Unguja. Zaidi ya miezi mitatu sasa makontena 25 ya vileo yameendelea kushikiliwa katika Bandari ya Malindi, Zanzibar.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Bodi ya Vileo Zanzibar kuliagiza Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) kuzuia uingizaji wa bidhaa hizo kwa madai wahusika hawana vibali vya kuingiza bidhaa hiyo.
Sakata la uingizaji pombe Zanzibar lilibuka Februari, 2024 baada ya aliyekuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Simai Mohamed Said kueleza uwepo wa uhaba wa pombe akisema unahatarisha sekta ya utalii.
Simai alitoa kauli hiyo alipokutana na wadau wa utalii, akiituhumu Bodi ya Vileo kuzinyima vibali kampuni zenye uzoefu na kuzipa ambazo hazina uwezo. Siku mbili baadaye waziri alijiuzulu katika nafasi hiyo.
Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) limesema jana Juni 21, 2024 kuwa makontena 25 yakiwa na bidhaa za vileo yanayoendelea kuzuiwa katika Bandari ya Malindi, Unguja kumetokana na Bodi ya Udhibiti wa Vileo Zanzibar kutotoa vibali vya uingizaji kwa kampuni tatu zilizoingiza bidhaa hizo visiwani humo.
Mkurugenzi wa ZPC, Akif Ali Khamis, amekiri kuendelea kushikilia makontena hayo kutokana na barua iliyotolewa na bodi ya vileo ikielekeza wafanye hivyo kwani wahusika hawana kibali.
“Ni kweli kampuni tatu ikiwemo One Stop, Sicoch na kampuni ya ZMMI zimeingiza vileo lakini tulipokea barua kutoka bodi ya udhibiti wa vileo wakitutaka kuendelea kuzuia mzigo walioingiza kwa sababu hawajapewa vibali vya uingizaji wa vileo Zanzibar,” amesema.
Hata hivyo, amesema tozo za ushuru za mzigo tangu kuingizwa katika bandari hiyo zinaendelea kulipwa na wahusika na gharama zake zitaamuliwa kwa mujibu wa sheria lakini mpaka sasa mzigo huo unaendelea kushikiliwa hadi uamuzi mwingine utakapotolewa.
Msimamo wa kuendelea kushikilia makontena hayo unakwenda kinyume cha hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Zanzibar ambayo ilisema Sheria ya Vileo ya Zanzibar namba 9 ya mwaka 2020 inakwenda kinyume cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Katika hukumu ya Jaji George Kazi, alisema kifungu cha 33 (1) cha sheria ya vileo kinavunja Katiba ya Zanzibar na sheria ya ushindani na kumlinda mlaji namba tano ya mwaka 2018 na kwa msingi huo alisema kampuni zote za uingizaji wa vileo zinapaswa kupewa vibali ili kuzingatia matakwa ya Katiba ya Zanzibar.
Wakili aliyekuwa akisimamia kesi dhidi ya walalamikaji, Hassan Kijogoo alisema maamuzi ya Mahakama Kuu yametokana na kifungu cha 12 (1) (2) cha Katiba ambacho kinasema hakuna sheria itakayokuwa na kifungu chochote ambacho ni ubaguzi wa moja kwa moja.
Wakili Kijogoo, alisema kwa msingi huo, mamlaka za Serikali zinapaswa kuruhusu makontena zaidi ya 25 yanayoendelea kushikiliwa katika Bandari ya Malindi, Unguja.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa bodi ya vileo, Juma Choum hakuwa tayari kuzungumzia jambo hilo.