SIMBA na Coastal Union wameingia kwenye mzozo. Msimbazi wamemtangaza Beki Lameck Lawi kama mchezaji wao mpya juzi usiku.
Muda mfupi badae wenzao wakajibu kwamba siyo kweli, hawatambui usajili huo kwa madai kwamba kuna makubaliano walikubaliana wakati anasaini mkataba wa awali na hayajatekelezwa.
Coastal Union wamesisitiza kusitisha biashara hiyo na wekundu hao, kwa kile ilichoeleza kukiukwa kwa makubaliano ya pande hizo tatu. Lakini kuna ukweli uko hivi;
Wanadai kwamba ilikubaliana na Simba kumlipa Lawi fedha zake mpaka kufika Mei 14,2024 lakini wekundu hao hawakufanya hivyo.
Madai ya pili ni kwamba Simba ilitakiwa kuilipa Coastal Union fedha ya manunuzi ya mchezaji huyo, mpaka kufika Mei 31,2024 iwe imekamilisha malipo hayo.
Hata hivyo Simba inaelezwa kulipa fedha hizo Juni 10 ikiwa imelipa sehemu kubwa ya fedha hizo na Coastal Union kuamua kusitisha mauziano hayo kisha kurudisha fedha zote za wekundu hao. Lawi aligoma kufafanua chochote jana lakini mtu wake wa karibu aliliambia Mwanaspoti kuwa kimenuka.
“Lawi ni kweli kasaini mkataba wa awali, makubaliano ilikuwa ni kumuingizia Sh.130 milioni lakini wao wameweka Sh.50 milioni,”kilidokeza chanzo chetu.
“Coastal Union imemtaka mchezaji arudishe kiasi hicho cha fedha ili waendelee na mambo mengine ikiwa ni pamoja na kuvunja biashara hiyo kufanyika,”aliongeza.
“Imetushtua kuona mchezaji anatambulishwa wakati biashara haikukamilika na fedha zilizoingizwa kwenye akaunti ya mchezaji zimerudishwa,”alihoji.
Habari za ndani ni kwamba kumeibuka pia mzozo baina ya viongozi wa Coastal Union huku ikielezwa kuwa baadhi hawakushirikishwa kwenye dili hilo na hawakujua hata kiasi ndio maana wakaja juu.
Lakini ushiriki wao kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa msimu ujao nao umeibua ishu kwani mpaka sasa hawajapata mbadala wake kwa haraka kwenye safu ya ulinzi kama walivyokuwa wamedhani hivyo wanaona pia ni bora wakaendelea kubaki na mchezaji huyo.
Mbali na hilo pia inaelezwa wakati dili hilo linafanyika ikaibuka ofa kubwa ya kutoka Ubelgiji ambayo imewachanganya mabosi wa Coastal Union na kuona ni vyema ikasitisha dili mpango wa kumuuza kwa Simba ili wavute parefu.
KWANINI SIMBA WALIMTAMBULISHA HARAKA?
Simba ilikuwa inaendelea na zoezi la kutema wachezaji ambao haitakuwa nao msimu ujao, lakini ghafla ikatoa tangazo kwamba kuna ujio mpya.
Habari zinasema kwamba Simba waliamua kumtoa hadharani kwa haraka mchezaji huyo baada ya Coastal Union kurejesha fedha za malipo ya awali walizopewa na ndio maana baada hata utambulisho wa Simba haukuwa na picha za mchezaji kwani alikuwa hajaandaliwa kutambulishwa rasmi.
Hata video za mbwembwe za usajili wa Lawi hazikuwepo kwenye utambulisho wa Simba tofauti na ilivyozoweleka awali.
Katibu Mkuu wa Coastal Union, Ayoub Omar ameliambia Mwanaspoti kuwa; “Haya yalikuwa ni makubaliano na yapo mambo ambayo tuliyafanya kuwa siri ya kimkataba,itoshe kwa kusema kwamba dhamira ya sisi kufanya biashara na wenzetu wa Simba ilikuwepo lakini kuna mambo waliyakosea na tunahaki ya kusema basi tukwamie hapa.”
“Hatuwezi kusema kwamba Lawi hatauzwa lakini kwa nukta hii ya hapa kati yetu na Simba tumeona yaishie hapa, kila kilicho chao tumewapatia na sisi tutabaki na mchezaji wetu.”
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori amesema; “Hoja yao ni rahisi sana kwamba huyo mchezaji fedha yao ilitakiwa ilipwe yote Mei 31 mwaka huu, na wao baada ya kuona haijakamilika Juni 17 waliwaandikia barua kusitisha biashara yao kutokana na sisi kushindwa kulipa.”
“Wakati wao wanaleta barua Juni 17 sisi tulikuwa tayari tumekamilisha malipo yote Juni 10 hivyo wao wameleta barua sisi tukiwa tayari tumelipa, lakini cha kushangazwa barua yao iliandikwa Mei 14 wakati ukomo wa kulipa ulikuwa Mei 31,”alisema Magori.
Alisema kanuni za Fifa inazitaka klabu zikishindwa kulipa madeni kwa siku husika zinapewa siku kumi ili kukamilisha hilo hivyo Coastal Union walitakiwa kutoa siku kumi kuanzia Juni Mosi kuwataka Simba walipe na kama wangeshindwa kufanya hivyo ndio mkataba ungevunjika.
“Coastal Union hawakufanya hivyo ndipo walipoibuka Juni 17 na sisi tukapitia nyaraka na kuwajibu Juni 18 kwa kuwakumbusha vipengere vyote katika mkataba wa makubaliano wa uuzwaji ambao ulisainiwa kati ya Simba na Coastal tulikubaliana kwamba mchezaji huyo lazima aletwe kwaajili ya vipimo vya Afya,” alisema na kuongeza;
“Ndio mauzo yafanyike lakini mchezaji huyo hakuletwa kwaajili ya vipimo kwasababu alikuwa na timu ya taifa Indonesia baadaye akasafiri kwenda Zambia lakini pamoja ya hayo yote kwa mchezaji kuto kufanya vipimo kama mkataba ulivyosema tulienda kulipa fedha zote Coastal Union pamoja na mchezaji,”alisema.
Magori alisema hayo yote yanatokea kwasababu kuna dili limetua Coastal Union kwa mchezaji huyo kutakiwa kuuzwa nje hivyo amesisitiza kuwa hilo dili lisiwe sababu ya kusababisha mkataba wao ukavunjika.
“Tutafuata taratibu zote na nyaraka zipo, Sheria zipo tutafika mpaka FIFA kwasababu ndio mpira ulipo hauishii Karume, Simba ni timu kubwa haiwezekani tukatangaza mchezaji wakasema tunafanya ubabaishaji, hii kwakweli imetusumbua sana na ni vitu ambavyo tunaviona ni vya ajabu sana kwenye mpira,” alisema na kuongeza;
“Katika hali ya kawaida namna hii hatukutegemea hili litokee lakini kwasababu limetokea tutalikabili kwasababu tunajua taratibu zote za mpira na sheria tunazifahamu kwakifupi mchezaji ameshasajiliwa, mikataba yote tunayo na kwasababu fedha hizo hakulipwa mkononi nyakara zote na mawasiliano vithibitisho vyote vipo,” aliema na kuongeza;
“Na hata hiyo klabu inayotaka kumnunua huyo mchezaji kama mkiifahamu ishaurini ije Simba tu kwasababu tukishtaki tutashtaki klabu zote mbili sio Coastal Union tu na rungu la Fifa wanalijua na mahakama ya mpira inajulikana sisi tutafuata sheria,”alisema Magori.