ANITHA; Fundi Bomba anayezitamani Simba, Yanga

LICHA ya Alliance Girls kufanya vibaya katika Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) iliyomalizika hivi karibuni kwa kushika nafasi ya tatu kutoka mkiani, ikinusurika kushuka daraja, lakini kuna baadhi ya nyota wa timu hiyo wameonyesha viwango bora kiasi cha kuanza kuwindwa na klabu kubwa za ligi hiyo.

Klabu za Simba Queens, JKT Queens na Yanga Princess zilizomaliza katika nafasi tatu za juu za ligi hiyo iliyoshuhudia Simba ikibeba taji la nne tangu kuasisiwa kwa WPL, zinatajwa kuanza harakati za kusaka saini na baadhi ya nyota wa Alliance Girls akiwamo Mkenya Anitha Adongo.

Anitha ndiye nahodha wa Alliance anatajwa kuwa miongoni mwa  wachezaji wanaowindwa na klabu hizo kubwa wakati dirisha dogo likiwa wazi tangu Juni 15 kutokana na kiwango bora alichokionesha.

Mwanaspoti ambalo limekuwa bega kwa bega na Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) limefanya mahojiano na beki huyo juu ya ishu ya usajili na maisha yake kwa ujumla, naye amefunguka na msimamo wake akidai kwa vile yeye ni mchezaji, haoni tatizo kutua kokote, yaani ye ni kambi popote tu. Endelea naye…

“Ni mchezaji huru kwa sasa, sina mkataba na Alliance kwani uliokuwapo umemalizika, hivyo kama Simba na Yanga zinanihitaji huduma yangu  basi tukae na kuzungumza,” anasema Anitha ambaye ni Mkenya aliyetua nchini tangu mwaka 2019 akisajiliwa na wakali hao wa soka la Wanawake kutokea Jijini Mwanza.

Akiwa na uzoefu wa misimu karibu mitano, Anitha anasema licha ya kuitumikia Alliance bado malengo aliyonayo katika soka la Wanawake hayajatimia, kwani ndoto kuu aliyonayo ni siku moja kucheza Hispania.

Anitha alijiunga na Alliance baada ya kuwasha moto katika Ligi Kuu ya Kenya akiwa na timu kadhaa ikiwamo Vika Queens na Kisumu Queens, hivyo ni mzoefu wa soka hilo na kiu kubwa ni kuvuka mipaka ya Afrika baada ya awali kuivuka ile ya kwao Kenya kuja Tanzania kukiwasha.

Anitha alisema hakuna mchezaji asiyependa kucheza timu kubwa na zenye mashabiki kama Simba na Yanga, hata kama ni za wawanake, lakini zinaungwa mkono na hata akiwa Alliance alikuwa akiona ukubwa wa timu hizo wanapovaana nao kuanzia ndani na nje ya uwanja na anatamani itokee ajiunge na timu mojawapo.

HEKAHEKA ZA KUSHUKA DARAJA

Hadi raundi ya mwisho ilikuwa inaamua timu gani inashuka daraja kutokana na kulingana pointi, Baobab Queens na Alliance Girls kila moja ilikuwa na 13, ila zilitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa na kama zali mechi za mwisho ambazo kila moja ilipoteza, ziliamua kwa Baobab kushuka na Alliance kusalimika.

“Kwanza tumshukuru Mungu kwa kubaki Ligi Kuu, mchezo wa mwisho ndio ulikuwa unaamua nani abaki nani ashuke na sisi tulikuwa tunacheza uwanjani huku tuna presha jambo lilikuwa gumu sana kwa upande wetu,” anasema Anitha.

Anaongeza ukiachana na changamoto mbalimbali walizopitia msimu huu hususani ya kuwa na kikosi kikubwa cha vijana ambao hawajapata uzoefu anaamini msimu ujao utakuwa tishio kwa upande wao.

“Wachezaji wengi wenye uzoefu waliuzwa kwenye timu kubwa nafikiri pia ni sababu ya sisi kutofanya vizuri sana kwa sababu wale waliocheza wengi wametoka mashuleni hawana ukomavu wa ligi lakini kwa sasa naamini wamepata joto kidogo la ushindani.”

