NEMC kutumia Sabasaba kutoa elimu ya mazingira

Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), limejipanga kutoa elimu kwa umma na kufanya usajili wa miradi ya uwekezaji kwa kuzingatia tathmini ya athari za mazingira kwenye Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF).

Hayo yamebainishwa Dar es Salaam leo Juni 21, 2024 na taasisi hiyo, huku zikiwa siku sita zimebakia kabla ya kuanza maonyesho hayo ambayo hadi jana maandalizi yalikuwa yamefikia asilimia 79 ya maandalizi yake.

Akizungumzia namna ilivyojipanga taasisi hiyo kutoa huduma bora, Meneja wa NEMC Kanda ya Temeke, Arnold Mapinduzi amesema maandalizi waliyofanya yanaendana na hadhi na ukubwa wa maonyesho hayo.

“Ni maonyesho makubwa yanayokutanisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, wanakuwa na wasaa wa kuonyesha biadhaa zao. Sasa zikiwa na ubora tafsiri yake wanatangaza soko la bidhaa zao, kwa hiyo NEMC tutakuwepo kamili kutoa elimu na ufafanuzi unaohitajika,” amesema.

Mapinduzi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa maandalizi ya maonyesho hayo, amewakaribisha wawekezaji na wazalishaji wote watakaohudhuria kukaribia kwenye banda lao kwa ajili ya ufafanuzi wa masuala ya kimazingira na utoaji elimu utakaofanywa na maofisa wake.

“Tutasaidia kutoa huduma zingine kama usajili wa miradi kwa wawekezaji wanaohitaji iwe kwa kufanya tathimini ya athari za mazingira na kwa wale waliokuwa wameanza uwekezaji bila kuzingatia sharti hilo,” amesema Mapinduzi. 

Mapinduzi amesema kwa kuzingatia sheria ya NEMC, kabla ya uwekezaji wowote kufanyika nchini ni lazima ianze kufanyika kwanza tathmini ya athari za kimazingira, ambayo baadhi wamekuwa wakipuuza kwa kujua au kutokujua.

“Ukizingatia sheria ya athari za mazingira unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kupata cheti cha ithibati cha utunzaji mazingira kinachosainiwa na waziri mwenye dhamana na mazingira,” amesema.

Meneja wa Mawasiliano kwa Umma wa NEMC, Irene John amesema ili nchi iwe na maendeleo endelevu ni lazima kanuni za utunzaji mazingira zizingatiwe.

“Tumekuwa tukitoa elimu kwa njia tofauti kwa kushirikisha jamii ambayo imekuwa ikituamini na kutupatia taarifa sahihi ambazo tumekuwa tukizifanyia kazi kwa baadhi ambao hawazingatii utuzaji mazingira,” amesema.

Kwa mujibu wa ratiba, maonyesho hayo yataanza Juni 28 hadi Julai 13, 2024 katika viwanja vya Maonyesho vya Mwalimu Julius Nyerere maarufu Sabasaba.

Related Posts