Waziri wa mambo ya nje wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani amewaeleza waandishi wa habari wakati wa mkutano wa pamoja na waziri mwenzake wa Uhispania mjini Madrid kwamba juhudi za kutafuta usuluhishi zimeendeleabila ya kuingiliwa. Amesema wamekuwa na mikutano kadha na viongozi wa Hamas, kujaribu kuunganisha pande hizo mbili ili kufikiwa makubaliano yatakayochangia kusitishwa kwa mapigano na kuachiliwa kwa mateka.
“Juhudi zinaendelea lakini mpaka sasa hatujafikia utaratibu ambao tunadhani ndiyo sahihi zaidi na unakaribiana na kile tulichokiwasilisha. Mara tu hili litakapokamilika, tutawasiliana na upande wa Israel ili kujaribu kuziba pengo na kufikia makubaliano haraka iwezekanavyo.”
Kauli hizo za matumaini zinatolewa wakati Israel ikiendelea kuushambulia Ukanda wa Gaza siku ya Ijumaa huku makabiliano ya risasi katika mpaka wake na Lebanon yakizusha wasiwasi wa kuenea kwa vita. Ama kwa upande mwingine Armenia imekuwa taifa la hivi karibuni kulitambua taifa la Palestina, huku wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo ikisema “janga la hali ya kibinadamu Gaza na mzozo wa kijeshi unaoendelea ni miongoni mwa masuala ya msingi katika ajenda za kimataifa yanayohitaji kushughulikiwa”.
Armenia mara zote imekuwa ikisimamia suluhisho la mataifa mawili kama njia bora ya kumaliza mzozo kati ya Israel na Palestina. Israeli tayari imekasirishwa na tangazo la Armenia na kulingana na wizara ya nchi hiyo tayari imemwita balozi wa Armenia kupinga hatua hiyo. Nchi nyingine ambazo tayari zimelitambua taifa la Palestina ni Norway, Uhispania, Ireland na Slovenia.
Hayo yakiarifiwa shirika la afya duniani la WHO, limeonya kwamba joto kali katika Ukanda wa Gaza linaweza kuzidisha matatizo ya kiafya kwa Wapalestina waliofurushwa na mashambulizi ya Israel na mapigano makali kati ya vikosi vyake na wanamgambo wa Hamas. Tayari shirika la mpango wa chakula duniani WFP lilitahadharisha kwamba mgogoro wa afya unainyemelea Gaza kutokana na ukosefu wa maji salama, chakula na vifaa vya matibabu. Soma: Mashirika ya misaada yatahadharisha juu ya kuzuka baa la njaa kaskazini mwa Gaza
Wimbi la joto kali limewaua mamia ya watu duniani kote na linaweza kuongeza madhila ya kiafya kwa wakaazi wa ukanda huo.