Uwanja wa ndege watajwa kuifungua Mbarali kiuchumi

Mbeya. Kuwapo kwa uwanja wa ndege katika kijiji cha Mulungu kilichopo Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya,  kumetajwa kuinua uchumi na kufungua fursa za ajira kwa vijana hasa kwenye sekta ya utalii.

Uwanja huo wenye urefu wa kilomita 1.2 ambao umezinduliwa Juni 20, umejengwa na Serikali kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa ushirikiano na shirika lisilo la kiserikali la Six Rivers Africa na tayari umeanza kutumika.

Uwanja huo una uwezo wa kupokea ndege kubwa zinazoweza kutua pale inapotekea dharura angani ili kuokoa maisha ya watu.

Akizungumzia maendeleo hayo, mkazi wa kata ya Miomboni wilayani humo, Diana Yonah amesema matarajio yao ni kutumia fursa ya kupokea wageni na watalii kwa kuuza bidhaa zao za kilimo.

“Licha ya kujishughulisha na kilimo, pia tumesoma, hivyo tunaweza kupokea wageni wakiwamo watalii kutoka mataifa ya nje na kuwaongoza katika hifadhi hii,” amesema Diana.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Godi Mabena amesema kwa sasa wananchi wa Mulungu watanufaika kwa kujiinua kiuchumi kwa sababu wataweza kusafirisha bidhaa zao nje ya mkoa huo na kuiweka Mbarali kwenye ramani ya kibiashara. 

Mabena ametumia fursa hiyo kuomba uboreshwaji wa miundombinu ya barabara kijijini hapo yenye urefu wa kilomita 10 ili kurahisisha shughuli za kibiashara na kutangaza wilaya hiyo.

“Serikali ya kijiji ipo tayari kutoa ushirikiano kwa wahifadhi na shirika la Six Rivers Africa ambao wameonyesha dhamira ya kuinua maendeleo ya wananchi wangu,” amesema Mabena.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha, Godwel Meing’ataki amesema mafanikio hayo ni utekelezaji wa makubaliano ya kimkataba baina ya Serikali na shirika hilo.

Amesema pamoja na ujenzi wa uwanja huo, pia kitajengwa chuo cha utalii ambacho kitatoa mafunzo mbalimbali ikiwamo elimu ya uhifadhi na utalii na kuwanufaisha wananchi wa maeneo ya jirani.

“Tunatarajia kuona watalii wengi wakimiminika na kuanzia kesho Ijumaa baadhi wataanza kuja, hivyo hii itafungua uchumi wa Taifa na mtu mmoja mmoja, Serikali imejitahidi kutengeneza na kuboresha mazingira katika sekta ya utalii.

“Lakini katika eneo hili la Ikoga ulipo uwanja huu, tumejenga zizi la kisasa, tunahitaji ulinzi katika hifadhi hii kwani tumeona mara kadhaa tembo wakisumbua hadi kutumia nguvu kubwa kuwatawanya,” amesema Meng’ataki.

Ameongeza kuwa kutokana na jitihada hizo za Serikali, amewaomba wananchi kutoa ushirikiano kulinda eneo la hifadhi na kwamba tayari uwanja huo umesajiliwa  Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini, akieleza kuwa haitakuwa vema mifugo kuingia maeneo hayo na kuleta taharuki kwa watalii.

“Itashangaza sana kuona mwingiliano wa mifugo, wananchi kuvua samaki na kufanya ujangili katika eneo hili la hifadhi na kusababisha taharuki kwa watalii,” amesema kamishna huyo.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbas, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Kanali Denis Mwila amesema uwanja huo una uwezo wa kupokea ndege kubwa kwa dharura na kupongeza shirika la Six Rivers Africa kwa mchango wao kufanikisha ujenzi huo.

“Serikali inajali na kuthamini uhifadhi na utalii, tutaendelea kuboresha miundombinu na kufungua milango katika lango la utalii kusini, tunaomba kuwapo ulinzi na usalama katika eneo hili,” amesema Mwila.

Naye Mwenyekiti wa shirika la Six Rivers Africa, Glenn Turner ameishukuru Serikali  kuwaamini katika kushirikiana kutengeneza uwanja huo, akieleza kuwa wataendelea kujenga miundombinu ya maendeleo ikiwamo chuo cha mafunzo ya uhifadhi.

“Ndani ya wiki chache zijazo, chuo hicho kitaanza kikilenga kunufaisha wananchi wa maeneo haya, Six Rivers Afrika tumejipanga kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo,” amesema Turner.

Related Posts