Rais Samia kunogesha tamasha la Utamaduni

RAIS wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa Tamasha la Utamaduni litakalofanyika mkoani Ruvuma katika viwanja vya Maji Maji kuanzia Julai 20-27 mwaka huu.

Hayo yamewekwa wazi na Naibu waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, katika uzinduzi rasmi wa tamasha hilo uliofanyika juzi jijini Dar es Salaam.

Mwinjuma aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa tamasha hilo alisema hilo ni tamasha la kimataifa la utamaduni lililotokana na maagizo ya Rais Samia mwaka 2021 jijini Mwanza na kuanza kufanyika 2022 Dar es Salaam na msimu wa pili ulifanyika mwaka jana Mkoa wa Njombe, hivyo hii ni awamu ya tatu huku akiwataka wadau kujitokeza kwa wingi kushiriki na kulisapoti.

“Nchi yetu imebarikiwa kuwa na makabila zaidi ya 120, yanayounganishwa na lugha ya Kiswahili. Wingi huu ni wingi wa urithi, mila na utamaduni kwetu jambo tunalopaswa kujivunia na kuendeleza,” alisema Mwinjuma.

Tamasha hilo limeandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na kampuni ya Drum Beats sambamba na taasisi ya Maji Maji Serebuka na litajumuisha michezo na maonyesho mbalimbali.

Riadha, Mbio za Baisikeli, Kushindana kula na kunywa vinywaji na vyakula asili, burudani na kazi mbalimbali za sanaa ni miongoni mwa vitu vitakavyonogesha tamasha hilo.

Aidha kutakuwepo na mashindano ya soka, maonyesho ya kibiashara na magari ya zamani, sambamba na mashindano ya ngoma za asili na mambo mengine mengi.

Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Drum Beats, Selestine Mwesigwa aliwakaribisha wadau kushiriki katika tamasha hilo na kusapoti.

“Tunaenda kuileta dunia Tanzania kupitia tamasha hili, kwani tulipewa jukumu la uhamasishaji na kutafuta rasilimali kwa ajili ya tamasha hili na tunaamini tutafikia malengo,” alisema Mwesigwa na kuongeza;

“Tunashukuru tumepata asasi zilizotuunga lakini tunatoa rai kwa serikali na taasisi binafsi kuendelea kutuunga mkono ili tukamilishe hili kwa pamoja na kuitangaza Tanzania.”

Uzinduzi huo uliofanyika katika kijiji cha Makumbusho, ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo Mkurugenzi wa utamaduni Dkt. Mnata Resani, Mwenyekiti wa umoja wa Machifu Tanzania, Antonia Shangalali, Mkurugenzi wa Tamasha la Maji Maji Serebuka, Reinafrida Rwezaura.

Related Posts