Tukiwa bado na majonzi ya kumpoteza Balozi Ferdinand Kamuntu Ruhinda, mmoja kati ya wazalendo walioitumikia nchi hii kwa muda mrefu na kwa mapenzi makuu, hatuna budi kuendelea kuyaenzi yale mazuri aliyoyafanya.
Kuna mambo mengi aliyoyafanya, ambayo hayakujulikana kabla ya kifo chake na hivyo kumfanya awe maarufu baada ya kuondoka duniani kuliko kipindi cha uhai wake.
Balozi Ruhinda alipenda kusema: “Kazi unazozifanya zikutangaze na si picha za magazetini au televisheni.” Kwa kifupi, hakupenda kuonekana mbele ya vyombo vya habari popote pale alipokuwepo.
Wengi tunashangaa kusikia kwamba tangu alipostaafu utumishi wa umma mwaka 1992, kama kuna picha alipiga katika matukio, basi ni za kuhesabika, kwa hakika hazizidi hata 10.
Ni watu wachache wanaojua kwamba yeye ndiye alikuwa meneja wa kampeni za urais zilizomwingiza Rais Benjamin Mkapa madarakani, kisha akaifanya kazi hiyo kwa Jakaya Kikwete, lakini si jina lake wala sura yake iliyopamba kurasa za vyombo vya habari. Hii haikuwa kwa bahati mbaya.
Pamoja na kazi zake hizo nyingi, Watanzania wengi hawajui Balozi Ruhinda alitoka wapi na kwa nini baada ya kifo chake ndio ameanza kuitwa chifu, cheo ambacho hakukipenda katika maisha yake yote, japo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipendelea kumuita hivyo, kwa mujibu wa hotuba ya Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba.
Je, ni kwa nini hakupendelea kuitwa chifu pamoja na kwamba amezaliwa katika familia ya watawala? Hilo ni swali ambalo linajadiliawa katika kumbukizi hii ya maisha ya Balozi Ruhinda.
Ni kweli kwamba Balozi Ruhinda alizaliwa katika familia ya watawala na kwa hakika alikuwa mtoto wa Chifu Bernad Itogo Ruhinda, mtawala wa mwisho wa kijadi wa himaya ya zamani ya Karagwe. Alizaliwa mwaka mmoja kabla baba yake hajatawazwa kuwa chifu wa Karagwe mwaka 1939.
Ikumbukwe kwamba cheo cha uchifu si cheo chetu Waafrika. Ni cheo ambacho kilianzishwa na Wajerumani na baadaye kuendelezwa na wakoloni wa Kiingereza. Kwa himaya ya Karagwe hata nyingine za maziwa makuu, kiongozi mkuu aliitwa Omukama, tafsiri yake ni Mfalme au Sultani. Huyu alikuwa ni kiongozi mwenye mamlaka yote hata kutoa hukumu ya kifo. Kwa Kiingereza wanamuita Absolute King. Kwa maana nyingine alikuwa juu ya Bunge na Mahakama na Serikali (wengi tutashangaa kusikia kwamba himaya ya Karagwe kabla ya ujio wa wakoloni ilikuwa na serikali chini ya Omukama, pia ilikuwa na Bunge likiitwa Orukiko na Mahakama ambayo iliitwa Egomborora).
Wakoloni waliwaondoa au kuwabadilisha wafalme (Abakama) na kuwaweka au kuwaita machifu. Pia waliwaondolea mamlaka yote waliyokuwa nayo. Badala ya kutokuwa chini ya amri yoyote, wakawa chini ya mkuu wa wilaya.
Iliyokuwa himaya ya Karagwe, sasa Wilaya ya Karagwe ilianza kutawaliwa na ukoo wa Bahinda (ukoo wa baba zake na Balozi Ruhinda) kuanzia mwaka 1450. Omukama (mfalme wa kwanza akiwa ni Ruhinda I). Utawala huo uliendelea mpaka mwaka 1914 (kwa mujibu wa kitabu cha Karagwe, Historia, Mila na Desturi), ambapo Omukama wa wakati huo aliyeitwa Ntare Kanyorozi alinyongwa hadharani mbele ya posta ya zamani katika mji wa sasa wa Bukoba. Baada ya mauaji hayo, Karagwe ililetewa mtawala wa muda kutoka Uganda aliyejulikana kama Issack Mumanya, ambaye alipewa nafasi ya kumuandaa mtawala mpya ambaye angekuwa chini ya utawala wa wazungu kupitia mfumo wa indirect rule kama ulivyoasisiwa na kufanyiwa majaribio na Lord Fredrick Lugard nchini Cameroun na Nigeria.
Baada ya wakoloni kuyaondoa mamlaka ya wafalme na kuweka machifu, Karagwe ilitawaliwa na machifu wawili tu kuanzia mwaka 1925 mpaka 1963 baada ya Serikali ya uhuru kupiga marufuku utawala wa jadi nchini.
Machifu hao walikuwa ni Daudi Tigwalaremu (1925-1938) aliyepewa jina la utawala la Omukama Rumanyika II na wa mwisho alikuwa Bernard Itogo Ruhinda, huyu alipewa jina la Omukama Ruhinda VII ambaye ni baba wa Balozi Ruhinda. Kuanzia mwaka 1450 mpaka 1963 Karagwe ilipita chini ya wafalme 21.
