Dar es Salaam. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa amewataka Watanzania kukemea vitendo vya mauaji ya watu wenye ualbino akisema havikubariki katika karne ya sasa yenye mwanga.
Kauli hiyo ya Askofu Malasusa inatokana na kile kilichotokea Mei 30, 2024 cha mtoto Asimwe Novath (2) mwenye ualbino, kuporwa mikononi mwa mama yake na watu wasiojulikana nyumbani kwao Kijiji cha Mulamula, wilayani ya Muleba, Mkoa wa Kagera.
Mwili wa Asimwe ulipatikana Juni 17, 2024 kwenye kalavati katika barabara ya Luhanga wilayani humo, huku baadhi ya viungo vikiwa vimenyofolewa. Tayari mwili huo umeshazikwa na watu tisa wanashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.
Askofu Malasusa ametoa wito huo leo Jumapili, Juni 23, 2024 wakati akizindua ofisi ya Upendo Media zilizopo katika Kanisa la KKKT Usharika wa Kinondoni na kuzitaka ofisi zitumike kupeleka habari njema na zenye usahihi kwa Watanzania.
Mkuu huyo wa KKKT, ametoa wito wakati akikagua studio za kisasa za Upendo Media ambapo amesema:”Tunaungana na Watanzania kuhusu tukio hili, tumehuzunika sana. Bado katika karne hii au miaka 2000 ya Yesu kuleta nuru lakini bado kuna watu wanaishi katika giza.”
“Tumeambiwa maisha yake yameondolewa kwa sababu ya watu wanaofikiria zipo nguvu za giza zinazoweza kuwasaidia katika maeneo mbalimbali, hatujui katika maeneo yapi kama biashara, kilimo au kuchaguliwa lakini ni nguvu za giza,” amesema Askofu Malasusa.
Kutokana na hilo, Malasusa ambaye ni pia ni Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Pwani, amewaomba Watanzania na waumini wa dini hiyo kuvikemee vitendo hivyo ambavyo havileti taswira nzuri katika Taifa.
“Tuwaombea mama au mzazi wa binti (Asimwe) ambaye ameuawa kikatili ili Mungu awajaze amani.
“Tumesikia hata walioshiriki na kukamatwa ni watu wanaomjua Mungu, tulitarajia wapeleke habari njema lakini bado tunarudi nyuma. Ndugu zangu habari njema hatutakiwi kusimama, bali kila wakati kupeleka habari njema ili Taifa na ulimwengu kuwe mahali pa amani,” amesema Dk Malasusa.
Kuhusu studio hizo, Askofu Malasusa amesisitiza zitumike kupeleka habari njema zitakazowaondoa watu katika fikra potofu zinazowafumbua baadhi ya wananchi wanaokwenda kuua watu wenye ualbino kwa sababu ya utajiri au jambo lolote ambalo halikubariki katika karne hii baada ya nuru kuwepo.
Katika hatua nyingine, kiongozi huyo wa kiroho amewapongeza Bakari Machumu, Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), na Frank Sanga, Mkurugenzi Mtendaji wa UTV kwa ushirikiano wao katika sekta ya habari na Upendo Media.
“Ninyi (Sanga na Machumu) mmedhihirisha umma wa Watanzania kwamba mpo makini katika sekta ya habari na sisi (Upendo Media) tunataka kufika huko hivyo msituache wote tunafanya kazi moja ya kumhudumia binadamu kupata habari njema zitakazomsaidia katika maisha,” amesema Dk Malasusa.
Naye, Machumu ameipongeza Upendo Media kwa hatua walizopiga za kufungua studio za kisasa akisema uwekezaji huo unatia moyo hasa wakati huu ambao vyombo vya habari duniani vinapita katika misukosuko mikubwa.
“Tunawashukuru Upendo kwa ushirikiano wao na kufanya kazi pamoja kwa miaka 10, naimani tutaendelea kufanya hivyo. MCL tunaamini katika mashirikiano ya vyombo vya habari ili kusonga mbele zaidi,” amesema Machumu.
Kwa upande wake, Sanga ameungana na Machumu kuipongeza Upendo Media kwa hatua hiyo ya uwekezaji huo hasa katika kipindi hiki.