Rais Dk. Samia Hassan azungumzia Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Tanzania na Guinea Bissau

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Guinea Bissau zina fursa nyingi za kushirikiana katika kukuza uchumi wa buluu na kilimo cha korosho, zao linalolimwa katika nchi zote mbili.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Juni 22, Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya mazungumzo na serikali ya Guinea Bissau, Rais Dk. Samia alieleza kuwa nchi zote mbili zina eneo kubwa la bahari, hivyo zimepanga kushirikiana katika kukuza uchumi wa buluu.

Ushirikiano wa Kiuchumi na Uwekezaji

Rais Dk. Samia alibainisha kuwa nchi hizo zitashirikiana katika kukuza maeneo huru ya uwekezaji (EPZA). Pia, alifafanua kuwa Rais wa Guinea Bissau, aliyepo nchini kwa ziara rasmi, atatembelea maeneo hayo na pia kukagua Reli ya Kisasa (SGR) inayoenda Burundi, DRC, na maeneo mengine ya Afrika.

“Nchi hizi zimepanga kukuza biashara baina yao, hasa katika zao la korosho kwa kuongeza tafiti za kukuza uzalishaji na kuongeza thamani,” alisema Rais Dk. Samia.

Kuimarisha Uhusiano wa Kudumu

Ziara hii ni msingi wa kuimarisha uhusiano wa kudumu ulioasisiwa na waasisi wa mataifa hayo, ambao walikuwa na dhamira moja ya umajumui na kupinga ukoloni. Rais Dk. Samia alikumbusha kuwa Tanzania ilikuwa Mwenyekiti wa nchi wanachama wa ukombozi, ambao baadaye uliunda Umoja wa Afrika. Ziara ya Rais wa Guinea Bissau imeleta fursa ya kufanya mazungumzo na kujadili mambo yaliyoasisiwa na waasisi wa mataifa hayo.

Mambo Muhimu Yaliyozungumzwa

Rais Dk. Samia alitaja baadhi ya masuala muhimu waliyoyazungumza, ikiwa ni pamoja na masuala ya kiuchumi, kikanda, ukuzaji wa amani na usalama, biashara na uwekezaji, ushirikiano katika sekta ya kilimo cha korosho, afya, elimu, ulinzi na usalama, pamoja na masuala ya kimataifa kama vile tishio la ugaidi na kupambana na dawa za kulevya.

“Bara lipo katika mbio za kuhakikisha biashara inafunguka Afrika, jambo litakalochochea ongezeko la viwanda. Tumekaa pamoja kuhakikisha eneo hilo linatumika ipasavyo,” alisema Rais Dk. Samia.

Ushirikiano wa Kibiashara

Rais Dk. Samia aliongeza kuwa wamekubaliana kushirikiana na nchi nyingine za Afrika kuhakikisha bei za bidhaa za kilimo zinapata bei nzuri kwa kutengeneza sauti moja. Alisema nchi hizo mbili zina eneo kubwa la mwambao wa pwani na zote zipo katika nafasi nzuri ya kufanya biashara na zinapakana na nchi zisizo na mwambao, hivyo fursa za utalii na uvuvi hasa wa fukwe zipo wazi.

Uwekezaji na Biashara

Rais Dk. Samia alieleza kuwa uwekezaji na biashara ni eneo muhimu walilojadili na wamesaini mkataba wa kuanza mazungumzo kwenye eneo hilo.

Kauli ya Rais wa Guinea Bissau

Rais wa Guinea Bissau, Umaro Sissoco Embaló, alisema: “Nimefurahi kuwa na ziara Tanzania na naleta salamu za dhati za watu wa Guinea Bissau.”

Alieleza kuwa mataifa hayo yalishirikiana katika kuondoa ukoloni na ubaguzi wa rangi, kazi ambayo ilifanyika jijini Dar es Salaam. Alikumbusha kuwa Mwalimu Julius Nyerere alitembelea Guinea Bissau mwaka 1979 na kupokelewa na watu wake kwa medali ya heshima.

Kuimarisha Mahusiano

Rais Embaló alisisitiza umuhimu wa kubadilisha mahusiano yawe imara zaidi, akisema Guinea Bissau haiwezi kusahau kuhusu Tanzania na kuwa shuleni, wanafundishwa kuhusu Mwalimu Nyerere. Aliahidi kuwa tayari kusaidia Tanzania na alimhakikishia Rais Dk. Samia kuwa mkataba uliosainiwa hautakwama.

Kualika Wanafunzi wa Kiswahili

Rais Embaló pia alisema atawaleta wanafunzi wa Kiswahili kuja kujifunza lugha hiyo ambayo ni muhimu kwa Afrika. Alimwalika Rais Dk. Samia kufanya ziara nchini Guinea Bissau na kuangalia muda mwafaka wa kwenda nchini humo.

Kwa kumalizia, Rais Dk. Samia alisema ushirikiano huo utasaidia kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi wa nchi zote mbili.

Related Posts