Dube amaliza utata Azam FC, ishu na Yanga iko hivi

HABARI mpya ni kwamba Prince Dube ameilipa Azam FC Sh500Mil na sasa yuko huru kujiunga na Yanga ambayo imekuwa ikihusishwa nae tangu asuse na kuondoka Chamanzi.

Mwanaspoti awali liliripoti kwamba Prince Dube ameukana mkataba wake na Azam FC unaoisha 2026 na akaondoka Chamanzi. Staa huyo alikwenda kushtaki kwenye Shirikisho la soka la Tanzania(TFF) na kesi yake ikaanza kusikilizwa Aprili 18.

Dube alipeleka kesi hiyo TF6F na Mwanaspoti liliripoti kwa mara ya kwanza taarifa hiyo pamoja na maisha ya kifahari anayoishi kwa sasa maeneo ya Salasala, Jijini Dar es Salaam chini ya ulinzi mkali wa mabaunsa wanaopeana zamu.

Katika kesi yake ya msingi, Dube alikuwa anadai kwamba  mkataba wake na Azam FC utaisha Juni 2024, siyo Juni 2026 kama wanavyodai Azam FC. Lakini Habari za ndani ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba baada ya kesi hiyo kurindima na uamuzi kutoka Dube ameamua kurusha taulo kwa kuwalipa Azam FC kununua mkataba huo kwa kiasi cha Sh700Milioni walichokuwa wakitaka Azam.

Staa huyo alikuwa akihusishwa na klabu kadhaa ikiwemo Al Hilal na Simba ambazo Azam waliwachomolea ofa zao. Inaelezwa kwamba watu wa karibu na Yanga wamemhifadhi mchezaji huyo Jijini Dar es Salaam na wameshampa ofa ya miaka miwili, wamemnunulia thamani za ndani za Sh30Milioni na ulinzi mkali wa saa 24.

Yanga licha ya kwamba hawajaenda rasmi kwa wamemuongezea ulinzi huo kwani hawataki abughudhiwe na wapinzani wao hususani Simba ambao wanamtaka kwa udi na uvumba.   

Kwenye taarifa ya Azam waliyoitoa kuhusu Dube kuomba kuvunja mkataba, Azam FC walisema mkataba wao na mchezaji huyo utaisha mwaka 2026 na Mwanaspoti limeambiwa wanamuuza Mil 700. Yeye amewaomba akawarudishia Mil 500 walizompa wakati wa usajili wakamalizana kiroho safi. Mwanaspoti linajua wikiendi hii watampa barua rasmi.

Dube alijiunga na Azam FC Agosti 2020 kwa kusaini mkataba wa miaka miwili hadi 2022. Mwaka mmoja baadaye, 2021, anasaini nyongeza ya mkataba hadi 2024.

Huu ndiyo mkataba ambao Dube alikuwa anadai kuutambua kabla mambo hayajabadilika. Lakini Azam FC waliwa wanasisitiza kwamba mwaka 2023 Dube raia wa Zimbabwe alisaini tena mkataba hadi 2026.Huu ndiyo mkataba ambao Dube aliukana lakini mambo yakamuelemea kwenye ‘mahakama’ ya TFF.

Wakala wa Prince Dube, Gerge Deda kutoka Zimbabwe amekuwa akikwepa kufafanua sakata la mteja wake lakini kesi ya Dube inataka kufanana na kesi kadhaa za wachezaji wa ligi ya Tanzania.

BERNARD MORRISON VS YANGA, 2020

Mchezaji huyo raia wa Ghana alijiunga na Yanga Januari 2020 akisaini mkataba wa miezi sita.

Baada ya miezi michache, Yanga wakatoa picha za mchezaji huyo akiwa na Kiongozi wa Yanga, Hersi Said, wakisema amesaini nyongeza ya mkataba.

Lakini mwisho wa msimu, Bernard Morrison akasema hakusaini nyongeza ya mkataba na hata zile picha aliomba apige ili kutuliza upepo.

Wakati sakata likiendelea, Morrison akatambulishwa na Simba.

Kesi ikaenda TFF na Yanga wakashindwa. Wakakata rufaa kwenye mahakama ya michezo, CAF, ambako pia walishindwa na Morrison akajiunga na Simba kwa ajili ya msimu wa 2020/21.

RAMADHAN SINGANO VS SIMBA

Mwaka 2015 chipukizi wa Simba kutoka timu yao ya vijana, Ramadhani Singano, alikana mkataba wake na klabu hiyo akisema haukuwa mrefu kama Simba walivyodai.

Yeye alisema mkataba wake na klabu hiyo ulikuwa wa miaka miwili na ndiyo ulikuwa unaisha baada ya msimu wa 2014/15.

Lakini Simba walisema alisaini miaka mitatu mkataba ulitakiwa kuisha baada ya msimu wa 2015/16.

Kesi ikaenda TFF na kupigwa sarakasi ya karne. Kesi ya msingi ılıtupwa na kuibuliwa kesi mpya ya Simba kutotimiza vipengele vya mkataba ikiwemo bima ya afya na makazi.

Hata hivyo, Simba walidai walikuwa wakimpa pesa hizo mchezaji huyo kwenye jumuisho la pamoja la mshahara wake.

Mchezaji alikana hilo na akataka Simba wathibitishe kwa stakabadhi za malipo.

Wakasema uangaliwe mshahara wa mchezaji huyo kwenye mkataba na iangaliwe pesa aliyokuwa akilipwa kama mshahara.

Ukweli ilionekana alikuwa akilipwa pesa nyingi kuliko mshahara wake, lakini hilo ongezeko halikuwa na maelezo ya maandishi.

Simba wakadai hilo ongezeko ndiyo fedha za makazi na afya, lakini walisema kwa mdomo tu kamati ikatupilia mbali kesi na kumtangaza Ramadhan Simba kuwa mchezaji huru akajiunga na Azam FC.

ATHUMAN IDD CHUJI VS SIMBA 2007

Hii ni moja ya kesi ambazo hazikuwahi kupata majibu hadi leo.

Chuji alikuwa mchezaji wa Simba tangu mwaka 2005 akitokea Polisi Dodoma.

Mwaka 2007 akasema mkataba wake na Simba ulikwisha na akasaini Yanga. Simba wakadai mkataba haukuwa umeisha hivyo kesi ikaenda TFF.

Simba wakatoa mkataba wao na Chuji akatoka mkataba wake. Chuji akaikana sahihi iliyokuwa kwenye mkakataba walioutoa Simba.

Ikabidi mikataba yote ipelekwe kitengo maalumu cha polisi cha kutambua sahihi za watu.

Majibu hayakuwahi kutoka hadi TFF ilipoamua kuuvunja mkataba na kumuacha mchezaji huyo huru akajiunga na Yanga. Sasa ni zamu ya Prince Dube ambaye Habari za ndani ya TFF ni kwamba ameshindwa kesi na kuamua kununua sehemu ya mkataba uliobaki Azam FC. Endelea kufuatilia Mwanaspoti tutakupa kila kinachoendelea.

Related Posts