Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limeipongeza Serikali kwa kuongeza kiwango cha malipo ya mkupuo ya Pensheni kwa Wastaafu kutoka asilimia 33 ya sasa mpaka 40 kwa wafanyakazi waliokuwa walipwa asilimia 50 kabla ya mifuko kuunganishwa na asilimia 35 kwa watumishi ambao walikua wakipokea asilimia 25 kabla mifuko hiyo kuunganishwa
Pongezi hizo zimetolewa na Rais wa TUCTA, Ndg. Tumaini Peter Nyamhokya katika mkutano na Waandishi wa Habari Mjini Morogoro wakati wa Kikao cha Kamati ya Utendaji cha Shirikisho hilo ambapo alieleza kuwa, Nyongeza hizo zitapunguza kwa kiasi malalamiko ya wafanyakazi ambayo yamekuwepo kuhusu Kikokotoo cha awali.
Aidha TUCTA wameishauri Serikali kuangalia upya na kuweka usawa katika nyongeza ya mkupuo ya kikokotoo kwa watumishi ambao wameguswa na mabadiliko haya ya Sheria ya Watumishi wa Umma.
“Watumishi hawa wote ni kundi moja la wafanyakazi hii inatokana na ukweli kwamba watumishi wa UMMA waliokuwa PPF mfuko wao ulikuwa imara na baada ya kuunganishwa umesaidia kufungua mfuko wa PSSSF lakini hao wanachama ndio sasa imependekezwa walipwe mkupuo wa asilimia 35 na wenzao wanalipwa asilimia 40”
Katika hatua nyingia TUCTA pia imeishauri Serikali kufanya mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii kwa watumishi wa Sekta Sinafsi kutokana na kwamba, mabadiliko yaliyopendekezwa hayo hayajagusa wanufaika wa mfuko wa NSSF bali PSSSF pekee.