Mahujaji zaidi ya 1,000 wafariki Makka, Bakwata yasema…

Dar es Salaam. Wakati taarifa zikitolewa kuhusu mahujaji zaidi ya 1,000 kufariki wakati wa ibada ya Hijja nchini Saudi Arabia, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Alhaj Nuhu Mruma amesema kati ya waliofariki hakuna Mtanzania.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari mbalimbali vya kimataifa,  vifo hivyo vimetokana na  joto kali lililofikia nyuzi joto 51.8 kwa wiki hii kwenye mji wa Makka.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa zaidi ya nusu ya waliofariki ni waumini ambao hawakuwa na vibali maalumu kuingia nchini humo kwa ajili ya ibada hiyo ambayo ni nguzo ya tano ya dini ya Kiislam.

Akizungumza na Mwananchi leo Juni 22, 2024, Alhaj  Mruma amesema kuwa kwa sasa Watanzania wote waliokwenda kwa ajili ya ibada ya Hijja,  wanatoka Makka na wanaelekea katika Mji wa Madinna.

“Kwa mahujaji wote waliotoka Tanzania hakuna aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa katika ibada hiyo na wanatarajiwa kurudi nchini ifikapo Juni 24, 2024,” amesema.

Takriban nchi 10 zimeripoti vifo hivyo huku Misri ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya vifo vya takribani mahujaji 658.

Indoneshia imeripoti vifo takribani mahujaji 183 huku Pakistan vikiripotiwa vifo 58 kati ya mahujaji 150,000 kutoka katika nchi hiyo.

Nchi nyingine ambazo tayari mamlaka zake zimethibitisha ni pamoja na Malaysia, India, Jordan, Iran, Senegal, Tunisia, Sudan.

Pamoja na vifo hivyo pia maelfu ya watu wanapatiwa  matibabu katika hospitali mbalimbali nchini humo.

Hijja hufanyika kila mwaka nchini Saudi Arabia kwa ajili ya kutekeleza nguzo hiyo ya  tano ya imani ya dini ya Kiislam.

Ibada hiyo inapaswa kufanywa mara moja katika umri wa muumini na ni ibada maalumu kwa kila mwenye uwezo wa kufunga safari kwenda katika mji huo Mtukufu.

Related Posts