuia kuongeza baadhi ya kodi, ukitetea kodi zinazopendekezwa kama zinahitajika ili kujaza hazina yake na kupunguza utegemezi wa kukopa kutoka nje.
Baada ya uamuzi wa kufuta tozo za ununuzi wa mkate, umiliki wa gari pamoja na huduma za kifedha na simu, hazina ilionya kuhusu upungufu wa Ksh200 bilioni (dola bilioni 1.5).
Kodi zilizopendekezwa zilitarajiwa kuongeza Ksh346.7 bilioni (dola bilioni 2.7), sawa na asilimia 1.9 ya Pato la Taifa hilo na kupunguza nakisi ya bajeti kutoka asilimia 5.7 hadi asilimia 3.3 ya pato hilo.
Serikali sasa imelenga ongezeko la bei ya mafuta na ushuru wa mauzo ya nje ili kujaza pengo lililoachwa na mabadiliko hayo, hatua ambayo wakosoaji wanasema itafanya maisha kuwa ghali zaidi katika nchi inayopambana na mfumuko wa bei.
Kenya ni mojawapo ya nchi zenye uchumi unaoendelea katika Afrika Mashariki, lakini theluthi moja ya watu wake milioni 51.5 wanaishi katika umasikini.