PROF.KUSILUKA AVUTIWA NA UBUNIFU, UHODARI WA WANAFUNZI WA UDOM KWENYE MATUMIZI YA TEHAMA

 

MAKAMU Mkuu wa Chuo UDOM Profesa Lughano Kusiluka, akizungumza wakati akifungua Wiki ya ubunifu na tafiti ya Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu yaliyofanyika Juni 21,2024 katika Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

KAIMU Rasi wa Ndaki Dkt. Daniel Ngondya akizungumza,akizungumza wakati akifungua Wiki ya ubunifu na tafiti ya Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu yaliyofanyika Juni 21,2024 katika Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

Vijana wa chuo Kikuu cha Dodoma UDOM wakionesha ujuzi wao wa kutumia Kompyuta kwenye Wiki ya ubunifu na tafiti ya Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu

Makamu mkuu wa Chuo UDOM Profesa Lughano Kusiluka akikagua mabanda ya wanafunzi waliokuja kuonesha ujuzi wao Wiki ya ubunifu na tafiti ya Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM chini ya Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na elimu angavu (CIVE), kimezindua wiki ya utafiti na ubunifu, yenye lengo la kuonyesha thamani ya elimu kwa jamii.

Akizungumza leo Juni 21,2024 kwenye uzinduzi huo makamu mkuu wa Chuo UDOM Profesa Lughano Kusiluka amesema amekuwa akivutiwa na uhodari wa wanafunzi wa chuo hicho kwa ubunifu na maarifa yao ambayo ndiyo sababu ya kufanya vizuri katika mashindanio ya TEHAMA ndani na nje ya nchi.

Amesema lengo la Chuo Kikuu cha Dodoma ni kuhakikisha kila mwanafunzi na mfanyakazi wa chuo hicho chini ya ndaki ya Sayansi za Kompyuta na elimu angavu anao uwezo wa kuonyesha ubunifu.

“Hatubuni kwasababu tunajifurahisha, akili mnemba hii sasahivi tunainunua na vitu vyote tunavyotumia tunavinunua kutoka kwa watu ambao walibuni, lengo letu sasa na sisi tufike mahali tuwe na ujasiri wa kwamba hatuwezi kununua vitu kwasababu tunaweza kubuni na kutengeneza,”

“Na sisi tufike mahali tuseme hatutangoja China ifanye, hatutangoja Marekani, Ujerumani, Korea, Singapor wafanye kitu ndio sisi tukakifanye, hakuna mahali ambapo nimewahi kusoma kuwa akili za wale walioko kule zinatofautiana na za kwetu.” amesema Kusiluka.

Amesema watanzania wanatakiwa kuwa na ujasiri pamoja na uhakika wa kutengeneza bidhaa ambayo nchi za nje watakuwa na uwezo wa kuinunua kwani ubunifu ni fursa moja wapo ya kujipatia kipato.

Aidha ameongeza kuwa viongozi wa nchi wamekuwa wakisisitiza kuwa vyuo vikuu vinatakiwa kuzalisha vijana ambao wakimaliza masomo wanakuwa na uwezo wa kujitegemea na kujitengenezea ajira.

Kwa upande wake Kaimu Rasi wa Ndaki Dkt. Daniel Ngondya amesema kupitia maonyesho hayo wanapata fursa ya kuonyesha jamii yale ambayo wanafunzi wa UDOM wanayojifunza na kuweza kuyatenda kwa vitendo.

Amesema pia maonyesho hayo ni fursa ambayo inawawezesha wanafunzi kukutana na wadau pamoja na wateja watarajiwa wa bidhaa za ubunifu pamoja na kubadilisha mtazamo uliokwepo kwa muda mrefu.

Wiki ya ubunifu na tafiti ya Ndaki ya Sayansi za Kompyuta na Elimu Angavu yenye kaulimbiu kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia ubunifu wa kidijtali yanaendelea katika viwanja vya Nyerere Square kuanzia leo Juni 21, 2024 na yanatarajiwa kufungwa Juni 2024.

Related Posts