Bagamoyo. Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed amesema jitihada za makusudi zinapaswa kufanywa ili kuziendeleza fursa mbalimbali za uchumi wa buluu ambao haujaangaziwa.
Amesema Serikali zote mbili za Tanzania Zanzibar, zinapaswa kuzichangamkia kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuchochea maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Dk Khalid amesema hayo leo Jumamosi, Juni 22, 2024 katika ufunguzi wa maonyesho ya Siku ya Mabaharia Duniani. Kwa Tanzania yanafanyikia Uwanja wa Nia Njema, Bagamoyo, Mkoa wa Pwani. Kilele chake ni Juni 25, 2024.
Maadhimisho hayo yameandaliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA).
Dk Khalid amesema ajenda ya uchumi wa Bluu duniani, inashika kasi lakini hapa nchini bado maeneo mengi kama ya utalii hayajatazamwa vizuri na kuwekezwa ikiwa wataalamu watavibainisha.
“Fursa zipo nyingi sana lakini kwa bahati mbaya hatujazitumia ipasavyo. Serikali zote mbili zinapaswa kuzifanyia kazi na hili linawezekana,” amesema Dk Khalid.
Ametolea mfano Zanzibar akisema watu wanajua visiwa vya Unguja na Pemba lakini kuna visiwa vingine vidogovidogo 44.
‘’ Hivi visiwa vimekaa tu lakini sasa tumeanza kuvifanyia kazi na kati ya hivyo inajengwa hoteli ya kisasa na wavuvi hawakuondoshwa bali wameboreshewa mazingira.
“Kule Pemba kuna chumba chini ya bahari, ukiwasha taa samaki wanakuja, usingizi unakuwa burudani kabisa. Na kutokana na umuhimu wa chumba kile, ukitaka kukipata unaweka oda mwaka mzima. Huu ndio uchumi wa buluu tunaoutaka,” amesema.
Amesema eneo jingine linaloweza kufanyiwa kazi ni kuangalia maunganisho ya Bagamoyo na Unguja kwa sababu ni dakika 45 tu, watalii wakafanya utalii Bagamoyo kisha wakaenda Zanzibar
“Hili nalo ni moja ya uchumi wa bluu tunaopaswa kuufanyia kazi,”amesema.
Dk Khalid amesema Meli ya MV Mapinduzi ambayo itakuwa inafanya safari zake Unguja – Pemba- Dar es Salaam na Tanga iko mbioni kuanza kazi baada ya matengenezo yake kukamilika.
Amesema hali kama hiyo iko Ziwa Victoria ambapo Serikali ya Jamhuri inaendelea kuboresha usafiri majini.
Amesema suala la usafiri majini ndio usafiri mkuu kwa sababu ndio unasafirisha mizigo kwa zaidi ya asilimia 90.
“Mathalani tulipopata tatizo la Uviko-19 mwaka 2021, meli zikashindwa kusafirisha mizigo kila mmoja alishuhudia maisha yakipanda. Kwa hiyo hii ni siku muhimu sana katika maisha ya binadamu,” amesema.
“Wenzetu mabaharia wanafanya kazi kubwa sana. Tuna kila sababu kuwashukuru na kuwapongeza. Kazi ni wito na bila ninyi hali ingekuwa ngumu sana,” amesema.
Waziri huyo amesema safari za majini zinachukua muda mrefu hivyo kuwafanya kukaa mbali na familia, watoto, ndugu, jamaa na rafiki na huko wanakutana na changamoto nyingi huko baharini.
“Kwa hiyo usalama wao ni kitu muhimu na lazima tuhakikishe tunaweka mazingira sawa kwanza wasafiri salama na wanapata haki zao zinazostahili. Serikali zote mbili zitafanya kila linalowezekana maslahi yenu yaendelea kuboreshwa,” amesema.
Amesema hilo litafanyika ili kutekeleza mikataba mbalimbali 25 ambayo nchi imeingia duniani ikiwemo mkataba wa kazi, mkataba wa kimataifa wa usalama wa maisha baharini, mkataba wa viwango vya mabaharia na mkataba wa utafutaji na uokoaji.
“Mikataba yote hii na mingine, Serikali zote mbili inazifanyia kazi kwani uchumi wetu unategemea usafiri huo,” amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amesema wanafahamu umuhimu wa maonyesho hayo.
“Nitoe rai kwa wananchi kuja kujifunza, shule kuleta wanafunzi ili kuja kujifunza na kujua kazi za ubaharia kwani msingi wake huanzia chini.”
Kunenge amesema Pwani ndio mkoa unaoongoza kwa viwanda vingi Tanzania. Mpaka sasa kuna viwanda 1,553 kati ya hivyo 124 ni vikubwa na 34 ni vipya vimejengwa hivi karibuni na vingine vinaendelea kujengwa.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), Sheikha Ahmed Mohamed amesema kila Juni 25 huwa ni siku ya mabaharia na Tanzania huanza na maadhimisho kuanzia Juni 22 kwa kutoa elimu na maonesho kwa wananchi.
Amesema katibu mkuu wa IMO amezitaka nchi mbalimbali kutambua umuhimu wa mabaharia kwani asilimia 90 ya mizigo inayosafirishwa inategemea mabaharia.
“Ni wajibu wetu kulinda maslahi ya mabaharia, kuwalinda na usalama kwani bila mabaharia hakuna usafirishaji, hakuna ununuzi,” amesema Sheikha