Dar es Salaam. Meli kubwa ya MSC ADU V iliyobeba makasha 4,000 imetia nanga katika bandari ya Dar es Salaam, ikiwa ni kwa mara kwanza kwa meli yenye mzigo mkubwa wa makontena kuwasili Tanzania.
MSC ADU V iliyotengenezwa mwaka 2005 ina urefu wa mita 294.12 unaokaribiana na viwanja vitatu vya mpira wa miguu imetia nanga leo Jumamosi Juni 22, 2024.
Akizungumza na wanahabari Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Abeid Gallus amesema ujio wa meli hiyo umetokana na maboresho yaliyofanyika katika bandari hiyo na uwekezaji wa Kampuni ya DP- World.
Gallus amesema bandari ya Dar ea Salaam imefanya maboresho katika kina cha na ununuzi wa vitendea kazi vya kisasa.
Amesema mwanzo kulikuwepo na kina cha mita nane hadi 13.7 sasa hivi kipo 14.5 chenye uwezo wa kuingiza meli yenye urefu wa mita 305 na kina 13.5.
“Hii ni historia kwetu hapo mwanzoni tulikuwa tunaingiza meli zenye urefu wa mita 267, tumeongeza uwezo wa bandari yetu ya Dar es Salaam katika uingizaji wa meli.
“Uwezo wa utendaji kazi wa bandari ya Dar es Salaam utazidi kuimarika zaidi kwa sababu hivi sasa tuna mwekezaji mpya DP World aliyeanza kazi na mabadiliko yameonekana mfano ni meli hii kubwa,”amesema Gallus.
Gallus amefafanua kuwa katika usafirishaji ukipokea meli kubwa uongeza kiwango cha mizigo unaokuja katika bandari husika sambamba na kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo.
“Wateja wetu watalipa kiwango kidogo cha fedha kusafirisha mizigo yao katika bandari ya Dar es Salaam. Meli itashusha mzigo ndani ya siku tano itapakua na kupakia kisha kuondoka,” amesema Gallus.
Kwa mujibu wa Gallus, ambaye ni Meneja wa Mizigo Mchanganyiko wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), meli ya mwisho kubwa iliyobeba makasha kutia nanga katika bandari ya Dar es Salaam ilikuwa na urefu wa mita 267 ilibeba makasha 3,500.
Aprili 18, 2022 bandari ya Dar es Salaam imepokea meli aina ya Frontier Ace iliyobeba magari 4,041, ikiwa ni ya kwanza yenye mzigo mkubwa wa magari kupokelewa tangu kuanzishwa kwa TPA.
Januari 16, 2024 meli kubwa ya abiria ya Norwegian Cruise Line Dawn yenye urefu wa mita 294 iliyobeba abiria 2,210 kutoka Canada ilitia nanga katika bandari hiyo, ikitajwa kuwa ni meli kubwa kuwasili ikibeba abiria.
Katika maelezo yake kwa wanahabari, mapema mwaka huu, mkurugenzi wa bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho alisema ujio wa Norwegian Cruise Line Dawn umechagizwa na maboresho yaliyofanyika katika bandari hiyo, na wanatarajia kupokea meli kubwa zaidi kwa siku za usoni.