Katika mechi hizo za mwisho za WPL, Alliance ilifungwa bao 1-0 na Yanga huku Amani Queens ikaishindilia Baobab mabao 5-0 yaliyoisukuma hadi nafasi ya tisa na kuungana na Geita Queens iliyozabuliwa na Simba kwa mabao 3-0.

JKT Queens iliishinda Ceasiaa Queens kwa mabao 2-0 na Fountain Gate Princess iliizamuisha Bunda Queens kwa bao 1-0.

Mkenya huyo anasema Kenya alikotokea kuna changamoto kubwa ya ukata wa fedha kuanzia kulipa mishahara wachezaji au posho na hata mashabiki hakuna wa kusapoti soka la wanawake.

“Yaani Tanzania iko tofauti mashabiki wengi wanapenda soka hasa kwa timu za kiume lakini kwa sasa hata wanawake wanakuja uwanjani na kusapoti sio jambo dogo tofauti na Kenya,” anasema Anitha na kuongeza

“Kenya uwanja uko kimya hakuna hata mashabiki wanaokuja kusapoti soka la kike angalau sasa hivi kidogo wanajitahidi muda mwingine uwepo wao uwanjani unatupa motisha.”

Juu ya soka la wanawake Kenya na Tanzania lipi linalolipa, Anitha hakumumunya maneno kwa kusema wazi;

“Ni kweli soka la Kenya halilipi tofauti na Tanzania ambapo angalau hata posho wachezaji wanapewa na kuendesha maisha yao kama kawaida. Na ndio sababu inayowafanya Wakenya wengi kukimbilia Bongo kwa ajili ya kupata pesa za kujikimu na hata kama hakuna mshahara kuna posho wapatazo zinawapa motisha ya kuendelea kucheza.”

Anitha anafichua kuwa, mbali na kucheza soka lakini yeye ni msomi wa Stashahada (Diploma) akisomea na kuhitimu kozi ya ufundi wa mabomba ya maji.

“Maisha ya soka ni mafupi nimefikiria nikistaafu niwe na shughuli ya kufanya hivyo nikasomea kozi hiyo na nilihitimu 2018 kwetu Kenya,” anasema Adongo anayekiri wazazi wake ni wakali, lakini linapokuja suala la ndoto yake kisoka wanakuwa watu wa kwanza kusapoti kwa asilimia kubwa.

“Wazazi wangu ni wakali sana, ndio maana sitaki kuwaangusha hata nilipokuwa mdogo nilipambaniwa kucheza mpira na kusoma vyote kwa wakati mmoja na wamekuwa wakiniunga mkono kila uchao.”

Anasema pesa kubwa aliyowahi kuipata tangu acheze soka ilikuwa mwaka 2017 walipocheza mchangani na kufanikiwa kupewa zawadi ya Sh 150 za Kenya ( ambazo ni sawa na Sh 2 milioni za Kitanzania)

“Ile pesa niliyopata nikampatia mama yangu mzazi ambayo namshukuru akafanyia jambo kubwa la kuendeleza biashara yake ambayo hata kikienda sasa hivi nyumbani najivunia hilo.” 

Anasema kucheza mpira haimfanyi mtu kukosa ama kuanzisha familia kwa kuwa ni kazi kama kazi zingine ambazo wanawake wanafanya utofauti wale wachezaji ni mazoezi tu.

“Natamani nikimaliza maisha ya soka basi na mimi nianzishe familia kwa kuwa hakuna kitu kitanizuia mimi ni mwanamke kama wengine tu.”

Nyota huyo alipoopatakiwa kukipanga kikosi bora za WPL kwa msimu wa 2023/2024 alikianika hivi;

Kipa Carolyne Rufaa (Simba), mabeki Elizabeth Msukuma, Winkate Kaari (Yanga), Ruth Ingosi (Simba), Anitha Adongo (Alliance), huku viungo wakiwa ni Vivian Corazone (Simba), Winifrida Gerald (JKT Queens), Donisia Minja (JKT Queens), Stumai Abdallah (JKT Queens) na Asha Djafar (Simba Queens), huku mshambuliaji akiwa ni Aisha Mnunka (Simba Queens).

Related Posts