Na Mwandishi WETU
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imekuwa mshindi wa 7 kati ya Mamlaka 84 za Maji nchini kwa ufanisi wa utoaji wa taarifa za taasisi kwa umma na kupatiwa Cheti cha Pongezi.
Cheti hicho cha Pongezi kwa DUWASA kimepokelewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma DUWASA Bi. Rahel Muhando kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph kutoka kwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye wakati akifunga Kongamano la Pili la Maendeleo ya Sekta ya Habari na Kikao Kazi cha 19 cha Maafisa Habari wa Serikali vilivyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
Ushindi wa DUWASA ni kwa mujibu wa Tathmini ya Utendaji Kazi wa Vitengo vya Mawasiliano na Habari katika Mamlaka za Maji uliyofanywa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Idara ya Habari Maelezo ya mwaka 2023/2024.
Maafisa Mawasiliano wanne wa DUWASA wameshiriki Kongamano hilo lililofunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Juni 18, 2024, ambaye amevitaka Vyombo vya Habari na Maafisa Mawasiliano nchini kuandika habari za uwajibikaji, uzalendo za kimkakati na zenye uchambuzi wa kina katika kuwahabarisha wananchi kuhusu maendeleo na utekelezaji wa miradi.
Kongamano na Kikao Kazi kwa Maafisa Habari kote nchini vimeanza Juni 18 hadi Juni 22, 2024 lengo ni kuwajengea uwezo Maafisa Mawasiliano hao katika masuala ya Teknolojia ya Habari, weledi wa kuandika, kuchapisha na kusambaza habari kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na kuwa washauri wa namna bora ya utoaji wa taarifa za taasisi kwa umma.