Kwa ufupi ni kwamba uchifu katika Karagwe ulikoma rasmi mwaka 1963 baada ya kupitishwa kwa sheria ya Bunge Februari 16, 1963, sheria ambayo ilisainiwa na Rais Nyerere Machi mosi, 1963. Kwa maelekezo ya sheria hiyo, matumizi yake yalianza kutekelezwa Januari mosi, 1963, yaani miezi miwili kabla ya sheria yenyewe kusainiwa.
Kuna sababu nyingi za kukoma kwa uchifu katika Karagwe, hapa nitaeleza sababu mbili. Moja ni hiyo ya sheria ya Bunge. Kuendeleza kitu kilichopigwa marufuku kisheria ni kosa, hivyo Wanyambo na waliokuwa watawala wao, walitii sheria hiyo. Sababu ya pili ni mchakato mrefu na mgumu wa kumpata mfalme (umukama au chifu). Pamoja na taratibu nyingine, mila ngumu sana ambayo ilimthibitisha Omukama madarakani ilikuwa ni kafara ya damu ya binadamu ambayo ilitirirshwa katika maji ya Mto Mwoga Mulinzi!
Kipindi cha ukoloni na pia kwa mafundisho ya Kikatoliki ambayo wafalme wengi waliamini, kufanya kafara ya damu lilikuwa kosa la jinai, hivyo kutofanyika kwake kuliondoa nguvu ya kumpata mfalme mwenye sifa. Kafara hiyo ya damu ndiyo ilimpa mamlaka mfalme kupitisha hukumu ya kifo kwa wakosefu wenye kustahili hukumu hiyo.
Kwa maana hiyo baada ya kufutwa kuwa utawala wa kijadi na baadaye kifo cha Omukama Ruhinda VII, Karagwe haikuwahi kuwa na chifu, kwa sababu kwanza hakuna aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo (wengi tunadhani mtu kuzaliwa wa kwanza ni tiketi ya moja kwa moja kuwa mrithi wa mfalme, ila si kweli. Yapo mambo mengine mengi yaliyoangaliwa), lakini pili, hata angeteuliwa, bado asingeweza kusimikwa kwa sababu mila maalumu za kumsimika zisingefanyika na hivyo kukosa sifa.
Kwa kuyajua yote hayo, ndugu au ukoo wa Balozi Ruhinda haukumteua yeyote kuwa mrithi wa chifu ili awe ‘chifu’ kwa jina tu, bila kazi yoyote. Lakini kitu cha msingi ni kwamba mfalme hakuteuliwa na kusimikwa na mfalme aliyepo hai, bali zilikuwepo koo maalumu katika himaya ambazo zilisimamia suala hilo.
Katika mazingira yale ya miaka 20 baada ya kupigwa marufuku utawala wa jadi, (Chifu Ruhinda alifariki mwaka 1983), isingewezekana kuyafanya haya. Hawakutaka kuwa na chifu wa “mchongo”.
Balozi Ruhinda hakupenda kuitwa chifu, maana hakuwahi kusimikwa uchifu. Hakupenda kuwa chifu wa mchongo. Yeye aliangalia mbele. Shemeji yake anayeitwa Dk Adrophine Gabone, kila alipojaribu kumuita chifu, yeye alimjibu “the past is a beautiful history, I focus on the present and future” (“Ya zamani ni historia nzuri, nazingatia ya sasa na yajayo”).
Hii inajibu ni kwa nini wenyeji wa Kagera, hususani Karagwe, hawana desturi ua kutoa uchifu wa heshima kwa viongozi na au watu maarufu. Ni kwamba uchifu haukuwa utamaduni wao.
Hata wangeamua kufanya kama makabila mengine kuwatunuku viongozi wakubwa zawadi ya ‘uzee wa mila’, bado ingeonekana ni maigizo kwa sababu himaya nyingi za maziwa makuu, zilikuwa na mfumo tofauti na huo wa kutumika wazee wa mila kwa maamuzi mbalimbali, wao walikuwa na ‘Bunge’ au Orukiko kama lilivyojulikana.
Kwa kutopenda mambo hayo ya kikoloni, Balozi Ruhinda alimwomba mwandishi wa makala hii kufikisha ujumbe wake kwa viongozi wa Afrika ya Mashariki kufikiria kuondokana na jina la Ziwa Victoria ambalo ni la mtawala wa kikoloni, kwamba tutafute jina moja la wenyeji wa kule, kwa mfano Lwelu, Nyanza na kadhalika.
Balozi Ruhinda hakupenda kujikweza kwa kuchukua hadhi au kuitwa kwa vyeo ambavyo si vyake, mfano kuitwa Chifu Ruhinda, tofauti na watu ambao kwa hakika si machifu ila wanalazimisha kuitwa hivyo, bila kujua kwamba ni kasumba ya kikoloni.
Ni bahati mbaya sana kwamba miezi ipatayo sita kabla Balozi Ruhinda hajafariki dunia, mwandishi wa makala hii pamoja wa ndugu yake, Frontline Ruhinda, walimwomba ruhusa ya kuandika kitabu cha historia yake akiwa bado hai ili isije kupotoshwa baada ya kifo chake, ila aligoma na kusema kama aliyoyatenda yalikuwa mema au mazuri basi yataandika historia yake. Balozi Ruhinda aliishi alichoamini, hakutaka makuu, alikataa majina na sifa za kikoloni, alikataa uchifu!