ACT-Wazalendo yatoa tahadhari mwenendo wa deni la Serikali

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kukopa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo, hali ya deni la Serikali na masuala ya mikopo yameendelea kuibua mijadala miongoni mwa jamii,  baadhi wakidai ndicho chanzo cha kodi zinazolalamikiwa.

Kufuatia mwenendo wa deni la Serikali ambalo sasa linatajwa kufikia zaidi ya Sh90 trilioni, Chama cha ACT-Wazalendo kimesema bajeti ya Serikali ya 2024/2025 ni ya kulipa madeni na gharama za utawala, huku ikiendelea kuacha maumivu kwa wanyonge.

Akizungumza na waandishi wa habari Juni 22, 2024,  Waziri Kivuli wa Fedha, Mipango na Hifadhi ya Jamii, wa chama hicho, Kizza Mayeye amesema licha ya fedha nyingi za bajeti kuelekezwa kulipa madeni,  bado Serikali imeendelea kukopa, huku athari za ukubwa wa deni la Serikali likiangukia kwenye mabega ya wananchi wanyonge.

Amesema hadi Aprili 2024 deni la Serikali limefikia Sh91.7 trilioni ikilinganishwa na Sh82.5 trilioni iliyokuwapo Aprili, 2023 ikiwa ni ongezeko la Sh10.94 trilioni sawa na asilimia 15.

 “Ongezeko hili halijawahi kutokea tangu nchi yetu ipate uhuru. Kimekopwa kiasi cha Sh27.18 trilioni ikijumuisha Sh17.7 trilioni (mtaji) na Sh9.48 trilioni za riba,” amesema.

Amesema mwenendo huo wa deni la Serikali unatishia maendeleo ya watu, uwezo wa nchi kujihudumia na kusababisha ukuaji wa uchumi unaoendeshwa na deni.

“Madhara makubwa ya ukopaji huu holela ni kuongeza gharama za kulipa deni kama tunavyoona kwenye bajeti ya mwaka huu. Gharama za madeni zimeongezeka kwa asilimia 25.3 wakati uwezo wetu wa makusanyo ya ndani umeongezeka kwa asilimia 13.4,” amesema.

Amesema matokeo ya suala hilo, wananchi wanaongezewa kodi, ushuru na makato katika huduma muhimu kama vile umeme, elimu, afya, maji na kodi kwenye mazao ya kilimo ili kulipa madeni.

Hata hivyo, katika mjadala wa deni la Serikali hivi karibuni, Kamishna wa Usimamizi wa Deni la Serikali wa Wizara ya Fedha, Japhet Justin, alisema ukubwa wa deni unakua kwa kuongozwa na shabaha za uchumi.

“Kuna kuwa na malengo yanayopelekwa bungeni, mfano mwaka ujao tunasema tunataka kukopa kiasi fulani, hivyo bajeti iliyosomwa hivi karibuni inaenda kutengeneza matumizi na mapato tarajiwa kwa mwaka husika wa fedha,” alifafanua.

Alisema ukopaji unasimamiwa na sheria ya mikopo na madeni na taratibu za kukopa zinafanyika kutokana na misingi ya sheria.

Asilimia 30 ya bajeti itategemea mikopo na misaada.

Mapendekezo ya bajeti ya Serikali yanaeleza kwa mwaka wa fedha ujao sehemu kubwa ya Sh49.3 zilizopangwa kutumika zitatokana na mapato ya ndani ya Serikali Kuu ambayo ni Sh33.25 trilioni za mapato ya kodi na yasiyo ya kikodi.

Eneo lingine ambalo Serikali inatarajia kukusanya mapato kwa kiwango kikubwa ni mikopo ya kibiashara ndani na nje ya nchi kwa kiasi cha Sh9.6 trilioni, huku misaada na mikopo nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo ikichangia Sh5.1 trilioni.

Kwa maana hiyo, ni kuwa pamoja na kutegemea mifuko ya walipa kodi kwa zaidi ya theluthi mbili (Sh33.25 trilioni), karibu theluthi moja itakayobakia Serikali itategemea kukopa na misaada ili kutekeleza bajeti yake ambayo kwa ujumla itakuwa (Sh14.7 trilioni).

Kuhusu utegemezi wa bajeti katika mikopo na misaada Meneja Mwandamizi wa Kampuni ya Ukaguzi wa Mahesabu ya Ernst & Young (EY), Fredy Rugangila amesema ni kwa sababu uchumi wa nchi bado ni mdogo.

Wakati wa uchambuzi wa bajeti uliofanywa hivi karibuni na EY, Rugangila alisema vyanzo vya nje haviepukiki kwa sababu vya ndani havitoshi na kutahadharisha kuwa zikitokea changamoto za kidunia chanzo hicho huathirika.

“Ni kweli bajeti yetu inategemea fedha nyingi za kukopa na msaada na ni kwa kuwa nchi yetu bado inaendelea, hatujafikia uwezo wa kujitosheleza kwa sasa kutegemea nje hakuepukiki, mapato ya ndani hayatoshi,” amesema Rugangila.

Wakati mijadala ya deni la Serikali ukiendelea,  Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF)  limeipatia Tanzania zaidi ya  Dola za Marekani milioni 935.6 (Sh2.46 trilioni), kati ya hizo, Dola milioni 149.4 (Sh394.4 bilioni) ni za kusaidia bajeti ya Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Juni 21 na Wizara ya Fedha, Dola milioni 786.2 (Sh2.07 trilioni), ni za kugharimia mpango wa miezi 23 wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha la ‘Resilient and Sustainable Fund’ (RSF).

Taarifa ya uamuzi huo uliofikiwa na Bodi ya Wakurugenzi wa IMF, imetolewa kupitia tovuti rasmi ya shirika hilo, Juni 20, 2024, baada ya kumaliza mapitio ya tatu ya utekelezaji wa programu ya Extended Credit Facility-(ECF).

ECF inahusika na upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii kwa Tanzania.

Julai 2022, shirika hilo liliidhinisha Dola za Marekani bilioni 1.1 (Sh2.8 trilioni) kwa Tanzania.

IMF limeiongezea Tanzania miezi sita ya utekelezaji wa mpango wa ECF hadi Mei 2026, ili kutoa muda wa kutosha katika kutekeleza na kutimiza malengo makuu ya mpango huo.

Mageuzi yatakayotokana na RSF, yanalenga kuimarisha uratibu wa sera za mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha usimamizi wa namna ya kukabiliana na hatari za majanga, kuingiza sera za hali ya hewa kwenye mipango ya bajeti na uwekezaji, kuoanisha sera za sekta za hali ya hewa na sera za nchi, na kuimarisha uangalizi wa hatari zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi katika sekta ya fedha.

Baada ya kupata mkopo huo, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, aliishukuru IMF kwa uamuzi wa kuridhia maombi ya Serikali kuhusu mpango huo baada ya majadiliano ya kina na yenye manufaa kwa Tanzania.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, Dk Mwigulu amesema hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa kuwekeza fedha hizo katika sekta za uzalishaji na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ameahidi fedha hizo zitasimamiwa ipasavyo ili kuhakikisha malengo ya upatikanaji wake kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Related Posts