SAA chache baada ya kutemwa na Simba, kiungo Saido Ntibazonkiza amepigiwa simu na moja ya vigogo wa juu wa Namungo akitaka huduma yake kwa msimu ujao.
Saido aliyemaliza msimu uliopita akiwa kinara wa mabao kwa Simba akifunga 11 na kwa sasa yupo kwao Burundi, lakini amepigiwa na kigogo wa Namungo, huku akitajwa pia Coastal Union na KMC.
MSHAMBULIAJI wa Singida Black Stars (zamani Ihefu), Ismail Mgunda yupo katika mazungumzo ya kujiunga na Mashujaa ya Kigoma.
Nyota huyo aliyewahi kuichezea Tanzania Prisons, awali alifuatwa na Simba waliohitaji saini yake ila kwa sasa inaelezwa hakuna mawasiliano yanayoendelea baina yao hivyo Mashujaa kuingilia dili hilo.
KLABU ya KMC imeanza mazungumzo ya kumpa mkataba mpya kocha mkuu wa kikosi hicho, Abdihamid Moallin kwa ajili ya msimu ujao.
Kocha huyo wa zamani wa Azam FC, alijiunga na KMC Julai 12, 2023 akichukua nafasi ya Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na kuonyesha uwezo mkubwa jambo lililowavutia mabosi hao kutaka kuendelea naye.
BAADA ya kushindwa kupanda Ligi Kuu, Biashara United inayoshiriki Championship imeanza harakati za kumnasaa aliyekuwa kocha wa JKT Tanzania, Malale Hamsini kwaajili ya msimu ujao.
Inaelezwa Biashara huenda isiendelee na Aman Josia kama kocha mkuu kwa msimu ujao na tayari wamefungua mazungumzo na Malale wakiamini ubora na uzoefu wake katika Ligi ya Championship.
BAADA ya kushuka daraja, Mtibwa Sugar imeelezwa ipo mbioni kumpa kocha msaidizi wa timu hiyo, Awadh Juma ‘Maniche’ kuinoa timu hiyo jumla kama kocha mkuu kwa Ligi ya Championship.
Inaelezwa mabosi wa timu hiyo hawana mpango wa kutafuta kocha mpya baada ya kuondoka Zubery Katwila hivyo kumuona Maniche mtu sahihi wa kuisaidia kuirejesha Ligi Kuu Bara.
MSHAMBULIAJI wa Fountain Gate (zamani Singida FG)Francis Kazadi huenda akaachana na timu hiyo msimu ujao.
Nyota huyo aliyejiunga na timu hiyo, Januari 7, 2023 akiwa mchezaji huru, hana mpango kuendelea kukichezea kikosi hicho ikielezwa sababu kuu ni malimbikizo makubwa ya mshahara anazodai.
KAGERA Sugar, iko katika mazungumzo ya kumpata kiungo wa Mlandege ya Zanzibar, Abdallah Kulandana kwa ajili ya msimu ujao.
Nyota huyo amekuwa katika kiwango bora hususani kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi jambo linalowafanya mabosi wa timu hiyo kuanza mipango mapema ya kuiwinda saini yake.