Wananchi kupewa mabomu baridi kukabiliana na tembo Lindi, Ruvuma

Tunduru. Wizara ya Maliasili na Utalii imepeleka askari wanyamapori kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (Tawa) kuwafundisha wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka hifadhi na mapori, namna ya kukabiliana na wanyamapori, hasa tembo wanaokatisha kwenye makazi yao.

Mafunzo haya yanatolewa katika Wilaya za Tunduru na Namtumbo mkoani Ruvuma na Wilaya ya Liwale mkoani Lindi, yakiwa yanahusisha matumizi ya mabomu baridi kujilinda na wanyama hao.

Hatua hiyo pia inahusisha ujenzi wa vituo pamoja na kupeleka vitendea kazi katika maeneo yenye changamoto ya mwingiliano na wanyama wakali, ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Mratibu wa mradi wa kutatua changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii katika mikoa hiyo, Gideon Mseja, amebainisha hayo leo wakati akifungua mafunzo ya waandishi wa habari yaliyofanyika Tunduru mkoani Ruvuma.

Mseja amesema changamoto ya wanyama wakali na waharibifu imeathiri wilaya 44 na Serikali imeendelea kuchukua hatua za kukabiliana nayo, ikiwa ni pamoja na kufanya doria za mara kwa mara na kujenga vituo vya askari wanyamapori.

Pia, Serikali imekuwa ikitoa vifaa vya kuondoa tembo kwenye maeneo ya wananchi kwa kufuatilia mienendo ya wanyamapori, kutumia helikopta na mabomu baridi, kutoa elimu, na kuwawezesha wananchi kiuchumi.

“Serikali imekuwa ikifuatilia mienendo ya wanyama kuona mzunguko wao ambapo kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (Tawiri), tembo wamefungwa vifaa vinavyoweza kutoa taarifa mapema endapo wanyama wanakaribia maeneo ya wananchi, ili askari wafike kuwaondoa,” amesema Mseja.

Serikali imeanzisha mradi wa ushirikiano kati ya Tanzania na Ujerumani unaolenga kutatua migongano baina ya binadamu na wanyamapori, unaotekelezwa kwenye ukanda wa Ruvuma. Mradi huu unalenga kutoa elimu kupitia waandishi wa habari. Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), John Chikomo, amesema mradi huo utawawezesha waandishi wa habari kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya shoroba za wilaya hizo tatu kuhusu namna ya kuishi na wanyama hao na kujilinda.

“Ni kweli changamoto ya migongano baina ya binadamu na wanyamapori ni nyingi. Tumeona habari kwenye magazeti na televisheni kuhusu ongezeko la wanyama kuingia katika maeneo ya makazi ya watu na kusababisha madhara mbalimbali kwa kuharibu mashamba na kujeruhi au hata kusababisha vifo,” amesema Chikomo.

Related Posts