Mufindi. Serikali ya Mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), tayari imefanya shughuli mbalimbali kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa ambao unatarajiwa kufanyiwa Oktoba mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba ameyasema hayo Leo Juni 22,2024 wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru 2024 katika kijiji cha Nyingo kata ya Itandula Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi mkoani hapa ukitokea Njombe.
Aidha, Serukamba ametaja shughuli za maandalizi ambazo tayari zimefanyika kuwa ni uhakiki wa maeneo ya utawala na kubaini ya idadi ya wapiga kura, vituo vya kupigia kura, ukaguzi wa vifaa vya kupigia kura ikiwemo mihuri na kuwasilisha majina ya waratibu wa usimamizi wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa ngazi ya halmashauri.
Pia amesema kuwa licha ya kuendelea kukamilika shughuli hizo za uhakiki, lakini wameendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika uchaguzi huo kwa sababu ni haki yao ya kikatiba kuchagua na kuchaguliwa katika uchaguzi huo.
“Matarajio yangu ni kuwa Mwenge wa Uhuru wa mwaka huu 2024 utawakumbusha wananchi kuhusu haki yao ya kikatiba kushiriki kuchagua kuchaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa, kwa sababu Serikali inaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika uchaguzi huo,” amesema Serukamba
Katika hatua nyingine, Serukamba amesema kuwa Mwenge utapitia jumla ya miradi 50 yenye thamani ya Sh665.6 bilioni na utakimbizwa umbali wa kilomta 873 .
Kwa upande wake, kiongozi wa Mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa, Godfrey Mnzava amesema viongozi hao wanatakiwa kuhakikisha taratibu zote ambazo zinatakiwa kufuatwa zinafuatwa ikiwemo matumizi ya sahihi ya fedha ambazo zinatolewa na Rais Samia Suluhu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
“Wakati tunapita kutembelea miradi viongozi mnapaswa kuhakikisha tunakuta nyaraka halisi pamoja na nakala ambazo zimechapishwa sambamba na wataalam wote katika maeneo ya miradi ambao watakuwa na maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo,” amesema kiongozi huyo.