Wachimba madini waonywa matumizi holela ya zebaki

Dodoma.  Wachimbaji wadogo wa madini nchini wametakiwa kuzingatia matumizi sahihi ya kemikali ya zebaki inayotumika kuchenjulia madini,  ili wajiepushe na madhara yanayotokana na matumizi holela ya kemikali hiyo ikiwemo magonjwa ya ngozi, figo, saratani, kifua na hata kifo.

Ushauri huo umetolewa leo Jumamosi Juni 22, 2024 na Baraza la Taifa la usimamizi wa mazingira (NEMC) na Ofisi ya  Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali,  wakati wakitoa semina ya matumizi sahihi ya kemikali ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini waliokutana jijini Dodoma.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo Mratibu wa mradi wa kudhibiti uchafuzi wa Mazingira na Afya (EHPMP), Dk Betrina Igulu,  amesema wachimbaji wadogo wengi hawana uelewa wa madhara ya kemikali ya zebaki na ndiyo maana wengi wao wameathirika na matumizi ya kemikali hiyo bila kujua.

Amesema wengi wao wanatumia kemikali hiyo bila kuchukua tahadhari zozote za kiusalama kama vile kuvaa mavazi yanayowakinga kugusana na kemikali hiyo, kuvaa glovu mikononi, barakoa na mabuti na hivyo kujikuta wanaathirika na kemikali hiyo baada ya kipindi cha muda mrefu.

“Serikali haijapiga marufuku matumizi ya zebaki kwenye migodi,  lakini inatakiwa itumike kwa tahadhari kubwa na kwa kiwango kidogo ili isilete madhara kwenye afya zenu, kwa sababu unaweza ukadhani kuwa unatafuta fedha lakini hata ukiipata usiitumie kwa raha kwa sababu unakuwa na magonjwa yanayotokana na kemikali hiyo,” amesema Dk Igulu na kuongeza:

“Pia mnatakiwa kutumia zebaki kulingana na kiwango kilichoidhinishwa na shirika la afya duniani cha asilimia 15 tu kwani tulifanya utafiti kwa kushirikiana na Wizara ya afya kwa wachimbaji wadogo wa mikoa ya Geita, Shinyanga, Mara, Mbeya na Singida ambapo tuligundua kuna matumizi makubwa ya kemikali ya zebaki hadi asilimia 60 na baadhi ya watu wameshapata magonjwa yanayotokana na kemikali hiyo.”

Amesema Nemc ina wajibu wa kulinda sheria ya mazingira ili kuhakikisha kuwa hakuna uharibifu wowote unaotokana na matumizi ya kemikali kwenye migodi ya wachimbaji wadogo na kwamba atakayebainika kuvunja sheria atafutiwa leseni yake ya uchimbaji.

Amewataka wachimbaji hao kuhifadhi kwa usalama mabwawa yanayohifadhi maji yenye kemikali ili yasilete madhara kwenye mazingira na kwenye vyanzo vya maji kwani ni hatari kwa viumbe hai.

Kwa upande wake,  Meneja wa kanda ya kati kutoka Ofisi ya mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu wa serikali, Gerald Mollel amewataka wachimbaji hao kuhifadhi na kutumia kwa usahihi kemikali zote zinazotumika migodini.

Aidha,  amesema matumizi mabaya ya kemikali hizo ni hatari kwa afya zao kwani madhara hayataonekana haraka lakini baada ya miaka 10 ndipo yatakapoanza kuonekana ikiwemo kutetemeka mikono, miguu na kichwa, ngozi kubabuka, saratani na hata kifo.

Amesema hata kama wanatafuta fedha lakini wachukue tahadhari ya kulinda afya zao ili fedha watakazozipata waweze kuzitumia kwenye malengo waliyoyakusudia badala ya kutumika kujiuguza.

“Kuna kemikali nyingine hazihitaji kugusa moto hivyo unapozitumia ni lazima usivute sigara kwani kwa kufanya hivyo utaweza kutengeneza bomu ambalo litawaathiri watu wengi bila wewe kujua hivyo kabla ya kutumia kemikali hakikisha unasoma maelekezo ya matumizi yake na namna bora ya kuzihifadhi ili zisilete madhara,” amesema Mollel

Nao baadhi ya wachimbaji wameiomba Serikali kuwaletea teknolojia mbadala ya kuchenjua madini yao badala ya kemikali ya zebaki kwani hata wakiitumia wanapata asilimia 55 tu madini wanayoyataka badala ya kuyapata yote.

Martha Mwageni amesema kama kemikali zinazotumika kwenye migodi zina madhara,  wanaomba Serikali iwapelekee mitambo yenye teknolojia ya kisasa itakayowawezesha kuboresha kazi zao badala ya kuhatarisha afya zao kwa kutumia kemikali zenye sumu.

Related Posts