NYOTA wa kimataifa, Clara Luvanga anayekipiga Al Nassr ya Saudia huenda msimu ujao akaibukia Marekani baada ya kuanza mazungumzo na moja ya timu za nchini humo.
Ikumbukwe Clara msimu uliopita, Nassr inayomiliki pia timu ya Ligi Kuu ya Saudia kwa wanaume anayoichezea Cristiano Ronaldo ilivunja mkataba wa straika huyo na Dux Lugrono ya Hispania ikiwa miezi mitatu tu asajiliwe huko.
Nyota huyo bado ana mkataba wa miaka miwili na miamba hiyo ya soka ya Saudia na kuna ofa za timu tatu kutoka Marekani zinazotaka kuvunja mkataba na klabu hiyo ili kumnasa.
Akizungumza na Mwanaspoti jana, Clara alisema ni kweli timu hizo za Marekani zimemfuata na kama mambo yatakwenda vizuri basi atatimkia huko.
“Siwezi kutaja ni timu gani, ila muda ukifika mtajua lakini ni kweli ni timu kubwa Marekani zimenitafuta nami bado nina mkataba na Al Nassr, iwapo tutafikia makubaliano basi naweza kujiunga na moja wapo,” alisema Clara.
Ingawa Clara hakutaja timu zinazomhitaji, lakini Mwanaspoti linafahamu Orlando Pride, Chicago Red Stars na Boston Breaker ni miongoni mwa timu zilizompeleka ofa za kumtaka.
Orlando, ndio watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Marekani na maskani ya klabu hiyo ni Orlando, Florida ikiwa inayoongoza hadi sasa msimamo ikicheza michezo 14 na pointi 32 na inatumia Uwanja wake wa nyumbani Inter&Co Stadium.
Kama Clara atasajiliwa timu hiyo ambayo inafundishwa na Muingereza, Sebastian Tony huenda akakutana na ushindani kwenye eneo la ushambuliaji ambalo hadi sasa Mzambia Barbra Banda anaongoza akiwa na mabao 10.
Kwa Chicago Red Stars inafundishwa na Mjamaica Lorne Donaldson na msimu wa mwaka 2011 iliwahi kuchukua ubingwa wa ligi hiyo na iwapo ataamua kutua Boston Breakers basi ataungana na timu ambayo ilishiriki Ligi hiyo msimu wa 2017 kwani kwa sasa ipo Daraja la Kwanza na inatumia Uwanja wa Jordan Field.